1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanataka hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wahusika

Faiz Musa 6 Juni 2019

Waandamanaji nchini Sudan wamekataa ombi la kufanya mazungumzo lililotolewa na baraza la mpito la kijeshi na badala yake wanataka haki kutendeka baada ya jeshi kuwauwa waandamanaji zaidi ya mia moja katika msako mkali

https://p.dw.com/p/3JwOE
BG Sudan Proteste
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Kamati ya madaktari wa Sudan wanaojihusisha na vuguvugu la maandamano hayo imesema watu 108 wameuliwa katika uvamizi wa jeshi dhidi ya waandamanji waliokuwa wamekita kambi nje ya makao makuu ya jeshi na miili 40 ilipatikana ndani ya mto huku watu zaidi ya mia tano wakiendelea kuuguza majeraha.

Msemaji wa Muungano wa Wasomi wa Sudan unaongoza maandamano hayo, Amjad Farid, amesema Wasudan hawako tarayi kwa mazungumzo na baraza la kijeshi linalouwa watu na wanataka hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wahusika wa mauaji hayo kabla ya kuanza mazungumzo yoyote ya kisiasa. Farid ameongeza kwamba wataendelea na maandamano bila ya umwagaji damu na kutotii sheria katika kuukataa uongozi wa baraza la kijeshi.

Sudan | Streik
Wafanyakazi wakiandamana nje ya benki ya KhartoumPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Siku mbili baada ya uvamizi uliosabaisha mauaji hayo makubwa na kulaaniwa kote ulimwenguni, naibu kiongozi wa baraza la kijeshi, Hamdan Dagalo, amesema wameanzisha uchunguzi na wahusika watafunguliwa mashtaka huku akiwataka waandamanji hao kushiriki katika kikao na baraza la kijeshi kuujadili mkwamo huo wa kisiasa.

"Mlango wa mazungumzo uko wazi na sisi kama baraza la jeshi tumetangaza mpango kamili wa amani kwa mavuguvugu yote yaliyo na silaha, tumetangaza mpango kamili wa amani kwa wale wote wanaotaka amani lakini hatutavumilia inapokuja katika usalama wa wananchi," alisema Hamdan.

Serikali yakana idadi ya vifo

Daktari Suleiman Abdul Jabbar, katika wizara ya afya kupitia shirika la habari la serikali, SUNA, amekanusha taarifa za waandamanaji zinazosema waliouliwa ni zaidi ya mia moja, akisema hadi sasa idadi ya waliopoteza  maisha hawapiti watu 46 .

Saudi Arabia yenye uhusiano wa ukaribu wa na baraza la kijeshi la Sudan imesema inafuatilia yanayoendelea nchini Sudan kwa wasiwasi mkubwa na kuhimiza vikao vya mazungumzo baina ya baraza la wananchi wanaoandamana wakiongozwa na miungano ya wasomi na vuguvugu la mabadiliko ambayo iliongoza maandamano ya miezi kadhaa yaliyosababishaa kupinduliwa kwa Omar al-Bashir.

Naibu waziri wa maswala ya mambo ya kigeni wa Urusi, Mikhail Bogdanov, amepinga mataifa ya nje kuingilia mzozo wa Sudan na kusema  serikali ya Urusi inahimiza mazungumzo ya kitaifa ya kuamua kipindi cha mpito kitakachowaongoza Wasudan kuelekea uchaguzi. Ameeleza kwamba kinachohitajika hivi sasa ni kuwakabili wasiotaka ustawi katika taifa hilo ila wanapinga mataifa mengine kuingilia maswala hayo kwa kuwawekea vikwazo vya aina yoyote.

Urusi imekuwa ikishirikiana na Iran ambayo ni hasimu mkubwa wa Saudi Arabia.

(RTRE/AFPE/APE)