1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Houthi 23 wauwawa Yemen

Mjahida24 Aprili 2015

Afisa mmoja nchini Yemen amesema waasi 23 wameuwawa katika mashambulizi mapya ya angani yalioongozwa na muungano wa Saudi Arabia siku ya Alhamisi, yaliolenga maeneo ya kusini mwa mji wa Daleh.

https://p.dw.com/p/1FEFb
Moshi uliotokana na shambulizi la angani nchini Yemen
Moshi uliotokana na shambulizi la angani nchini YemenPicha: Reuters/K. Abdullah

Nasser al-Shuaibi kiongozi wa makundi yaliojihami kwa silaha yanayomtii rais Abedrabbo Mansour Hadi amesema maeneo mengi ya waasi katika shule kadhaa na majengo mjini Daleh na mji mwengine wa Lahj, yalilengwa kwa mashambulizi hayo ya angani.

Afisa mwengine wa serikali mjini Daleh amesema waasi 23 waliuwawa lakini ni vigumu kwa waasi wenyewe wa Houthi kukubali hasara wanayopata kwa hiyo vifo hivyo havikuweza kuthibitishwa.

Waasi hao wa Houthi walichukua nafasi ya tangazo la Saudi Arabia kwamba wamesitisha mashambulizi dhidi yao, na siku ya Jumatano wiki hii wakadhibiti makao makuu ya jeshi mjini Taez.

Hata Hivyo wakaazi wa eneo hilo wamesema kulikuwa na mashambulizi ya angani usiku mzima yakilenga maeneo ya waasi mjini humo. Kwa upande wao maafisa wa afya wamesema kumekuwepo na majeruhi lakini hawakuweza mara moja kutoa idadi yao.

Gari la kubeba wagonjwa lapita Karibu na wapiganaji waliotiifu kwa rais Abedrabbo Mansour Hadi
Gari la kubeba wagonjwa lapita Karibu na wapiganaji waliotiifu kwa rais Abedrabbo Mansour HadiPicha: AFP/Getty Images

Wakati huo huo katika mji wa pili kwa ukubwa wa Aden nchini Yemen mkurugenzi wa idara ya afya Al-Kheder Lassouar amesema watu wapatao sita wakiwemo raia na wanamgambo wanaomuunga mkono rais hadi waliuwawa huku watu wengine 56 wakijeruhiwa katika mapigano kati ya pande mbili zinazohasimiana.

Kwa sasa shirika la afya duniani WHO limesema idadi ya watu waliouwawa katika mapigano nchini Yemen tangu kuanza kwa mapigano tarehe 26 mwezi Machi imefikia watu 1000.

Ndege za kivita za Saudi Arabia zilianzisha mashambulizi mengine mapya dhidi ya waasi hapo jana licha ya matakwa kutoka kwa waasi hao wanaoungwa mkono na Iran kwamba uvamizi dhidi yao usitishwe ili kutoa nafasi kufanyika mazungumzo ya amani yatakayoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Ban Ki Moon ametangaza kumteua Ismail Ahmed kama mjumbe wake mpya wa Yemen.

Huku hayo yakiarifiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametangaza mipango ya kumteua mwanadiplomasia anayetokea Mauritania Ismail Ould Cheikh Ahmed kama mjumbe wake mpya nchini Yemen. Ismail Ould Cheikh Ahmed anachukua nafasi ya Jamal Benomar raia wa Morocco aliyejiuzulu wiki iliopita baada ya juhudi zake za upatanishi kukosa kuungwa mkono na mataifa ya ghuba yalio na utajiri wa mafuta.

Kwengineko Muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia umesema utaingia katika awamu ya pili ya kampeni yake dhidi ya waasi itakayolenga juhudi za suluhusho la kisiasa, kupeleka misaada katika maeneo yalioathirika na kupambana na ugaidi.

Mjumbe mpya mtarajiwa wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed
Mjumbe mpya mtarajiwa wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Cheikh AhmedPicha: Zoom Dosso/AFP/Getty Images

Kwa upande wake rais wa Marekani Barrack Obama ameitaka Iran kusaidia kupatikana suluhu ya kisiasa nchini Yemen huku akilishutumu jamhuri hiyo ya kiislamu kuchochea mgogoro wa Yemen. Jana jioni maafisa wa ulinzi wa Marekani walisema msafara wa meli za Iran inayoshukiwa kubeba silaha kwa waasi wa Houthi imegeuka na kuelekea upande wa Kaskazini huku waziri wa mambo ya nchi za nje wa Yemen akiishutumu Iran kujaribu kuzipeleka meli zake mahali wanapozuwiya akisema huu unaonekana kuwa mpango wa Iran uliopangwa na waasi wa houthi.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba