1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wadhibiti kasri la Gaddafi

Sekione Kitojo24 Agosti 2011

Miripuko na milio ya bunduki imeendelea kusikika katika mitaa ya mji mkuu wa Libya Tripoli hadi alfajiri ya leo Jumatano, hali ikiashiria kuwa wanajeshi watiifu kwa Gaddafi wanaendelea na mapambano

https://p.dw.com/p/12Mpd
Wapiganaji wa Libya wakisherehekea baada ya kuingia katika kasri la Gaddafi la Bab Al-Aziziya jana Jumanne.Picha: dapd

Miripuko na milio ya bunduki imekuwa ikisikka katika mitaa ya mji mkuu wa Libya Tripoli majira ya alfajiri leo Jumatano, hali inayowakumbusha wakaazi wa mji huo wenye hofu kuwa majeshi ya Moammar Gaddafi bado yanaendelea kuleta kitisho licha ya kusambaratishwa na waasi.

Wakati huo huo kiongozi wa Libya Moammar Gaddafi hajulikana aliko.

Libyen Gaddafi TV Fernsehauftritt
Kiongozi wa Libya Moammar Gaddafi ambaye hajulikani aliko hadi sasa .Picha: dapd

Wanajeshi watiifu kwa Gaddafi wanaendelea kushikilia baadhi ya maeneo ya mji wa Tripoli na wanaendelea kudhibiti hoteli ya Rixos, eneo ambalo limekuwa makaazi ya waandishi habari wa kigeni waliopewa kibali na serikali , wakiwazuwia kuondoka.

Waasi pia wanasema kuwa wanajeshi wa Gaddafi ambao wamejificha juu ya mapaa ya nyumba ambao huwashambulia watu wamewekwa katika njia ya kuelekea uwanja wa ndege na waasi wamesema walipoteza kiasi wapiganaji wanne usiku.

Wapiganaji ambao wameweka vizuizi barabarani , baadhi wakiwa wamejifunika bendera mpya za Libya huru , wamekuwa wakiyapekua magari kwa kutumia tochi kwa kuwa katika baadhi ya maeneo hakuna umeme.

Kabla ya hapo , wamesema wapiganaji hao kuwa hatukujua nani anakuja au anaekwenda. Hivi sasa tuna udhibiti mkubwa zaidi lakini watu wana hofu kwamba bado wanajeshi wa Gaddafi wapo katika maeneo ya mji huu. Mpiganaji mwingine amesema kuwa tuko karibu sana kumaliza kazi. Ni wanajeshi wachache sana waliobaki. Mungu akijalia katika siku chache zijazo nchi hii itakuwa safi kabisa.

Libyen Tripolis Aufständische haben den Stützpunkt Bab al Asasija gestürmt Muammar al Gaddafi Kopf
Wapiganaji waasi wakisherehekea kwa kufyatua risasi hewani wakiwa katika kasri la Gaddafi la Bab al-Aziziya.Picha: dapd

Sherehe za milio ya bunduki zilitikisa mji wa Tripoli jana wakati wapiganaji walipovunja kuta za makaazi ya Gaddafi ya Bab al-Aziziya katikati ya mji huo mkuu na kusababisha wanajeshi wa Gaddafi kukimbia. Inashangaza kuona watu wote walivyojitolea muhanga hadi kufika hapa tulipo. Tuko ndani ya viwanja vya makaazi yake, sasa yuko wapi? Amejificha, hawezi kufanya lolote. Yuko wapi ! alisema mmoja wa wapiganaji baada ya kukamata makaazi hayo ya Gaddafi

Wapiganaji , wakiwa katika hali ya tahadhari wamekuwa wakifanya safisha safisha katika mji huo mkuu kuwasaka wanajeshi wa serikali ambao wanaendelea kupambana katika maeneo mbali mbali ya mji huo.

Swali kuu hadi sasa lakini linalotia wasi wasi wakaazi wa mji huo pamoja na wapiganaji ni wapi aliko kanali Gaddafi na familia yake.

Kiongozi huyo wa Libya anadai kuwa anazunguka mjini humo bila kutambuliwa baada ya waasi kukamata makaazi yake, televisheni ya Al Arabia imetangaza leo.

Wanamapinduzi nchini Libya sasa wanakabiliwa na kazi ngumu ya kuijenga upya nchi hiyo baada ya kuanguka kwa utawala wa Gaddafi, lakini hofu ya kuangukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe inakuzwa mno, wamesema wataalamu.

Kiongozi wa baraza la taifa la mpito Mahmoud Jibril amesema kuwa uongozi wa baraza hilo hautakuwa katika misingi ya kulipiza kisasi.

Libyen Mahmud Dschibril
Kiongozi wa baraza la taifa la mpito Mahmud Jibril.Picha: dapd

Hapo baadaye tunapaswa pia kuwarejesha kazini maafisa wa jeshi na polisi waliokuwa upande wa Gaddafi , ambao katika miezi ya hivi karibuni wameonyesha uaminifu kwetu.

Nae kiongozi wa upinzani nchini humo Mustafa Abdel Jalil pia amesema leo kuwa Libya itafanya uchaguzi katika muda wa miezi nane ijayo na Moammer Gaddafi atafikishwa mahakamani nchini humo. Nae rais wa Urusi Dmitry Medvedev amemtolea wito Muammar Gaddafi na waasi wa Libya kuacha mapigano na kukaa chini kwa mazungumzo.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre/dpae

Mhariri:Abdul-Rahman