1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wahujumu Mogadishu

8 Septemba 2009

Wasomali zaidi watimuliwa maskani mwao .

https://p.dw.com/p/JVt2
Waasi wa Kiislamu mjini MogadishuPicha: AP

Taarifa kutoka Mogadishu,mji mkuu wa Somalia, zinasema kwamba raia 5 jana waliuwawa na wengine 25 walijeruhiwa kufuatia hujuma ya waasi wa kiislamu katika kambi ya serikali mjini Mogadishu. Miezi 4 ya mapigano makali mjini humo kumefanya idadi ya wasomali waliopoteza maskani kufikia zaidi ya milioni moja na nusu.Hii ni kwa mujibu wa Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa lilivyoiarifu jana.

Shahidi mmoja aitwae Omar Abdi amesema kwamba, mama mmoja na watoto 2 ni miongoni mwa maiti 5 alizoziona baada ya kufanyika hujuma hiyo mara tu jua lilipotua huko kusini mwa mji mkuu Mogadishu. Msemaji wa kijeshi wa Somalia Sheikh Abdirisak Mohamed ,aliarifu kwamba upande wa serikali hakuna maafa yoyote yaliopatikana katika hujuma hiyo.

Miezi 4 ya mapigano makali mjini Mogadishu yamefanya idadi ya wasomali waliobidi kuhama maskani zao kufikia milioni 1.55.Idadi hiyo kwa muujibu wa Shirika la wakimbizi la UM inajumuisha watu robo-milioni waliohama maskani zao tangu mapigano mapya kuutikisa mji mkuu huo mapema mwezi Mei.

"Sababu kuu ya muongezeko huo ni mapigano mapya mjini Mogadishu yaliowatimua majumbani mwao zaidi ya watu robo-milioni tangu Mei 7." Taarifa ya Shirika la wakimbizi la UM ilisema.

Hapo Mei 7, vikundi 2 vyenye itikadi kali ya kiislamu vilivurumisha hujuma kali mjini Mogadishu na sehemu za Somalia ya kati na kusini ikiwa na shabaha ya kumtimua madarakani Rais wa Somalia anaeungwa mkono na jamii ya kimataifa, Sheikh Sharif Ahmed.Mamia ya raia pia wameuwawa katika mapigano ambayo hujumuisha mapigano ya mizinga katika mitaa inayokaliwa na raia -mapigano yanayovipambanisha vikosi vya serikali na vile vya washirika wake vya Umoja wa Afrika dhidi ya waasi hao.

Shirika la wakimbizi la UM (UNHCR) limearifu kuwa kiwango cha kutimuliwa wakaazi makwao kimepungua ukilinganisha na ilivyokuwa wiki za kwanza za hujuma za waasi ,lakini shirika hilo likaongeza kusema kuwa, watu 95.000 walilazimika kuyakimbia majumba yao mnamo miezi 2 iliopita . Sehemu kubwa ya wasomali waliotimuliwa makwao na mapigano hukimbilia upande wa magharibi katika mji mdogo wa Afgoye, kiasi ya maili 18 kutoka Mogadishu.Sasa lakini, mji huo umesheheni wakaazi na vibanda hadi watu nusu-milioni.

Kwa muujibu wa UM ,Somalia wakati huu, inakumbana na msukosuko wake mkubwa kabisa wa kibinadamu tangu miaka 18 ya vita vyake vya kienyeji na ni miongoni mwa misiba mikubwa ya kibinadamu duniani.

Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na UM inapambana na waasi wa kiislamu waliotishia kuuteka kwa nguvu mji mkuu Mogadishu na kuipindua serikali inayoungwa mkono na nchi za magharibi.

Muandishi:Ramadhan Ali /AFPE

Mhariri: O.Miraji