1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Ukraine watangaza Jamhuri ya Donetsk

7 Aprili 2014

Waandamanaji wanaoiunga mkono Urusi wamezidhibiti ofisi za serikali za mikoa 3 ikiwa ni pamoja na Donetsk,mashariki ya Ukraine walikotangaza "jamhuri iliyojitenga" huku wanajeshi wa Urusi wakijongelea mpaka wa Ukraine

https://p.dw.com/p/1BdN1
Waandamanaji wanaoelemea upande wa Urusi wanapambana na wanaharakati wanaopigania umoja wa taifa la UkrainePicha: Reuters

Wanaharakati hao wanaodhibiti maeneo hayo tangu jana usiku,wanataka iitishwe kura ya maoni hadi May 11 ijayo kuhusu kuundwa nchi mpya kwa jina "Jamhuri ya umma wa Donetsk.Mmojawapo wa waandamanaji amesoma risala inayoitaka Urusi itume kikosi cha kulinda amani pindi serikali ya mjini Kiev,wanayoitaja kuwa "haramu" ikiamua kuingilia kati.

Opereshini kama hiyo ya Donetsk imefanyika pia katika miji ya Luhansk na Kharkiv.

Akizungumzia pirika pirika za wanajeshi wa Urusi waliokusanywa umbali wa kilomita 30 karibu na mpaka wa mashariki wa Ukraine,waziri mkuu wa Ukraine Arseny Yatseniuk amesema nyendo hizo zimeandaliwa makusudi na Urusi kwa lengo la kuitwaa sehemu ya mashariki ya Ukraine.Akilihutubia baraza lake la mawaziri waziri mkuu Yatseniuk ameongeza kusema tunanukuu"hilo hatutoliachia."mwisho wa kumnukuu.

Nae rais Olexandre Turtchinov ameituhumu Moscow "kuanzisha awamu ya pili ya kuimega Ukraine baada ya Crimea Marchi 21 iliyopita."

Wanajeshi wa Urusi Wamewekwa karibu na Mpaka wa Mashariki

Balozi wa Marekani katika jumuia ya usalama na ushirikiano barani Ulaya -OSCE,Daniel Baer amesema Urusi imekusanya maelfu ya wanajeshi wake karibu na mpaka na Ukraine na kuitolea wito Moscow ipitishe hatua ya kutuliza hali ya mambo.

Ostukraine Krise 07.04.2014 Donezk
Jengo la serikali huko Donetsk lakaliwa na waasi wanaoelemea upande wa UrusiPicha: Reuters

"Tuna ushahidi thabiti wa nyendo za maelfu ya wanajeshi karibu na mpaka na hawako katika hali ya kawaida kama wakati wa amani au wanapokuwa kambini"-amesema Daniel Baer mbele ya waandishi habari baada ya mkutano wa dharura wa jumuia hiyo yenye wanachama 57,waliokusanyika kuzungumzia mzozo wa Ukraine.

Ujumbe wa Urusi ambayo pia ni mwanachama wa jumuia hiyo haukuhutibia mkutano huo.

Wakati huo huo serikali kuu ya Ujerumani imesema imeingiwa na wasi wasi kutokana na matumizi ya nguvu ya waandamanaji wanaoelemea upande wa Urusi,mashariki ya Ukraine.

"Yanayotokea Donetsk na Kharkiv tunayafuatilizia kwa makini na yanazusha wasi wasi mkubwa" amesema msemaji wa serikali Steffen Seibert katika mkutano na waandishi habari mjini Berlin.

Ujerumani yaitaka Urusi itekeleze ahadi ilizotoa

Msemaji wa serikali kuu ya Ujerumani amesikitika kwamba ahadi alizotoa rais Vladimir Putin,alipozungumza na kansela Angela Merkel, kuwarejesha nyumbani baadhi ya wanajeshi wake ,mpaka leo hazikutekelezwa.

Regierungssprecher Steffen Seibert
Msemaji wa serikali kuu ya Ujerumani Steffen SeibertPicha: DW/P: Kouparanis

"Tunasubiri,sio tu sisi,bali Ulaya nzima, kuona ahadi hizo ambazo ni muhimu katika kurejesha hali ya kuaminiana,zinatekelezwa haraka iwezekanavyo-amesema msemaji wa serikali kuu ya ujerumani Steffen Seibert.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir:Reuters/Afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman