1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wa upinzani wapigwa na polisi nchini Sudan

14 Desemba 2009

Ni katika kujaribu kuyazuia maandamano hayo.

https://p.dw.com/p/L1oM
Mandhari ya jiji la Khartoum, ambako waandamanaji walipambana na polisi hii leo.Picha: DW/Stefanie Duckstein

Hali nchini Sudan bado si ya utulivu pamoja na kwamba jana Jumapili viongozi kutoka pande mbili za nchi hiyo, yaani Sudan Kaskazini na Sudan Kusini, kutangaza mpango wa kufanya mageuzi ya kidemokrasia, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani, na kura ya maoni ya Sudan Kusini juu ya uhuru wake.

Leo waandamanaji kutoka chama cha Sudan Kusini cha SPLM walipigwa na polisi wakati walipokuwa wanaandamana kuelekea bungeni.

Polisi wa usalama nchini humo walizifunga barabara zote zinazoelekea katika jengo la bunge kwenye mji wa Omdurman uliopo upande wa pili wa Khartoum, ambao pia wanachama wa chama hicho cha Sudan Kusini, SPLM waliokuwa na bendera za chama hicho walipigwa na polisi wakiwa njiani kuelekea kwenye maandamano hayo.

Karibu vikundi 21 vya upinzani vikiwemo vyama vya SPLM na Ummah, vimeitisha maandamano kudai demokrasia zaidi, hata baada ya mpango wa mageuzi ya kidemokrasia kufikiwa wiki iliyopita.

Makamu mwenyekiti wa chama tawala cha (NCP) Nafie Ali Nafie, alisema vyama hivyo viwili pia vimekubaliana kuiangazia sheria ya usalama na upelelezi, ili kuweza kufikia makubaliano.

Nafie alikuwa akizungumza na waandishi wa habari huku akiwa na mkuu wa waasi wa zamani wa SPLM, Pagan Amum, ambaye alisema kwa makubaliano hayo, walikuwa wametangaza kumalizika kwa mvutano baina ya vyama hivyo viwili.

Mapema chama cha SPLM kilitaka matokeo ya kura ya maoni yaamuliwe kwa ushindi wa zaidi ya asimilia 50, wakati chama cha NCP kilitaka matokeo yaamuliwe kwa ushindi wa theluthi mbili ya kura.

Suala jingine lililokuwa linasababisha kutoelewana kwa vyama hivyo, ni juu ya mamlaka ya vyombo vya dola vya nchi hiyo.

Amum alisema maelezo kamili ya makubaliano hayo yatatangazwa baada ya mashauriano na vyama vyote vya kisiasa vya Sudan, na akaongeza kwamba wabunge wote waliogoma kwa siku 45 wataanza kuhudhuria bungeni ndani ya saa 24.

Tangazo hilo limekuja baada ya mfululizo wa mikutano tangu Alhamisi iliyopita, baina ya Rais Omar El-Bashir na kiongozi wa Sudan Kusini John Kiir.

makubaliano hayo yamezingatia katika kuondoa hali ya mvutano kati ya vyama hivyo viwili, hali ambayo imekuwa ikitishia mpango wa amani uliosainiwa mwaka 2005 kati ya Sudan Kusini na Kaskazini, ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo kadhaa.

Mageuzi na mabadiliko katika sheria ya uchaguzi vilikuwa ni vigezo muhimu katika mpango wa amani wa mwaka 2005.

Ghasia ziliongezeka pale polisi wa Sudan walipowakamata viongozi watatu wa ngazi ya juu wa upinzani, akiwemo Amum, na waandamanaji kadhaa kutoka upande wa kusini, katika kujaribu kuyazuia maandamano hayo.

Waandamanaji wa Sudan Kusini walijibu kwa kuchoma moto ofisi za NCP katika mji wa Kusini wa Wau.

Mjumbe wa Marekani Scott Gration, alitarajiwa kufika Sudan jana usiku, kama sehemu ya juhudi za kuondoa mvutano baina ya vyama hivyo viwili.

Uchaguzi mkuu wa 2010 utakuwa wa kwanza nchini Sudan tangu mwaka 1986, miaka mitatu kabla ya Bashir kuipindua serikali iliyokuwa imechaguliwa kidemokrasia, katika mapinduzi yasiyokuwa ya umwagaji damu, na yakiwa ni mapinduzi ya tano tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1956.

Mwandishi:Lazaro Matalange/AFP

Mhariri:Aboubakary Liongo