1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi waidungua ndege na kuuwa 49 Ukraine

15 Juni 2014

Wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi Jumamosi (14.06.2014) wameidungua ndege ya uchukuzi ya kijeshi ya Ukraine mashariki mwa nchi hiyo na kuuwa watu wote 49 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

https://p.dw.com/p/1CIPz
Ndege ya Kirusi chapa Iljushin 76.
Ndege ya Kirusi chapa Iljushin 76.Picha: picture-alliance/dpa

Wanaharakati wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi Jumamosi (14.06.2014) wameidungua ndege ya uchukuzi ya kijeshi ya Ukraine mashariki mwa nchi hiyo na kuuwa watu wote 49 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Ni pigo kubwa kwa wanajeshi wa Ukraine ambao wamekuwa mbioni kuuzima uasi unaohusisha matumizi ya silaha, wa maadui wa serikali mpya ya Ukraine.

Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali imesema wanajeshi 40 na wahudumu 9 walikuwemo ndani ya ndege hiyo chapa Iljushin -II-76 wakati ilipoangushwa mapema leo hii ikikaribia kutuwa katika uwanja wa ndege katika mji wa Luhansk.

Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu imesema uchunguzi wa kihalifu wa tukio hilo umeanza kufanyika chini ya sheria za kupiga vita ugaidi.

Maafa hayo yamepindukia yale ya wanajeshi 12 akiwemo generali mmoja hapo Mei 29 wakati waasi walipoidungua helikopta ya wanajeshi karibu na mji wa mashariki wa Slovyansk.

Tukio hilo linazusha masuala la vipi waasi hao wanapata silaha zao.

Urusi yashutumiwa

Ukraine imekuwa ikituhumu Urusi kwa kuruhusu vifaru vitatu kuvuka mpaka na kuingia Ukraine ambako vinatumiwa na waasi.Urusi imekanusha kuwapatia silaha waasi hao.

Mpiganaji wa waasi mashariki ya Ukraine.
Mpiganaji wa waasi mashariki ya Ukraine.Picha: Reuters

Marekani hapo Ijumaa imeishutumu Urusi kwa kuwapelekea waasi wa Ukraine vifaru na zana za kufyatulia maroketi ambapo naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje Marie Harf amesema wana wasi wasi mkubwa na juhudi za Urusi kuwasaidia waasi hao.

Rais Poroshenko wa Ukraine hapo Alhamisi alimwambia Rais Vladimir Putin wa Urusi kwamba kuvusha vifaru na kuviingiza Ukraine ni "jambo lisilokubalika."

Denis Pushilin kiongozi wa waasi wanaotaka kujitenga wa Jamhuri ya Donetsk ameiambia televisheni ya taifa ya Urusi hapo Ijumaa kwamba waasi wanavyo vifaru hivyo lakini "haitokuwa vyema kuuliza"wamevipata wapi.

Usaliti na ubeuzi

Taarifa ya wizara ya ulinzi imesema waasi kwa "usaliti na ubeuzi" wameidungua ndege hiyo kwa kutumia mizinga na bunduki za rashasha.Imeelezea masikitiko yake kwa familia za wale waliouwawa kutokana na msiba huo mkubwa unaoacha pengo lisilozibika.

Wanajeshi wa Ukraine katika mji wa Mariupol. (13.06.2014)
Wanajeshi wa Ukraine katika mji wa Mariupol. (13.06.2014)Picha: Reuters

Msemaji wa kitengo cha ulinzi cha Jamhuri ya Luhansk ilijiojitangazia uhuru Alexei Toporov amesema ndege hiyo imedunguliwa baada ya kile alichokieleza "watu wanaoukalia kwa mabavu" uwanja wa ndege wa Luhansk kugoma kuzingatia muda wa mwisho waliotakiwa kuondoka kwenye uwanja huo.

Luhansk iko mashariki mwa Ukraine karibu na mpaka na Urusi,eneo ambalo limeshuhudia waasi wakiyanyakuwa majengo ya serikali na kujitangazia uhuru baada ya kuitisha kile walichokiita kura ya maoni yenye utata.

Serikali ya Ukraine imedai kupata mafanikio hapo Ijumaa wakati vikosi vya serikali vilipoyakomboa majengo yaliokuwa yamenyakuliwa na waasi katika mji wa bandari wa Mariupol.Hakuna maafa yalioripotiwa.

Fadhaa na wasi wasi

Umoja wa Ulaya umeelezea kumuunga kwake mkono Rais Petro Poroshenko wa Ukraine anayelemea mataifa ya magharibi kwa kuendeleza mashambulizi yake ya kuutokomeza uasi ambapo Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya Thorbjoern Jagland amesema "amefadhaishwa na kuwa na wasi wasi mkubwa" kutokana na shambulio hilo la kuidengua ndege.

Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya Thorbjoern Jagland.
Katibu Mkuu wa Baraza la Ulaya Thorbjoern Jagland.Picha: DW/Samir Huseinovic

Jagland amesema katika taarifa kwamba "Rais Poroshenko anafahamu kwamba anaweza kutegemea msaada wetu".

Imeripotiwa kusikika kwa milio ya mapambano makali na miripuko kadhaa mizito masaa machache kabla ya kuangushwa kwa ndege hiyo sasa saba za usiku huko Luhansk mji wa wakaazi 400,000 ulioko kilomita 25 magharibi mwa mapaka na Urusi.

Kitovu hicho cha shughuli za viwanda kilikuwa chini ya udhibiti kamili wa waasi tokea kuanza kuzuka kwa vuguvugu la uasi mashariki mwa nchi hiyo hapo mwezi wa Aprili lakini vikosi vya Ukraine viliweza kuendelea kuudhibiti uwanja wake wa ndege na kuutumia kusafirishia zana za kijeshi na vikosi vyake kwa ajili ya operesheni zake za kijeshi za kupambana na waasi.

Mvutano kati ya Ukraine na Urusi ulipamba moto hapo mwezi wa Februari baada ya rais aliekuwa akiiunga mkono Urusi Viktor Yanukovych kuondolewa madarakani na vuguvugu kubwa la maandamano la watu wanaotaka mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya.

Uasi huo wa miezi miwili umegharimu maisha ya takriban watu 320 wakiwemo raia na wapiganaji kwa pande zote mbili serikali na waasi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ AP/AFP

Mhariri:Hamidou Oummilkheir