1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viwanjani wiki hii

Ramadhan Ali29 Juni 2007

Copa America linaendelea huko Venezuelabaada ya Brazil kulazwa 2:0 na Mexico.Shule ya chipukizi ya dimba nchini Senegal na jinsi nahodha wa Ufaransa Patrick Vieira anavyoendeleza vipaji huko. dada 2 serena na Venus william wamerudi Wimbledon katika medani ya Tennis.

https://p.dw.com/p/CHbq

Wakati timu za bara la Asia zinajiandaa kwa kombe la Asia,kinyan’ganyiro cha Copa America-kombe la Amerika kinaendelea nchini Venezuela ambako wenyeji hao jana walirudi uwanjani kwa mpambano wao wapili na Peru.

Venezuela ilimudu suluhu tu nyumbani 2:2 ilipofungua dimba wakati Peru, ilianza kwa vishindo kwa kuitimua Uruguay,mabingwa wa kwanza kabisa wa kombe la dunia la FIFA kwa mabao 3:0.

Mstuko ilipata Brazil ilipozabwa katika mpambano wake wa kwanza mabao 2:0 na Mexico.Hatahivyo, kocha wao Dunga anadai kuteleza sio kuanguka.Kabla pigo hilo,Brazil ilimudu suluhu tu 0:0 na uturuki katika mpambano wa kirafiki hapo juni 5.Hatahivyo, Dunga aliungama kwamba hakulala usingizi baada ya pigo kutoka vigasnja vya Mexico.Haya ni mashindano ya kwanza makubwa kwa Dunga akiwa kocha wa Brazil.

Dunga utakumbuka alishika hatamu za timu ya Brazil baada ya Kombe la dunia hapa Ujerumani 2006 akimtua mzigo kocha wa sasa wa Afrika Kusni-Carlos Parreira.

Paraguay pia ilivuma kwa kishindo katika Copa America pale mshambulizi wa Bayern Munich, Roque Santa Cruz alipokomea mabao 3 pekee katika ushindi wa mabao 5-0 katika lango la Colombia.

Argentina wanaopigiwa upatu kutwaa ubingwa mara hii nusra wakione kilichomtoa kanga manyoya.ilikuwa Marekani iliotangulia kuufumania mlango wake,lakini waargentina wakadai kutangulia si kufika.Mwishoe, wakaondoka na ushindi wa mabao 4-1 la Marekani.

FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni limeregeza kamba kati ya wiki hii baada ya rais wa Bolivia Morales kucheza dimba na rais wa FIFA Sepp Blatter huko Uswisi-makao makuu ya FIFA.

Sasa FIFA itaruhusu mechi za kimataifa kuchezwa kwenye uwanja wa mpira wa La Paz,mji mkuu wake uliopo mita 3.000 kutoka upeo wa bahari.

Hapo kabla, FIFA iliamua kuwa mechi zote katika viwanja viliopo zaidi ya mita 2.500 kutoka upeo wa bahari ni marufuku.Hii ikazusha vilio kutoka nchi za mlima Andeas na rais Evo molars-shabiki wa dimba binafsi na mchezaji akateremka uwanjani kuonesha hakuna dhara yoyote kucheza dimba katika hali kama hiyo.

Baadae rais wa Bolivia, akafunga safari hadi Zurich,makao makuu ya FIFA ili kuonana na Sepp Blatter aliefuta amri ya hapo kabla ya FIFA.

Dibaji ya kombe la dunia la chipukizi chini ya umri wa miaka 20 imetoka:

Afrika itawakilishwa na timu kutoka Zambia,Kongo,Nigeria na Gambia:Zambia itakua kesho uwanjani ikicheza katika kundi A na Jordan.

Nigeria ina miadi na Costa Rica keshokutwa Julai 2.Kongo inacheza kesho na Austria wakati Gambia ina miadi na Mexico.

CHUO CHA DIMBA -Diambars Academy.

Shule hii ilianzishwa miaka 4 iliopita na Patrick Vieira nahodha wa Ufaransa na wenzake ili kuwafunza mastadi wa kesho wa Afrika ili kama Vieira mwenyewe wajikomboe kutoka hali ya umasikini na kufuata nyayo za mastadi kama yeye.

