1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky kuingia duru ya pili ya uchaguzi na Poroshenko

Amina Mjahid
1 Aprili 2019

Shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE limesema uchaguzi Ukraine ulisimamiwa vizuri. Matokeo ya mwanzo yanamuonesha mchekeshaji Volodymyr Zelensky kuwa mshindi wa duru ya kwanza ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3G2h6
Ukraine Präsidentschaftswahl 2019 | Wolodymyr Selenskyj, Kandidat
Picha: Getty Images/B. Hoffman

Mratibu maalum wa shirika hilo la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE Ilkka Kanerva amewaambia waandishi habari  kwamba wapiga kura nchini Ukraine walikuwa na sauti kubwa na walijitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo uliofanyika jana jumapili.

Mchekeshaji ambaye hana uzoefu wa kisiasa Volodymyr Zelensky amechukua ushindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais na kuonesha mwanzo mpya wa kisiasa kwa wapiga kura waliochoshwa na ufisadi katika taifa hilo lililoko katika msitari wa mbele likiungana na mataifa ya Magharibi kuipinga Urusi.

Ukraine Präsidentschaftskandidat Wolodymyr Selenskyj
Mchekeshaji/Mgombea urais nchini Ukraine Volodymyr Zelensky Picha: AFP/S. Supinsky

Huku robo tatu ya kura zikiwa tayari zimehisabiwa hii leo Volodymyr Zelensky aliye na miaka 41 ambaye anaigiza kama rais wa maigizo katika filamu maarufu katika runinga nchini humo alishinda zaidi ya asilimia 30.5 ya kura.

Hali hii inamuacha rais Petro Poroshenko kuchukua nafasi ya pili akiwa na asilimia 16.6 ya kura, pengo ambalo ni kubwa kuweza kumfikia mpinzani wake.

Poroshenko kwa sasa anakosolewa vikali nchini mwake kwa kukosa kukabiliana na ufisadi na kukosa kuimarisha hali ya maisha miaka mitano baada ya  viktor Yanukovych alipoondolewa madarakani kupitia maandamano.

Waziri Mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko amechukua nafasi ya tatu katika uchaguzi huo akiwa na asikilia 13.2 ya kura katika uwanja mkubwa wa mapambano wa wagombea 39 katika uchaguzi huu wa urais nchini Ukraine.

Duru ya pili ya uchaguzi kufanyika baada ya wiki tatu zijazo

Kwa sasa mchekeshaji Zelenskiy na Petro Poroshenko watapambana tena katika duru ya pili ya uchaguzi wiki tatu zijazo. Zelenskiy amekuwa akikosolewa kuwa na msimamo mwepesi katika masuala ya sera huku hotuba yake ya ushindi aliyoitoa hapo jana ikikosa kuelezea zaidi kile atakachokifanya baada ya kuchukua ushindi kamili.

Bildkombo Petro Poroshenko und Volodymyr Zelenskyi
Rais Petro Poroshenko na mchekeshaji Volodymyr Zelenskyi

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa Ukraine wamekuwa na maoni tofauti juu ya wagombea waliochukua ushindi wa mwazo katika duru ya kwanza ya uchaguzi. Anton mkaazi wa Kiev anasema hakutarajia mchekeshaji Volodomyr Zelenskiy kuchukua ushindi huku wengine wakisema wanaamini matokeo hayo maana kura ya maoni awali ilikuwa tayari imeshatabiri hilo.

Poroshenko, rais anayetetea kiti chake aliye na miaka 53 alimshambulia Zelenskiy akisema hayuko makini na ni chaguo baya wakati huu ambapo taifa lipo vitani na watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo