1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa NCP na SPLM waafikiana kukubali matokeo.

21 Aprili 2010

Makamu wa pili wa rais, Ali Osman Taha wa NCP akutana na Salva Kiir wa SPLM.

https://p.dw.com/p/N1tI
Bendera ya Sudan. Uchaguzi uliokamilika ulikuwa wa kwanza tangu 1986.Picha: AP

Makamu wa pili wa rais nchini Sudan, Ali Osman Taha alisema katika taarifa kwenye televisheni ya serikali kwamba wameafikiana na viongozi wa kusini kukubali matokeo kama yatakavyotangazwa na tume ya uchaguzi na pia kuheshimu uamuzi wake.

Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi huo wa kwanza wa vyama vingi nchini humo tangu mwaka wa 1986 bado linaendelea. Wapiga kura milioni 16 waliojiandikisha walikuwa na fursa ya kumchagua rais, wabunge na viongozi wa mabaraza mikoani. Raia wa kusini mwa Sudan pia walipiga kura kumchagua kiongozi eneo la kusini.

Rais Al-Bashir anatarajiwa kushinda kwa kishindo baada ya wapinzani wake kususia uchaguzi huo lakini uchaguzi wa wabunge na viongozi wa mashinani ulikuwa na wagombeaji wengi katika nchi hiyo kubwa zaidi barani Afrika.

Sudan Wahlen Omar al-Bashir
Rais Omar al-Bashir atarajiwa kushinda kwa kishindo.Picha: AP

Yasser Arman aliyekuwa mgombeaji wa urais wa chama cha SPLM kabla ya kujiondoa, alihudhuria mkutano kati ya Taha na Salva Kiir licha ya shutuma zake siku ya jumatatu kwamba chama tawala cha National Congress kilikuwa kinapanga kuiba kura katika jimbo la Blue Nile mpakani mwa kaskazini na kusini.

Bw. Taha alisema pande zote mbili zilikubaliana pia kuharakisha na kutekeleza vipengee, hasa suala la mpaka, katika makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2005 na yaliositisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kaskazini na kusini.

Suala la mpaka kati ya kaskazini na kusini lina uzito zaidi kabla ya kura ya maoni inayotarajiwa kufanywa mwaka ujao kuhusu mustakbali wa eneo la kusini kama linataka kujitenga au kubakia sehemu ya Sudan.

Sudan Wahlen Kandidat Salva Kiir
Salva Kiir Mayardit, kiongozi wa Sudan kusini aliafikiana na makamu wa pili wa rais wa Sudan, Ali Osman Taha kukubali matokeo ya uchaguzi.Picha: AP

Taarifa ya Ikulu ya Marekani kuhusu uchaguzi huo ilisema kuwa haki ya kisiasa na uhuru wa raia haukuzingatiwa katika uchaguzi huo na pia machafuko katika eneo la Darfur hayakuruhusu kuwepo kwa mazingira mazuri ya uchaguzi wa haki.

Taarifa hiyo pia ilisema kwamba wachunguzi wa kimataifa walithibitisha uchaguzi huo haukufikia kiwango cha kimataifa lakini ilisifu raia wa Sudan kwa kuzingatia uchaguzi wa amani. Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Robert Gibbs alisema maandalizi duni ya uchaguzi huo yalisababisha udanganyifu mkubwa.

Siku ya Jumatatu wiki hii, shirika la Kimarekani la Enough Project lilituma picha kwenye mtandao wa Youtube iliyoonyesha karatasi za kura zikishindiliwa katika sanduku la kupigia kura. Hata hivyo Hadi Ahmed, afisa wa ngazi ya juu katika tume ya uchaguzi nchini Sudan alitupilia mbali picha hiyo akisema ni ukarabati tu wa kiteknolojia.

Wachunguzi wa kisiasa nchini Sudan wanadai kuwa rais Al-Bashir alinuia kutumia fursa ya uchaguzi huo kuhalalisha uongozi wake hasa baada ya mahakama kuu ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kumtaka ajibu mashtaka ya uhalifu wa kivita na dhidi ya binaadamu katika jimbo la Darfur. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba watu laki tatu wamepoteza maisha yao katika jimbo hilo tangu vita vianze mwaka wa 2003.

Mwandishi, Peter Moss/ AFP

Mhariri, Abdulrahman Mohammed