1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafrika olimpik Beijing 2008

22 Julai 2008

Wasichana na wavulana wa Ethiopia na Kenya watazamiwa tena kupepea bendera ya Afrika katika olimpik huko Beijing:

https://p.dw.com/p/Ehgv

Michezo ya Olimpik ya Beijing, itaanza rasmi kiasi cha wiki 2 kutoka sasa-August 8; na wanariadha wa Afrika ni miongoni mwa wale wanaotazamiwa kutia fora katika medani ya riadha kuanzia mita 800 wanaume na wanawake hadi mbio za marathon.

Afrika italenga huko Beijing,kuondoka na medali zaidi kuliko Athens,2004.Nguvu za Afrika itakayoshiriki pia katika dimba la olimpik na ringi ya mabondia, zinatuwama hatahivyo, katika riadha-na hapo ndipo msisimko na jazba ulipo.

Wakati wanariadha wa mbio za kasi wa Marekani,Karibik na wa Afrika magharibi kama vile bingwa wa sasa wa rekodi ya dunia,Mjamaica Usain Bolt,bingwa wa zamani wa rekodi ya dunia Asafa Powell na bingwa wa dunia kutoka Marekani Tyson Gay wataumana kuania taji la mita 100 wanaume, wanariadha wa Afrika watazamiwa kutamba tena kuanzia mita 800 hadi marathon:

Majina ya kwanza yanayochomoza usoni ni chipukizi wa Kenya wa mita 800 aliekimbia muda bora msimu huu na wa kasi zaidi katika miaka 11 iliopita,Pamela Jelimo,mwenye umri wa miaka 18 tu. Muda wa Jelimo wa dakika 1 sek.54.99 ndio wa kasi kabisa msimu huu uliotangulia olimpik.

Hasimu yake mkubwa huko beijing atakua mkenya mwenzake bingwa wa dunia Janeth Jepkosgei,bingwa wa dunia, agfrika na Jumuiya ya madola. Janeth alitamba mwaka jana huko Osaka, Japan, lakini anaelewa kwamba Beijing ana changamoto kali zaidi kutoka nyumbani kenya kwa Jelimo.

Msichana mwengine wa kutupiwa macho kurudi na medali za dhahabu ni muethiopia Tirunesh Dibaba ambae atalenga kunyakua medali mbili za dhahabu tangu katika mita 5000 hata mita 10.000.

Dibaba ni bingwa wa dunia mara mbili katika masafa hayo na ingawa ana umri wa miaka 23 ana maarifa ya kutosha.Dibaba alivunja rekodi ya dunia ya masafa ya mita 5000 kwa sekunde 5 mjini Oslo, mwezi uliopita (June).Lakini anajua kwamba changamoto kali ataipata Beijing kutoka bingwa wa zamani wa rekodi hiyo nae anatoka pia Ethiopia Meseret Defar.

Upande wa wanaume, wakenya wanatazamia kuendelea na mila na desturi yao ya kurejea Nairobi na taji la mita 3000 kuruka viunzi na mara hii wanayataka yote 2-ya wanaume na wanawake.

Kama upande wa wanawake, changamoto ya mita 5000 na 10.000 wanaume itakua kati ya waethiopia wenyewe.Baada ya mzee Gebreselassie, kujitoa katika mbio za marathon za Beijing kutokana na hali ya hewa ya jiji hilo,anatazamiwa kupeana tena changamoto katika mita 10.000 na mwenzake Kenenisa Bekele.Bekele ndie bingwa wa rekodi za dunia tangu mita 5000 hata mita 10.000 ambazo ziliwahi kuwa mali ya gebre.Halkadhalika, Bekele alirithi mataji ya ubingwa wa dunia ya Gebre katika masafa hayo.

Gebreselassie akiwa sasa na umri wa miaka 35,hafai bado kutolewa maanani.Wakenya watakua na kazi ngumu kupenya kati ya madume hao 2 wa Ethiopia.

Bekele anatazamiwa kujaribu mara hii huko Beijing ,kutamba katika masafa yote 2 na kumuigiza mzee Miruz Yifter alivyofanya katika michezo ya olimpik ya Moscow, 1980.

Mbio za marathon tangu wanawake hata wanaume ni wazi na nivigumu kubashiri nani mwishoe ataingia kwanza uwanjani mjini Beijing siku ya finali ya wanawake na wanaume.Kenya ilioshinda mwaka jana huko Osaka katika ubingwa wa dunia,inatazamia ushindi mwengine tangu upande wa wanaume hata wanawake.