1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Rohingya watangaza kusitisha mapigano

Mohammed Khelef
10 Septemba 2017

Waasi wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar wametangaza usitishaji mapigano wa mwezi mmoja ili kuyaruhusu makundi ya misaada kuwafikia walengwa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2jeoM
Pakistan Hyderabad Proteste Myanmar Aung San Suu Kyi
Picha: picture-alliance/Zumapress/J. Laghari

Takribani Warohingya 300,000 wamekimbilia nchini Bangladesh na raia wengine 30,000 wasiokuwa Waislamu wamegeuka wakimbizi ndani ya Myanmar, baada ya jeshi kuanzisha mapigano dhidi ya kundi la Arakan Rohingya Salvation Army (ARSA) ambalo tarehe 25 Agosti lilishambulia vituo 30 vya polisi na kimoja cha kijeshi.

"ARSA inazitaka pande zote zinazohusika na huduma za kibinaadamu kuendelea na kazi zao kwa wahanga wote wa mzozo huu, bila kujali kabila au dini yao, ndani ya kipindi hiki cha usitishaji mapigano," linasema kundi la ARSA kwenye taarifa yake iliyotolewa leo (Jumapili, 10 Septemba).

Athari ya hatua hiyo bado haijafahamika, kwani kundi hilo halionekani kuwa na upinzani mkubwa dhidi ya jeshi la Myanmar linalolikalia eneo lote la jimbo la Rakhine lililo kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Katika kipindi cha wiki mbili sasa, maelfu ya nyumba zimechomwa moto, vijiji kadhaa kuangamizwa na maelfu ya watu bado wako njiani kuelekea mpaka wa nchi hiyo na Bangladesh.

Bangladesh yazidiwa na wakimbizi

Wakimbizi wa Rohingya wakiwa nchini Bangladesh
Wakimbizi wa Rohingya wakiwa nchini Bangladesh Picha: picture-alliance/dpa/N. Islam

Wimbi la wakimbizi wenye njaa na fadhaa linalomiminika nchini Bangladesh limeyazidi nguvu makundi ya misaada ambayo tayari yalikuwa yanawahudumia maelfu ya wengine waliokuwa wamekimbia ghasia za huko nyuma.

Katika tamko lao la upande mmoja, ARSA wamelitaka pia jeshi kuweka silaha chini na kuruhusu msaada wa kibinaadamu kwa watu wote walioathirika na mapigano.

Serikali ya Myanmar inayoongozwa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi, inasema inaendelea na operesheni za kusafishasafisha ili kujilinda dhidi ya ARSA, inayoliita kundi la kigaidi.

Lakini waangalizi wa haki za binaadamu na Warohingya wanaokimbia eneo hilo wanasema jeshi na wanamgambo wa Kibudha wameongeza mashambulizi ya kuchoma moto vijiji kwa lengo la kuwafukuza Waislamu wanaoishi huko. 

Siku ya Ijumaa (Septemba 8), Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Bangladesh iligundua maelfu ya wakimbizi wa Rohighya ambao hawakuwa wameorodheshwa hapo kabla, na kuifanya idadi ya wakimbizi hao kufikia 270,000 kutoka ile ya 164,000. Kufikia Jumamosi, wakimbizi wengine 20,000 waliorodheshwa, na hivyo kuifanya idadi yao kuwa 290,000.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Sudi Mnette