1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji Thailand walenga majengo ya serikali

14 Januari 2014

Waandamanaji wa upinzani nchini Thailand leo (14.01) wameelekea kwenye majengo ya serikali kuwashawishi wafanyakazi wa umma kufunga ofisi zao na kujiunga na kampeni yao ya kusimamisha shughuli katika mji mkuu, Bangkok.

https://p.dw.com/p/1AqVg
Waandamanaji Thailand wataka waziri mkuu ajiuzulu.
Waandamanaji Thailand wataka waziri mkuu ajiuzulu.Picha: Reuters

Kiongozi wa waandamanaji hao ametoa onyo kwa waziri mkuu wa nchi hiyo kuwa ndiye atafuatia kuwa mlengwa mkuu, huku wengine wakitabiri vurugu hizo kudumu kwa miezi miwili.

Maandamano hayo ambayo leo yameingia siku yake ya pili yamesababisha kufungwa kwa makutano ya barabara muhimu katika mji huo katika juhudi za kumlazimisha waziri mkuu Yingluck Shinawatra na baraza lake la mawaziri kujiuzulu, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Waandamanaji hao ambao pia walitishia kuchoma kituo cha hisa nchini humo wameapa kuendelea na maandamano yao hadi hapo serikali ya Shinawatra itakapoondoka madarakani, ukiishutumu kwa rushwa na upendeleo.

Waratibu wa maandamano hayo wamesema kundi moja la waandamanaji litakuwa likiondoka kwenye makutano kila asubuhi, na kurejea jioni.

Kituo cha televisheni cha BlueSky kimesema kuwa asubuhi ya leo maelfu ya waandamanaji wameelekea kwenye mamlaka ya forodha, wizara ya fedha na wizara ya biashara, huku kiongozi wa upinzani Suthep Thaugsuban akitoa wito kwa wafanyakazi wa umma, walimu na wanafunzi kujiunga na maandamano yao.

Waziri Shinawatra asisitiza kutojiuzulu

Hata hivyo, Waziri Mkuu Shinawatra amesisitiza kutojiuzulu huku waandamanaji wakitishia kuzuia shughuli muhimu za serikali na kuathiri shughuli nyingine za wakaazi milioni 12 wa mji huo.

Mmmoja wa waandamanaji nchini Thailand.
Mmmoja wa waandamanaji nchini Thailand.Picha: Reuters

Ingawa mji mkuu ulikuwa umetuliwa na maelefu ya waandamanji hao kuandamana kwa amani, wachambuzi wanasema makubaliano ya amani ni muhimu yakazingatiwa kutatua mzozo huo, katika kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwezi ujao.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo, hakuna namna nyingine zaidi ya makubaliano kutokana na waandamanaji kuonyesha kwa vitendo juu ya kuchukizwa na serikali yake na kuna hatari ya kueneza vurugu hizo nchi nzima.

Taarifa zinasema kuwa wizara mbali mbali na Benki kuu ya nchi hiyo vililazimika kufanya kazi kwa kupitia mlango wa nyuma, baada ya waandamanji hao kuwazuia wafanyakazi umma kuingia kazini.

Huku kiongozi wa upinzani Suthep Thaugsuban akitishia kuwa siku tatu au mbili zijajazo watafunga ofisi zote za serikali, na hilo likishindikana watawazuia waziri mkuu na mawaziri wengine, sambamba na kukata umeme na maji majumbani mwao na kuwaonya kuwaondoa watoto wao.

Wazorotesha utendaji kazi serikalini

Maandamnao hayo yameanzia katika eneo kubwa la kambi ya maandamano hadi katika ofisi za mawaziri, ofisi za forodha, mipango, na ofisi nyingine muhimu za serikali kwa ajili ya kuzoretesha utendaji kazi wa serikali.

Maandamano kusababisha vurugu zaidi.
Maandamano kusababisha vurugu zaidi.Picha: Reuters

Kufuatia tishio la kuchomwa kwa kituo cha hisa, rais wa kituo hicho, Jarumporn Chotikasathien amesema hatua muhimu za kuimarisha ulinzi zimechukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.

Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Thailand kitivo cha biashsra unaonyesha kuwa maandamano hao yanaweza kusababisha kuyumba kwa uchumi wa nchi na kupoteza zaidi ya Dola milioni 30.33 kwa siku.

Mwandishi: Flora Nzema/RTRE/APE

Mhariri: Mohamed Khelef