1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wadhamini wakubaliana kubuniwa maeneo salama Syria

4 Mei 2017

Wadhamini watatu wakuu wa mpango wa usitishwaji mapigano kote nchini Syria, Alhamis walitia saini mkataba wa kubuni maeneo salama, ili kukabiliana na mzozo wa kibinadamu katika nchi hiyo iliyozongwa na vita.

https://p.dw.com/p/2cOKp
Kasachstan Syrien Friedensgespräche in Astana
Picha: picture-alliance/abaca/A. Raimbekova

Makubaliano hayo yalitangazwa wakati wa mazungumzo ya amani katika mji wa Astana nchini Kazakhstan. Lakini wakati ambapo maafisa kutoka Uturuki, Iran na Urusi walipokuwa wakitia saini makubaliano hayo, baadhi ya wawakilishi wa upinzani nchini Syria katika mazungumzo hayo, walipinga na kuondoka katika chumba cha mazungumzo.

Upinzani unapinga kuhusishwa kwa Iran katika mazungumzo hayo, kwani unaishutumu kwa kuhusika pakubwa katika vita vinavyoendelea nchini humo, vita vilivyopelekea zaidi ya watu 400,000 kuuwawa.

Urusi na Iran wanaunga mkono utawala wa sasa wa Syria

Makubaliano hayo ya Kazakhstan yanataka kuundwa kwa maeneo manne salama kaskazini, kati na kusini mwa Syria, ingawa haikuelezwa jinsi mapigano yatapunguzwa katika maeneo hayo.

Russland Türkei - Präsidenten Putin & Erdogan in Sotschi
Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdigan, kushoto, na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, kulia.Picha: Reuters/A. Zemlianichenko

Rais wa Urusi Vladimir Putin alipendekeza katika mazungumzo na mwenzake wa Urusi Reccep Tayyip Erdogan siku ya Jumatano kwamba, ndege za kivita katika maeneo salama kama hayo huenda zikapigwa marufuku.

Urusi na Iran zimekuwa nchi mbili ambazo zinaunga mkono uongozi wa serikali ya Syria nayo Uturuki imekuwa ikiunga mkono baadhi ya makundi ya waasi yanayotaka kupinduliwa kwa rais wa Syria Bashar al-Assad. Mataifa yote matatu lakini yanakubaliana kwamba makundi ya kigaidi nchini humo ni sharti yaangamizwe.

Mkataba huo utatekelezwa Jumamosi

Wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilitoa taarifa Alhamis, ikionesha kufurahishwa kwake na kutiwa saini kwa makubaliano hayo, ikisema makubaliano yanaashiria juhudi zinazofanywa ili kusitishwa matumizi ya silaha ikiwemo ndege za kivita baina ya pande zinazozozana, ili kuwezesha kusambazwa kwa misaada ya kibinadamu.

Wizara hiyo pia ilisema Uturuki itaendeleza juhudi zake za kuhakikisha kwamba hatua ya kusitishwa mapigano iliyoko sasa inaendelezwa ili kupatikane suluhu la kisiasa.

Kasachstan Syrien Friedensgespräche in Astana Opposition
Ujumbe wa waasi katika mazungumzo hayo ya AstanaPicha: Reuters/M. Kholdorbekov

Mkuu wa ujumbe wa Urusi katika mazungumzo hayo ya Astana Alexander Lavrentyev alisema makubaliano ya kubuni maeneo salama yataanza kutekelezwa Jumamosi na jeshi la Syria linatarajiwa kusitisha kuendesha ndege zake katika eneo hilo.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Lavrentyev alisema serikali ya Syria itayatii makubaliano hayo na itakwenda kinyume tu iwapo mashambulizi yatafanywa na makundi ya waasi katika maeneo hayo.

Lakini suala kuhusiana na nchi zipi zitakazosimamia na kuyalinda maeneo hayo salama ni suala ambalo bado halijulikani. Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema Jumatano kwamba, njia za kuyasimamia maeneo hayo litakuwa ni suala litakalohitaji mazungumzo ya kivyake.

Rais Putin alisema Jumatano kwamba, rais wa Marekani Donald Trump anaunga mkono kubuniwa kwa maeneo hayo, kwa mujibu wa mazungumzo waliyoyafanya Jumanne kupitia simu.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/APE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga