1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa kuanguka ndege ya Urusi waanza

1 Novemba 2015

Wachunguzi wa kimataifa wameanza kazi ya kutafuta chanzo cha kuanguka kwa ndege ya Urusi iliyokuwa imebeba abiria 224 iliyoanguka katika milima ya Sinai nchini Misri, na kuwauwa abiria wote katika ndege hiyo.

https://p.dw.com/p/1GxoL
Airbus-Absturz über Ägypten Absturzstelle
Mabaki ya ndege ya shirika la ndege la Urusi iliyoanguka nchini MisriPicha: picture-alliance/AP Photo/S. el-Oteify

Hii ni ajali mbaya kabisa kutokea katika ndege za Airbus katika miongo kadhaa iliyopita.

Wakati Urusi leo Jumapili (01.11.2015) ikianza siku moja ya maombolezi kwa ajili ya wahanga wa ajali hiyo, serikali za Misri na Urusi zote zimepuuzia madai kutoka kwa kundi la wanamgambo lenye mafungamano na wapiganaji wa jihadi wa kundi la Dola la Kiislamu kwamba wameiangusha ndege hiyo inayomilikiwa na shirika la ndege la Kogalymavia, chini ya jina la Metrojet.

Waziri mkuu wa Misri Sharif Ismail amesema wataalamu wamethibitisha kwamba wanamgambo hawawezi kutungua ndege katika umbali wa mita 9,000 ambapo ndege hiyo ya Airbus 321 ilikuwa ikiruka, wakati waziri wa usafirishaji wa Urusi Maxim Sokolov amesema madai hayo "hayawezi kufikiriwa kuwa ni sahihi".

Kisanduku cheusi

Kisanduku cheusi cha ndege hiyo kinachonakili data za safari kimepatikana na kupelekwa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini, na jioni ya jana Jumamosi Sokolov na waziri wa masuala ya dharura Vladimir Puchkov wamewasili mjini Cairo na kikosi cha wataalamu kusaidia katika uchunguzi unaoongozwa na Misri.

Airbus-Absturz über Ägypten Absturzstelle
Mabaki ya ndege ya Urusi iliyoanguka nchini MisriPicha: picture-alliance/dpa/Str

Wachunguzi wawili wa ajali za anga kutoka Ufaransa--nchi ambayo inatengeneza ndege hizo chapa Airbus -- pia watasafiri kwenda Misri pamoja na wataalamu sita kutoka shirika la aerospace ili kusaidia katika uchunguzi huo.

Shirika la Ujerumani la Lufthansa, Emirates na shirika la ndege la Ufaransa Air France, yote yamesema yanasitisha safari zake kupitia anga ya Sinai hadi pale sababu zilizosababisha kuanguka kwa ndege hiyo zitakapobainishwa.

Tahadhari kuruka eneo la Sinai

Mwezi Machi mwaka huu, uongozi wa safari za anga nchini Marekani ulishauri ndege za abiria za Marekani kuepuka kurusha ndege zake katika eneo tete la rasi ya Sinai kwa kurusha ndege hizo chini ya futi 26,000.

Ndege , iliyowachukua abria 214 raia wa Urusi , Waukraine watatu na wafanyakazi saba , ilipoteza mawasiliano na kituo cha udhibiti wa safari za anga dakika 23 baada ya kuruka kutoka mji wa kitalii katika bahari ya Sham wa Sham el-Sheikh , ikiwa safarini kwenda katika mji wa Saint Petresburg.

"Kwa bahati mbaya , abiria wote katika ndege hiyo ya Kogalymavia yenye namba za safari 9268 kutoka Sham el-Sheikh kwenda Saint Petresburg wamefariki. Tunatoa rambi rambi kwa familia na marafiki," Ubalozi wa Urusi mjini Cairo umesema.

Urusi imetangaza siku ya leo Jumapili (01.11.2015) kuwa siku ya maombolezi kitaifa kwa ajili ya wahanga ambao ni kuanzia mtoto wa kike wa umri wa miezi 10 hadi mwanamke mwenye umri wa miaka 77.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Isaac Gamba