1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge nchini Kenya waifanyia kazi Miswaada ya Katiba

24 Agosti 2011

Wabunge nchini Kenya wana kibarua cha kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha miswaada iliyosalia ya kikatiba inapitishwa kabla kumalizika mwaka mmoja tangu katiba mpya iidhinishwe tarehe 27 Agosti mwaka uliopita.

https://p.dw.com/p/12MrT
Wananchi wa Kenya wakisubiri kupiga kura ya mabadiliko ya katiba hapo mwaka 2010

Kutoka Nairobi mwandishi wetu Alfred Kiti ametuandalia taarifa hiyo….

Wabunge wameamua kwa kauli moja kuongeza muda vikao vya bunge hadi saa sita usiku na kuamua kufanya kazi hadi siku ya Jumamosi ili kukamilisha miswaada 12 iliyosalia kati ya miswaada 21 iliyotakiwa kupitishwa kabla katiba mpya iweze kufanya kazi kikamilifu kuhakikisha inajadiliwa na kupitishwa.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya utekelezaji katiba Mheshimiwa Abdikadir Mohammed anasema…

“Imefika wakati ambapo Bunge aidha likiuke katiba na liongoze muda wa kupitisha miswaada hii au tufanye kazi usiku na mchana kuhakikisha shuhuli hii inakamilika”.

Mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji Katiba Charles Nyachae amepongeza hatua hiyo akisema…

“Ninafuraha kuona kwamba bunge limejitolea kufanya kazi ya ziada na sisi katika Tume ya Utekelezaji katiba tumekuwa tukifanya kazi kwa masaa 16 hadi 18 kila siku kwa sababu tunataka kuhakikisha kazi hii inakamilika kabla siku ya mwisho iliyowekwa kufika.”

Kwa mujibu wa katiba mpya uchaguzi mkuu ujao unafaa kufanywa mwezi Agosti mwakani jambo ambalo linazua wasiwasi kwamba endapo miswaada iliyosalia ya kikatiba haitapitishwa mapema uchaguzi huo huenda usifanyike wakati huo.

Kamati ya bunge ya utekelezaji katiba hata hivyo imeamua kwa ushirikiano na wizara husika kutenga miswaada mitatu kati ya miswaada 12 iliyosalia na kubaki na miswaada tisa ambayo bunge wakati huu linang'ang'ana kuipitisha kufikia tarehe 27 mwezi huu.

“Miongoni mwa miswaada tuliyokuwa tumewasilisha awali tumeamua kuondoa miswaada mitatu, miwili ya marekebisho ya kikosi cha polisi na mmoja wa uhamiaji”.

Bunge linayo nafasi ya kuongeza muda wa kupitisha miswaada iliyosalia kwa hadi mwaka mmoja lakini hilo linaweza tu kufanyika ikiwa thuluthi mbili za wabunge wataidhinisha hatua hiyo. Na wakati huo huo mtu yeyote anaweza kujitokeza na kwenda mahakamani kupinga hatua hiyo na mahakama kuamuru bunge livunjwe kwani litakuwa limekiuka katiba.

Mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji Katiba Charles Nyachae hata hivyo anaonya akisema..

“Ikiwa tutafikia wakati wa uchaguzi na tuwe na wabunge wa jinsia moja walio zaidi ya thuluthi mbili basi tutakuwa na mzozo mkubwa wa kikatiba na bunge hilo litakuwa limeundwa kinyume na katiba”

Miswaada iliyosalia inaendelea kujadiliwa bungeni hivi sasa huku kukiwa na matumaini kwamba ikiwa wabunge wataendelea na ushirikiano huo hakutakuwa na haja ya muda kuongezwa

Mwandishi: Alfred Kiti DW Nairobi.

Mhariri: Mohamed Abdulrahman