1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Ennahda waandamana

9 Februari 2013

Wafuasi wa Chama tawala chenye itikadi kali za Kiislamu nchini Tunisia cha Ennahda wameandamana leo Jumamosi (09.02.2013) katika mji mkuu wa Tunis.

https://p.dw.com/p/17bPI
Waandamanaji wa Tunisia
Waandamanaji wa TunisiaPicha: Khaled Ben Belgacem

Maandamano hayo yanafanyika ikiwa ni siku moja baada ya polisi kupambana na waandamanaji wakati wa mazishi ya kiongozi wa upinzani Chokri Belaid. Waandamanaji hao baadhi yao wamebeba bendera ya chama huku wengine wakiwa na bendera ya taifa ya Tunusia. Chama hicho kimewakusanya wafuasi wake katikati ya mji wa Tunis kwa lengo la kulitetea bunge halali la nchi hiyo na kupinga ghasia za kisiasa.

Chama hicho kimesema pia kinaandamana kupinga hatua ya Ufaransa kuingilia kati masuala ya kitaifa ya Tunisia, baada ya nchi hiyo kulaani mauaji ya Belaid. Mapema wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Manuel Valls, alisema kuwa mauaji hayo ni kama mashambulizi ya maadili ya mapinduzi ya Jasmine ya Tunisia.

Wito wa kwanza wa Ennahda

Huu ndio wito wa kwanza wa maandamano kutolewa kwa wafuasi wa chama tawala tangu, Belaid alipouawa siku ya Jumatano. Waandamanaji katika mazishi yake Ijumaa, walikilaumu chama cha Ennahda kuhusika na mauaji yake, tuhuma ambazo imezikanusha vikali. Tuhuma hizo zilizotolewa na vyama vya upinzani dhidi ya Ennahda ikiwa ni miezi kadhaa baada ya mvutano kati na wasiasa wa chama cha Kiliberali na wale wenye itikadi kali za Kiislamu kuhusu mustakabali wa baadae wa taifa hilo.

Mabomu ya kutoa machozi yakirushwa kwa waandamanaji
Mabomu ya kutoa machozi yakirushwaPicha: Reuters

Waandamanaji hao walichoma moto makao makuu ya chama hicho kwenye mji wa Sidi Bouzid, eneo ambalo ndio chimbuko la vuguvugu la mapinduzi. Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi wakati baadhi ya waandamanaji walipochoma moto magari wakitaka kufanyika mapinduzi mapya.

Matukio ya jana Ijumaa yameongeza mzozo nchini Tunisia ambako muda wa mpito kutoka utawala wa kidikteta hadi utawala wa kidemokrasia umekumbwa na mgawanyiko na tofauti za kidini, kisiasa na jitihada za kukabiliana na uchumi unaoyumba. Vikosi vya usalama na vifaru vimetawanywa leo kuzunguka mtaa wa Habib Bourguiba, eneo kuu la vuguvugu la mapinduzi ya mwaka 2011 yaliyouondoa madarakani utawala wa Zine El Abidine Ben Ali. Maandamano hayo yanaonekana kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea tangu yale ya Januari 14 mwaka 2011, siku ambayo Ben Ali alikimbilia uhamishoni Saudi Arabia anakoishi hadi sasa.

Jebali arudia kauli yake

Saa chache baada ya mauaji ya Belaid, Waziri Mkuu wa Tunisia, Hamadi Jebali alitangaza pendekezo la kuunda serikali mpya ya wataalamu wasiohusika na upande wowote wa kisiasa, jambo ambalo limekataliwa na chama cha Ennahda. Jebali alirejea kauli yake hiyo jana jioni, huku akitoa ahadi ya kujiuzulu wadhfa wake iwapo bunge lililochaguliwa halitakubali pendekezo la baraza lake la mawaziri.

Ingawa Jebali amesema ana uhakika wa kuungwa mkono na chama cha Ennahda, chama chake awali kilikataa pendekezo hilo. Sahbi Atig, kiongozi wa Ennahda bungeni, amemkosoa Jebali akisema kuwa hakushauriana kwanza na chama chake, huku afisa mwingine wa ngazi ya juu wa chama hicho akisisitiza haja ya ya kuiendeleza serikali halali ya umoja wa kitaifa.

Waziri Mkuu wa Tunisia, Hamadi Jebali
Waziri Mkuu wa Tunisia, Hamadi JebaliPicha: AFP/Getty Images

Ama kwa upande mwingine, shirika la kusimamia haki za binaadamu nchini Tunisia limesema kuwa vitisho vimekuwa vikiendelea chini ya serikali inayoongozwa na Ennahda na limetoa wito wa kulindwa kwa wanasiasa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE
Mhariri: Stumai George