1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi Chad wadai kuteka mji mwingine

Kalyango Siraj16 Juni 2008

Serikali yasema hizo ni 'Propaganda'

https://p.dw.com/p/EKfH
Rais wa Chad Idris Deby,kulia akiwa na waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Herve Morin, Feb. 6, 2008 mjini N'Djamena, Chad. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner asema serikali yake haina hamu ya kuingilia kati sasa ChadPicha: AP

Waasi nchini Chad wanasema kuwa wamefikia moja wa malengo yao leo jumatatu katika mkakati wao mpya wa kumg'oa madarakani rais Idris Deby wa nchi hiyo.

Waasi wa kundi la National Alliance wanadai kuwa wamefanikiwa kuuteka mji wa Biltine,ambao unapatikana umbali wa kilomita 750 kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa nchi wa Ndjamena.

Mji wa Biltine,unaodaiwa kuchukuliwa na waasi hao uko umbali wa kilomita 100 kaskazini ya mji mkuu wa mkoa huo wa Abeche. Pia ndio mji wa tatu kudaiwa kuchukuliwa na waasi hao katika vita vipya dhidi ya utawala wa sasa wa Ndjamena.

Msemaji wa chama cha waasi hao,Ali Gueddei,ameliambia shirika la habari la kifaransa la AFP kuwa mbali na kufanikiwa kuuteka mji huo wa Biltine, lakini hawatakaa katika mji huo bali watafululiza kuuteka mji mwingine wa Mongo ulioko umbali wa kilomita 400 mashariki mwa mji mkuu wa Ndjamena.

Msemaji huyo ameeongeza kuwa hakukuwa na mapigano makali katika mji huo akisema kuwa wanajeshi wa serikali hawakuwategemea.

Serikali haijatoa taarifa kuhakikisha madai ya waasi ya kuuteka mji wa Biltine.

Wakuu mjini Ndjamena wameyaelezea madai ya awali ya kuelekea katika mji mkuu kama mbinu tu za kujipigia debe.

Nae kiongozi mwingine wa kundi hilo aitwae,Abderahman Koulamallah,akiongea kutoka Libreville Gabon,amesema kuwa mkakati wa waasi hao ni kujaribu kuepuka miji ambayo inaulinzi mkali ili kuepuka kupata hasara kubwa.

Aidha ameongeza kuwa mara hii wamejiandaa kwa vita vya mda mrefu akisema wanavyombo vya kutosha kuendelea na mapambano.

Mji wa Biltine uko masafa ya kilomita 100 hivi kaskazini mwa Abeche.Abeche ndio eneo muhimu kwa kuunganisha shughuli za misaada ya kibinadamu mashariki mwa Chad,eneo linalopakana na lingine la Sudan maarufu la Darfur.

Vikosi vya Ufaransa pamoja na vya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Ulaya la EUFOR vimepiga kambi mjini Abeche.

Shahidi moja alisema kuwa siku ya jumamosi waasi waliukalia kwa mda mji wa Goz-Beida ulio umbali wa kilomita 200 kusini mwa Abeche.

Na jana jumapili serikali ya Chad ilisema kuwa kundi la waasi lingine lilifanya kile ilichokiita kupitia, mji mwingine wa Am-Dam ulio umbali wa kilomita 140 kusini magharibi mwa Abeche.Waasi wanasema waliukalia mji huo kwa mda kabla ya kusonga mbele na kusema kuwa walikabiliana na upinzani mdogo.

hali katika mji mkuu wa Ndjamena imebaki tulivu leo jumatatu, ingwa wakaazi wanasema wanaingiwa na wasiwasi kutokan na taarifa za waasi kusonga mbele.Ofisi za serikali,soko pamoja na benki zimebaki zikifanya kazi kama kawaida jumatatu.

Jumapili serikali ya Chad ilisema katika taarifa kuwa waasi wanatumia mbinu za kuwavuta wanajeshi kutoka ngome zao za ulinzi katika vituo muhimu.

Serikali ya Ufaransa inawanajeshi wake huko Chad pia inamkataba wa ushirikaino na serikali ya sasa.Lakini waziri wake wa mashauri ya kigeni Bernard Kouchner alisema jumapili alipokuwa nchini Cote D'ivore kuwa nchi yake haina nia ya kuingilia kati katika mapigano ya sasa.

Ufaransa ilimsaidia sana rais Deby katika hujuma ya waasi walioifanya mwezi Febuari mwaka huu ambapo walifurushwa.