1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafadhili wa Kombe la Dunia waiwekea FIFA shinikizo

9 Juni 2014

Wafadhili wa Kombe la Dunia Sony na Adidas wamejitokeza kuelezea wasiwasi wao kuhusiana na madai mapya kuwa hongo zilitolewa ili kuipa Qatar kibali cha kuwa mwenyeji wa dimba la 2022.

https://p.dw.com/p/1CEyt
Symbolbild WM Katar 2022
Picha: picture-alliance/dpa

Kampuni kubwa inayotengeneza bidhaa za elektroniki ya Japan Sony imesema kuhusiana na madai hayo ya hivi karibuni kuwa inataraji kuona “uchunguzi sahihi”. Wiki iliyopita, gazeti la Uingereza la Sunday Times lilifichua kile lilisema kuwa ni ushahidi unaoonyesha nyaraka za benki na barua pepe, ambazo aliyekuwa afisa wa ngazi ya juu wa soka nchini Qatar Mohamed Bin Hammam aliwahonga maafisa wakuu wa soka katika juhudi za kuliunga mkono ombi la nchi yake la kuandaa Kombe la Dunia mwaka wa 2022.

Kampuni ya Sony imesema katika taarifa kuwa “kama mshirika wa FIFA, tunataraji kuona shirika hilo likizingatia kanuni zake za uadilifu, maadili na mchezo wa haki katika masuala yake yote ya utendaji kazi.

Mfadhili mwenzake wa Kombe la Dunia kampuni ya Adidas ilisema katika taarifa tofauti kuwa “picha mbaya ya mjadala wa umma kuhusiana na FIFA kwa wakati huu siyo nzuri kwa mchezo wa kandanda au kwa FIFA na washirika wake”.

Ripoti hiyo ya Sunday Times, pia inamhusisha kwenye kashfa hiyo gwiji wa soka wa Ujerumani Franz Beckenbauer pamoja na Rais wa UEFA Michel Platini.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman