1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi wa kimataifa wapewa tuzo ya DW

15 Agosti 2013

Waandishi wa habari wanaotetea haki za binaadamu kupitia kazi yao wamepewa tuzo ya Kijerumani ya vyombo vya habari katika sera za maendeleo. Mwaka huu, tuzo hiyo inawaenzi wapiga picha wa magazeti na majarida.

https://p.dw.com/p/19QMb
Washindi wa tuzo ya vyombo vya habari
Washindi wa tuzo ya vyombo vya habariPicha: DW/T.Ecke

Tangu mwaka 1975 tuzo hiyo imekuwa ikitolewa kwa waandishi wa habari wanaofanya kazi bora ya kuripoti juu ya haki za binaadamu na maendeleo. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, tuzo hiyo imetolewa kwa waandiishi wa habari wa kimataifa kwa ushirikiano wa DW na wizara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya hapa Ujerumani. Zilitolewa tuzo saba, sita kwa waandishi kutoka kanda mbali mbali za ulimwengu, na tuzo moja maalumu kwa wapiga picha wa Kiafrika.

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Kwa sababu hiyo, tuzo inawaenzi wale wasiokubali kunyang'anywa haki yao ya kutoa maoni, alisema Niebel na kuongezea kwamba lengo ni kuwapongeza waandishi wa habari wanaoripoti juu ya maendeleo na hali ya haki za binaadamu katika nchi zao kwa ujasiri mkubwa na mara nyingi katika mazingira magumu.

Waziri wa maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani, Dirk NiebelPicha: DW/T.Ecke

Naye mkurugenzi wa DW, Erik Bettermann, aliongezea, "Tuzo hii ni ya kuwatia moyo wengine waingilie kati na kupaza sauti zao. Tunataka wafahamu kwamba hawako pekee yao!"

"Penye nia pana elimu"

Tuzo ya eneo la Amerika ya Kusini ilikwenda kwa watengenezaji wa tovuti inayoelezea kisa cha watu waliotoweka nchini Colombia. Majaji waliwasifu washindi kwa kutumia ubunifu wao na kudhihirisha namna ambavyo visa vinaweza kuelezwa kwa njia tofauti katika mtandao wa intaneti. Mshindi mwingine aliyeamua kuelezea ripoti yake mtandaoni ni mjerumani Uwe Martin. Yeye amefanya uchunguzi kuhusu uzalishaji wa pamba na namna unavyoharibu maisha ya wakulima wa zao hilo.

Kulikuwa pia na tuzo maalumu, ambapo umma ndio uliochagua nani awe mshindi. Tuzo hiyo ilitolewa kwa mpiga picha Oluyinka Ezekiel Adeparusi kutoka Nigeria. Picha yake inaonyesha watoto katika eneo la mabanda la Makoko, mjini Lagos. Watoto hao wamekaa katika boti na wako njiani kuelekea nyumbani wakitokea shuleni. Kichwa cha picha hiyo kinasema: "Penye nia pana elimu."

Picha ya mshindi Adeparusi kutoka Nigeria inaonyesha watoto wa shule
Picha ya mshindi Adeparusi kutoka Nigeria inaonyesha watoto wa shulePicha: Oluyinka Ezekiel Adeparusi

Majaji waliwasifu washindi kutoka India na Liberia kwa kuweka uwiano kati ya kuguswa na kisa kinachoripotiwa na kwa upande mwingine kuweka umbali fulani kati yao na kisa wanachokizungumzia. Wade Williams kutoka Liberia alisema "Aliye mwandishi wa habari ana kalamu mkononi. Kalamu hiyo inaweza kutoa sauti kwa wale wanaoihitaji."

Mwandishi: Ralf Witzler

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Josephat Charo