1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Kenya wataka kujipatia mamilioni

Admin.WagnerD11 Januari 2013

Wabunge hao walipitisha muswada huo kisiri ambapo Rais Kibaki atapata jumla ya shilingi milioni 25 kama marupurupu yake ya kustaafu na shilingi milioni moja kila mwezi hadi atapofariki.

https://p.dw.com/p/17Hsm
Fedha za Kenya
Fedha za KenyaPicha: Rafael Belicanta

Hatua ya wabunge wa Kenya kuufanyia marekebisho na kuupitisha mswaada wa sheria ya fedha ambao utawapa fursa ya kwenda nyumbani na kitita cha zaidi ya shilingi milioni 9 kila mmoja, pale bunge litakapovunjwa wiki ijayo, imezua ghadhabu miongoni mwa wananchi na mashirika ya kijamii.

Ni hatua ambayo imezua hisia tofauti tofauti miongoni mwa wananchi. Hata hivyo kuna wale wanaounga mkonoi hatua hiyo.

Mashirika ya kijamii japinga uamuzi wa bunge

Mashirika ya kijamii nayo hayajaachwa nyuma. Mkurugenzi wa shirika la Ahadi Kenya Trust Stanley Kamau anasema: "Pesa inayopewa Rais, pesa inayopewa Waziri mkuu, Makamu wa Rais na Spika wa bunge haistahili kabisa inafaa ipewe wakongwe na watu wanaougua.”

Ikiwa Rais Mwai Kibaki atatia saini mswaada huo, Wabunge hao ambao kipindi chao cha kuhudumu bungeni kinamalizika Jumanne tarehe 15 mwezi huu watapata jumla ya shilingi milioni 9 na laki tatu kila mmoja na marupurupu mengine yakiwemo kupewa mlinzi wa kibinafsi atayelipwa na serikali, kupewa hati ya kusafiria ya kibalozi yaani diplomatic passport na kupewa mazishi ya kitaifa watakapofariki.

Je, rais Mwai Kibaki atasaini muswada?
Je, rais Mwai Kibaki atasaini muswada?Picha: AP Photo

Baadhi ya wabunge waliupinga msaada huo mmoja wao akiwa mbunge wa Makadara Mbuvi Kioko. Wakati wabunge walipofanyia marekebisho ya mswaada huo, mashirika ya kijamii yalifanya maandamano kumtaka rais asikubali kutia saini marekebisho hayo.

Wananchi wataka Kibaki agome kusaini mswaada

"Hatukubali yaliyofanyika bungeni. Kwamba wabunge wamejiamulia kujiongeza ama kujipatia mapato baada ya kukaa bungeni kwa miaka mitano," amesema Robert Alai, mwenyekiti wa kikundi cha Kenyans for Twitter and Facebook.

Viti vilivyogharimu dola 3,000 kila kimoja katika bunge la Kenya
Viti vilivyogharimu dola 3,000 kila kimoja katika bunge la KenyaPicha: Simon Mania/AFP/GettyImages

Lakini kutokana na ukosefu wa wakati hilo halitawezekana kwani ikiwa Rais atakataa kutia saini mswaada huo itabidi urudishwe bungeni kufanyiwa marekebisho na muda haupo tena kwani bunge litakuwa imekamilisha muda wake tarehe15 Jumanne ijayo. Mswaada huo pia unajumuisha vipengele muhimu vya kukusanya ushuru na ikiwa hautatiwa saini serikali haitakuwa na nafasi ya kukusanya ushuru. Uamuzi sasa umebaki na Rais Mwai Kibaki ambaye hata yeye atannufaika atakapotia saini mswaada huo.

Mwandishi: Alfred Kiti

Mhariri: Mohammed Khelef