1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZEC, UNDP 'zawanoa' waandishi kwa uchaguzi

Salma Said25 Septemba 2015

Vyombo vya habari visiwani Zanzibar vimetakiwa kuheshimu na kufuata sheria, miongozo na maadili ya kazi zao ili kuepusha nchi kuingia katika machafuko katika wakati ambapo uchaguzi unakaribia.

https://p.dw.com/p/1GdR7
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Salim Kassim.
Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Salim Kassim.Picha: DW

Ushauri huo ulitolewa na wataalamu wa habari walioshiriki mkutano wa siku moja uliotayarishwa kwa ushirikiano kati ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), visiwani Zanzibar.

Afisa Habari wa ZEC, Salha Mohammed Ali, alisema katika uchaguzi wa 2010 "baadhi ya vyombo vya habari vilitangaza matokeo kabla ya wakati" na hivyo ili kuepusha hilo wameona waanze mapema kutoa muongozo.

Akiwasilisha mada ya "Maadili ya Vyombo vya Habari vya Elektroniki na Magazeti" katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Chande Omar, alisema ni muhimu kwa waandishi wa habari "kufuata maadili ya kazi zao ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza kufuatia taarifa zao."

Mkurugenzi huyo wa aliwataka wahariri kuheshimu maadili na kuzingatia kwamba hali ya nchi itakapochafuka wao watakuwa ni miongoni mwa waliochangia kuichafua.

Masanduku ya kupigia kura visiwani Zanzibar.
Masanduku ya kupigia kura visiwani Zanzibar.Picha: AP

Deodatus Balile, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, katika mada yake isemayo "Kujenga Uaminifu wa Vyombo vya Habari Wakati wa Uchaguzi" alisema wapo baadhi ya wahariri wamekuwa wakifanya upendeleo kwa makusudi "ili wagombea wao washinde lakini wanapaswa kufuata miiko ya kazi zao.

Licha ya semina, makongamano miongozo ya mara kwa mara kuvikumbusha vyombo vya habari kutenda haki na kufuata maadili, bado kampeni za mwaka huu zinaendelea kushuhudia upendeleo au chuki za wazi wazi kwenye vyombo vya habari vya umma, hasa kupitia kutoa ama kunyima fursa kwa wagombea katika kutoa taarifa zao.

Tayari Mamlaka ya Mawasiliano ya Tanzania (TCRA) imewahi kutoa karipio kali kwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambalo televisheni yake ilitajwa kuwa kwenye mkumbo huo.

Baraza la Habari Tanzania (MCT) ni miongoni mwa wafuatiliaji wa vyombo vya habari juu ya mwenendo wa kuripoti taarifa za uchaguzi na meneja wake kwa upande wa Zanzibar, Suleiman Seif, aliiambia DW kwamba vyombo vya habari vinahitajika kufanya zaidi ya kile vinachokifanya sasa ikiwa kweli vinataka kuwa sehemu sahihi ya demokrasia ya nchi.

Akielezea uzoefu wa Kenya katika mada "Yanayochochea Machafuko na Fujo Wakati wa Uchaguzi", mtaalamu wa uchaguzi kutoka shirika la UNDP, Bi Hamida Kitwana, alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuweka hali ya amani "iwapo tu vitatekeleza wajibu wake wakati wote wa uchaguzi."

Lakini akatahadharisha iwapo vyombo vya habari vitaharakisha kutoa matokeo kabla ya kutangazwa na Tume, vinaweza kuchochea vurugu kama ilivyotokea katika nchi nyengine.

ZEC imekuwa ikifanya semina mbalimbali kwa wadau wa uchaguzi, wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini na waandishi wa habari, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kufahamu wajibu unaowakabili katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Uchaguzi wa mwaka huu unaofanyika tarehe 25 Oktoba unatajwa kuwa na ushindani mkubwa zaidi kuliko nyengine nne zilizofanyika huko nyuma, sio tu kwa sababu ya wagombea maarufu wanaowakilisha kambi zote mbili - utawala na upinzani, bali pia kwa muamko wa wananchi, hasa vijana, na uwepo wa vyombo vipya vya mawasiliano kama vile mitandao ya kijamii na simu za mikononi.

Mwandishi: Salma Said/DW Zanzibar
Mhariri: Mohammed Khelef