1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyombo vya habari mashakani Uganda

Sylvia Mwehozi
3 Oktoba 2017

Wanahabari nchini Uganda na vyombo wamo katika mashaka makubwa kufuatia wimbi la vitisho na kamatakamata kufuatia vurugu kuhusu kubadilisha katiba ya nchi ili kuondoa kipengee cha ukomo wa umri wa mgombea urais.

https://p.dw.com/p/2l9ob
Uganda Hetzkampagne gegen Homosexuelle Zeitung stellt Schwule an den Pranger
Picha: AP

Hali hii imefuatia mabishano na vurugu kuhusu kubadilisha katiba ya nchi ili kuondoa kipengee cha ukomo wa umri wa mgombea urais ambapo maafisa wa vyombo vya usalama wameshuhudiwa kuzuia vifaa vya wanahabari pamoja na tume ya mawasiliano kuandikia vyombo vya habari vikiamrishwa kutotangaza habari za wanasiasa wa upinzani au kuwalika wajadili hewani.

Wiki iliyopita baadhi ya wanahabari waliokuwa wakiripoti moja kwa moja kuhusu makabiliano kati ya askari wanaodaiwa kuwa wa kikosi cha ulinzi wa rais na wanasiasa wa upinzani walikamatwa na kuzuiliwa kwa muda huku vifaa vyao vikitwaliwa. Haya yote yalitendeka maeneo ya jengo la bunge.

Waliachiwa na kupewa vifaa vyao baada ya masaa kadhaa hivyo hawakuweza kuwasilisha habari hizo wakati wa taarifa za habari kwenye vyombo vyao mbalimbali. Mwenendo huu wa kuwatatiza wanahabari katika kuendesha shughuli zao umeendelea hii leo walipokuwa wakifuatilia visa mbalimbali vya kuwazuia wanasiasa wa upinzani kufanya maandamano. Ijapokuwa wanahabari wengine sasa wanahofia maisha yao, baadhi yao wameapa kuendelea kuwapasha wananchi habari kuhusu yale yanayoendelea.

Uganda Razzia Medien Protest
Waandishi wa habari wa gazeti la Daily Monitor wakiandamana kulaani kufungiwa kwa ofisi zao na serikali ya Uganda Mei 2013.Picha: Reuters

Wakati huo huo wamiliki na wasimamizi kadhaa wa vyombo vya habari wameelezea kupokea maagizo kutoka tume ya mawasiliano UCC ikiwatahadharisha dhidi ya kuwaalika wanasiasa Fulani wa upinzani kushiriki kwenye mijadala inayorushwa hewani moja kwa moja. Hali kama hii imewatia wasimamizi hao katika mashaka makubwa wakiwa hawajui jinsi ya kutoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusu vitisho vya kufungiwa iwapo watakiuka maagizo hayo.

Juhudi za kupata ufafanuzi zaidi kutoka  tume hiyo UCC au kutoka kwa msemaji wa serikali zimegonga mwamba kila upande ukisema kwamba ufafanuzi rasmi utatolewa na pia kukanusha madai kuwa wanahabari wanazuiliwa kuafanya kazi yao.

Huku mazingira ya kufanya kazi yakizidi kuwa magumu kwa wanahabari, polisi inachunguza visa vya magurunedi kulipuka kwenye makazi ya wabunge watatu wa upinzani.Polisi imethibityisha kwamba vilipuzi hivyo ni gurunedi. Wakati huo huo, mswaada wa kuondoa ukomo kwa umri wa rais ulipangiwa kusomwa rasmi kwa mara ya kwanza bungeni licha ya wabunge wa upinzani kuendelea kususia vikao.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.

Mhariri:Yusuf Saumu