1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafrika 100 Waandamana nchini China.

17 Julai 2009

Masharti ya kupata Visa ya China kwa Waafrika yamelegezwa

https://p.dw.com/p/IrU7
Askari wa ChinaPicha: AP

Uhusiano wa Kibiashara kati ya China na Afrika umeendelea kuimarika, huku kukiwa na kikwazo cha Waafrika kujumuika katika Jamii ya Kichina.

Zaidi ya Wafrika 100 waliandamana mpaka kituo cha polisi cha Guangzhou, nchini China, baada ya mfanyabiashara wa Kinigeria kuanguka na kufa wakati akijaribu kukwepa ukaguzi wa Viza.

Mwandishi Thomas Bäarthelein wa Idara ya matangazo ya Asia ya Duetsche Welle anasema tukio hilo linaashiria ongezeko kubwa la idadi ya Waafrika nchini China.

Takwimu za rasmi zinaonesha kuwa Waafrika elfu 20 kwa hivi sasa Wanaishi China, wengi wao wakiwa wafanyabiashara na Wanafunzi.

Lakini takwimu zisizo rasmi zinaonesha kuna idadi kubwa zaidi ya hiyo, ambapo katika mji wa Guangzhou pekee kuna kiasi hicho cha watu elfu 20 na wengi wao ni raia kutoka Nigeria.

Msomi mmoja kutoka Ethiopia, Alexandra Demissie, aliyefanya utafiti wake kuhusu uhusiano wa China na Afrika kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Bochum cha hapa Ujerumani anasema Waafrika hao ni muhimu katika sekta ya biashara baina ya nchi hizo mbili.

"Ki msingi, ni watu wa kati. Wanaunganisha wanaviwanda wa China na wafanyabiashara wa Afrika. Na muda wote, hawa Wanigeria wanaoishi Guangzhu ni wasomi wa hali ya juu na wanazungumza lugha ya Kichina vizuri sana, kwa sababu wamekisoma katika vyuo vikuu. Chuo Kikuu cha Sun Yatsen cha Guanzhou ni miongoni mwa vyuo vikuu maarufu ambacho utaweza kuona idadi kubwa ya wanafunzi wa Kiafrika. Na ndiyo maana inakuwa rahisi kwao kuweza kuingia katika soko la Kichina kutokana na kujua lugha. Na hii inasaidia sana wafanyabiashara wa Afrika wanaingia China tuseme kwa wiki mbili au kwa wiki tatku kununua bidhaa.``alisema Demissie.

China Schuhfabrik
Biashara ya Viatu nchini ChinaPicha: AP

China imekuwa na maoni ya hali ya juu katika kupanuwa wigo wa biashara yake na mahusiano ya kisiasa na nchi za Afrika, na hivyo kurahisisha masharti ya kupata viza.

``Watu wanaweza kupata viza ya Kichina kwa urahisi sana,haraka watakapoonesha vielelezo kwamba wafanyabiashara au wanafunzi na vinginevyo, na kunakuwa hakuna matatizo kwa kweli na hakukuwa sababu tukio hili kutokea``

Kwa upande mwingine, anasema Polisi wanajaribu kuwawekea ngumu wahamiaji kutoka Afrika.

``Waafrika wanakutana na kunyanyaswa, wakiwa China zaidi ya nchi nyingine yeyote``

He Wemping ni mtaalamu wa masuala ya Afrika kutoka Chuo cha Sayansi ya Jamii nchini China. Anasema waafrika wana mahusiano mazuri, ikilinganishwa na wale wanaotoka nchi za Magharibi.

``Waafrika, wote Wafanyabiashara na Wanafunzi, inakuwa rahisi kukabiliana na tatizo la lugha, ikilinganishwa na Watu kutoka Ulaya na Marekani. Nimekutana na watu wengi wanazungumza vizuri lugha ya Kichina. Na imekuwa rahisi kwao kuweza kuzungumza hata kwa lafudhi ya kichina, ukilinganisha na watu wa ulaya au Marekani.Wapo rahisi kwenda sambamba na mazingira ya miji ya Kichina, na chakula cha Kichina siyo tatizo kwao."amesema He Wemping.

Lakini Alexander Demissie,ambae aliwahi kuishi China, anasema anazungumzia jambo lingine linalosababisha ugumu.

``Kwa uzoefu wangu, siyo rahisi kwa Mwafrika kuwa na rafiki wa kike wa Kichina. Kwa mfano kama unaishi katika nchi moja, na unashiriki katika maisha ya kijamii,unaweza pia kupata msichana wa Kichina, lakini hili halionekani, na hiyo inaweza kuwa sababu ya kwa Wachina kuwa na kiburi au kufanya mabaya dhidi ya Waafrika``aliongeza Demissie.

Demissie anasema mara nyingine kunatokea mapigano mitaani kati ya vikundi vya Waafrika na Wachina,na kuna ufahamu duni kuhusu Afrika kwa watu wa China.

Lakini, pengine, kutokana na muingiliano wa kibishara na kisiasa, Wachambuzi wanadai kuna uwezekano wa kutokea mabadiliko katika siku za zijazo.


Mwandishi Sudi Mnette
Mhariri Othman Miraji.