1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi nchini Kongo wajiimarisha na kuudhibiti mji wa Kanyabayonga

Saumu Mwasimba13 Novemba 2008

Maelfu ya watu wamekimbia eneo hilo huku vita vikihofiwa kuingia Kinshasa.

https://p.dw.com/p/Fu5Y
''Laurent Nkunda atishia kuipindua serikali''Picha: picture-alliance/ dpa

Waasi katika eneo la mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo leo hii wameingia kwenye mji wa Kanyabayonga mji ambao ulishuhudia wizi pamoja na wanawake kubakwa na vikosi vya serikali mapema wiki hii.Waasi hao wanadai kuingia mjini humo bila ya kusababisha umwagikaji damu wowote.Mji huo wa Kanyabayonga ni muhimu kwa sababu ni kituo cha makutano ya barabara zote kubwa katika jimbo la Kivu ya Kaskazini.

Duru zisizoegemea upande wowote zimefahamisha kuwa waasi wanaongozwa na generali Laurent Nkunda kufikia jana usiku walikuwa tayari wameshadhibiti eneo lililoko kiasi kilomita 10 kutoka kusini mwa mji wa Kanyabayonga ambako ni takriban kilomita 175 kutoka mji mkuu wa jimbo la kivu kaskazini,Goma.

Taarifa zinasema kwamba waasi wa generali Nkunda ambao kwa kipindi cha zaidi ya wiki mbili wamekuwa kilomita 15 nje ya mji wa Goma tayari wameshakidhibiti kijiji cha Mirangi kijiji cha mwisho wakielekea kwenye mji wa Kanyabayonga.

Aidha taarifa hizo zimethibitishwa pia na msemaji wa chama cha CNDP cha Generali Laurent Nkunda,Bertrand Bisimwa ambaye amesema kwamba wameweza kuingia katika eneo hilo bila ya kusababisha umwagikaji wa damu kama ilivyofanywa na jeshi la serikali mapema wiki hii.

Msemaji huyo wa CNDP ameongeza kusema kwamba hali ni shwari kwa sasa mjini Kanyabayonga ingawa watu bado wanaendelea kukimbia.

Generali Laurent Nkunda ametishia kuipindua serikali madarakani ikiwa haitokubali kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na kundi hilo.Aidha Umoja wa Mataifa unasita sita juu ya kupeleka wanajeshi zaidi katika eneo hilo.Hali hiyo imewafanya wakaazi wa Kongo kuingiwa na wasiwasi zaidi kwamba huenda ghasia zikazagaa hadi mji mkuu Kinshasa.Akizungumza hivi punde na Dw msemaji wa chama cha waasi cha CNDP Bertranda Bisimwa amedai kwamba wako njiani kueleka mji mkuu Kinshasa.

Mji wa Kayabayonga ambako waasi wameshaingia ni muhimu kwakuwa ni eneo linalounganisha barabara kubwa katika kivu ya kaskazini.Msemaji wa ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Kongo Monuc ambao unakambi yake mjini Kanyabayonga hakuweza kufikiwa kuzungumzia hali ilivyo.

Hapo jana jeshi la Monuc liliwalaumu waasi kwa kuwalazimisha maelefu ya watu walioachwa bila makaazi kuihama kambi walikokuwa wamekimbilia hifadhi wakati serikali ya rais Joseph Kabila mjini Kinshasa ikiahidi kuwaadhibu wanajeshi waliohusika katika kutekeleza maovu huko Kanyabayonga.

Maelfu ya raia walikuwa wamekimbilia hifadhi karibu na kambi ya jeshi la Monuc huko Kiwanja kiasi kilomita 80 kutoka kaskazini mwa mji wa Goma ili kuyatoroka mapigano ya wiki iliyopita kati ya waasi wa Nkunda na makundi yanayoiunga mkono serikali.

Waasi wanaoongozwa na Laurent Nkunda waliliteka eneo la kiwanja mnamo Novemba 5 na kuanzisha opresheni ya mauaji ya wanamgambo wachache waliobakia wa Mai Mai wanaoiunga mkono serikali.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limefahamisha kwamba watu kiasi cha 50 waliuwawa.Watu wanaokadiriwa kufikia hamsini elfu wamekimbia makambi yaliyoko kwenye eneo la Rutshuru kilomita chache kutoka Kiwanja.Kwa jumla Umoja wa mataifa unasema kuwa tangu mwezi wa Agosti mapigano yalipochacha zaidi ya watu 250 wameachwa bila maakaazi.