1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vitisho vya kushambuliwa Syria vinazidi makali

Oumilkheir Hamidou
11 Aprili 2018

Maamizio yanayokinzana ya Marekani na Urusi kuhusu nani wa kubebeshwa jukumu la mashambulio ya gesi za sumu nchini Syria yameshindwa kuungwa mkono katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/2vqyZ
Syrien Mutmaßlicher Giftgasangriff in Duma
Picha: Reuters/White Helmets

Malumbano kati ya Marekani na Urusi kuhusu mzozo wa Syria yamezidi makali: Moscow mshirika asiyetetereka wa Damascus imetumia kura ya turufu jana katika baraza la usalama kupinga mswaada wa azimio uliopendekezwa na Marekani kwa lengo la kubuni mkakati wa uchunguzi huru kuhusu matumizi ya gesi za sumu nchini Syria.

Katika baraza la usalama mapendekezo mawili ya maazimio yaliwasilishwa na Urusi nayo pia hayakupata uungaji mkono wa kutosha.

Balozi wa Urusi katika umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia amesema kura ya turufu ya Urusi, ya 12 katika kipindi cha miaka saba, katika ugonvi ulioangamiza maisha ya watu zaidi ya 350.000, imelengwa kuzuwia "baraza la usalama lisitoswe katika hatari." "Mngepitisha uamuzi wa kujitosa katika shambulio haramu la kijeshi, basi wenyewe mngebeba dhamana ya yatakayotokea. Mnachojaribu kufanya  ni kiisingizio cha kufikisha mswaada wa azimio mbele ya baraza la usalama ili kutekeleza mpango wa muda mrefu. Mmeshasema mara kadhaa ikiwa baraza la usalama halitaamua, mtapitisha uamuzi wenu wenyewe. Kwanini mnajaribu kudharau madaraka ya baraza la usalama kwa kupitisha mswaada ambao tokea hapo mnatambua hautoungwa mkono? Amesema balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki HaleyPicha: picture-alliance/dpa/AA/A. Ozdil

Nchi za magharibi zinajiandaa kwa mashambulio dhidi ya Syria

Nchi za magharibi, zikitanguliwa na Marekani na Ufaransa zinaeneza kitisho cha kufanya hujuma za kijeshi dhidi ya serikali ya mjini Damascus."Ufaransa itafanya kila liwezekanalo kujibisha shambulio la gesi za sumu" amesema balozi wa Ufaransa katika Umoja wa mataifa Francois Delattre. Rais Emmanuel Macron alisema kwa upande wake uamuzi utapitishwa siku chache zinazokuja baada ya mashauriano pamoja na Marekani na Uingereza.

Rais wa Marekani Donald Trump ameshasema watajibisha wakati wowote ule kutoka sasa kufuatia madai ya shambulio la gesi ya sumu linalodaiwa kufanyika katika mji wa Douma katika Ghouta ya mashariki na kuangamiza maisha ya watu wasiopoungua 40.

Manuari ya kivita ya marekani USS Donald Cook imeshaondoka katika bandari ya Cyprus ya Larnaca na kuelekea katika eneo la bahari karibu na Syria. Nalo shirika la Ulaya linalosimamia  usalama wa angani limeonya dhidi ya hatari ya kutokea mashambulio ya angani nchini Syria katika kipindi cha masaa 72 yanayokuja.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassili Nebensia
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassili NebensiaPicha: picture alliance / Julie Jacobson/AP/dpa

Urusi inasema shambulio lolote litajibiwa

Vikosi vya Syria vimewekwa katika hali ya tahadhari huku ikulu ya Urusi Kremlin ikitahadharisha hawatovumilia shambulio lolote dhidi ya Syria.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef