Waasi wa ADF waushambulia mji wa Beni
23 Julai 2019Kubwa katika yote ni mauwaji ya watu kumi yaliyofanywa na ADF usiku wa kuamkia leo katika kata ya Mabasele, katika mji mdogo wa Oicha, ambako watu kumi wameuawa kwa kukatwa kwa mapanga.
Akizungumza na idhaa ya kiswahili ya DW, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji wa Beni Kizito Bin Hangi alisema, kuwa haelewi hali ya kusuasua kwa operesheni za kijeshi dhidi ya waasi kutoka Uganda ADF katika eneo hili.
Akizungumzia maeneo yaliyoshuhudia mauwaji hayo, Kizito Bin Hangi anamuomba rais Félix Tshisekedi kutekeleza ahadi yake kwa raia wa Beni, wakati wa ziara yake katika eneo hilo.
Mauwaji ya usiku wa leo yakiwa yanatokea baada ya yale yaliyofanywa na waasi hao katika vitongoji vya Eringeti, Mayimoya, Mangboko na Malolu, yamezusha hofu mioyoni mwa wakaazi, waliokuwa na matumaini kwamba amani ya kudumu itarejea katika eneo hili.
Hatua itakayowapelekea kurudi katika mashamba waliyoyahama wakihofia maisha, na kuanzisha upya shughuli za kilimo.
Jeshi la serikali ya DRC yafanikiwa kuwaangamiza baadhi ya waasi
Katika kuwashambulia waasi wa ADF, baada ya kuwauwa raia, majeshi ya serikali yalifanikiwa kuwauwa waasi wanne, na kuchukuwa silaha mbili kutoka waasi hao.
"Hongera kwa majeshi ya serikali ya Kongo, kwa kazi walioifanya ya kuwauwa waasi wanne na kuchukuwa silaha zao,"alisema Meya wa Beni Bwanakawa Masumbuko Nyonyi.
Idadi ya waasi wa ADF waliouawa katika operesheni za kijeshi, imeongezeka na kufikia watano,kama anavyotueleza Sheikh Djamali Mussa,mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika kongamano la Batangi Mbau
Mauwaji ambayo kwa sasa yanakita mizizi, yamewapelekea wadadisi wa maswala ya usalama,kuiomba serikali ya DRC kuomba msaada wa kijeshi toka nchi jirani ya Uganda, ADF wakiwa ni maadui wa nchi zote mbili.
Ombi hilo haijulikani ikiwa litakubaliwa na serikali zote mbili yaani Kongo na Uganda.