Azama ya Diambars Academy pia ni kuwaandaa mastadi wa Afrika magharibi wa siku zijazo-mastadi watakaofuata nyayo za akina Samuel Eto ò wa Kamerun, Didir Drogba wa Ivory Coast au Michael Essien wa Ghana.Wachezaji kama Samuel Eto’o na Vieira wanapiga vita pia ubaguzi katika dimba na hasa barani Ulaya.

Vieira amewaambia chipukizi hao na ninamnukulu,

“Huwezi kuchukulia tu mambo yatakua mazuri.Lazima ujitolee na kupigania kile utakacho na ujiamini.”

Akaongeza Vieira kusema:

“Sisi sote tuna jukumu-wachezaji kutoka Afrika waliofaulu kama mimi wanapaswa kurejea Afrika na kuwasaidia chipukizi kutimiza ndoto zao.”

Kinyume na vyuo vyengine vya dimba vinavyochipuka kila kukicha barani Afrika,chuo cha Diambars kinalenga sio tu kuwajenga wachezaji hodari wa soka, bali pia wanabeki,wataalamu wa majenzi ya majumba na wahandisi-kinalenga kuwaandaa vijana kuwa na maisha bora kikazi endapo ndoto zao za kuwa wachezaji mashuhuri hazikutimilia.

Madarasa yake chuo hiki huko nchini Senegal ni safi kabisa na kuna wanafunzi 87.Kujipatia nafasi katika chuo hiki ni kukimbia maskani ya madongo-poromoka ya umasikini.

Katika bara ambamo zaidi ya thuluithi-mbili ya watoto hawana elimu ya kimsingi,chipukizi katika chuo hiki cha akina Patrick Vieira na wenzake kinanoa siku zao bora za usoni.

Miaka 4 iliopita,Ali Sileymane Ly, akitumia ustadi wake wa kucheza dimba akiomba fedha mitaani kwaajili ya ujenzi wa shule ya Koran. Sasa akiwa na umri wa miaka 17, anakichapa barabara kingereza na kifaransa na anajua sasa kutumia komputa.

Kila kitu chazunguka juu ya mpira –asema Vieira ,kwani wanatumia mpira kuendeleza elimu.kwani, anaelewa kwamba elimu ndio ufunguo kwa maisha.

Patrick Vieira, alianzisha shule hii 2003 kwa ubia na kipa wa zamani wa Ufaransa Bernard Lama aliewahi kwa muda mfupi, kuwa kocha wa Harambee Stars-timu ya taifa ya Kenya.Mwengine, ni Jimmy Adjovi-Boco. Kuna mpango wa kufungua shule zaidi za aina hii katika pembe mbali mbali barani Afrika.

Patrick Vieira ingawa ni raia wa Ufaransa, ni shujaa anaependwa na nchi yake ya asili Senegal.Akipita huko mwambao wa pwani wa Senegal wa Saly ambako chuo hicho ndiko kilipo,watu humuita “Vieira, Vieira.”

TUMALIZIE TENNIS WIMBLEDON:

Wakati bingwa upande wa wanaume mswisi Roger Federer alikumbana jana na changamoto yake kali kabisa hadi sasa alipokutana na mrusi Marat Safin katika duru ya tatu ya mashindano haya, dada wawili upande wa wanawake-Serena na Venus Williams walirejea kwa pamoja uwanjani kuania tena taji la wimbledon na kujaribu kutoroka nalo tena.

Ikiwa hii ni mara ya kwanza kucheza tena kwa pamoja katika mashindano haya tangu 2003 Serena na Venus waliwashinda maadui zao akina Claire Curran na Anne Keothavong wa Uingereza kwa seti 6-1 na 6-3.

Baadae Venus akakutana na Akiko Morigama ili kupanga miadi na bingwa wa 2004 Maria Sharapova wa Russia.

Dada Serena na Vinus walitwaa 2000 na 2002 ubingwa wa wimbledon wa wachezaji 2-2.