1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Gaddafi waandamana Benghazi

5 Agosti 2015

Wafuasi wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi wameandamana katika mji wa mashariki wa Benghazi, wakipaza sauti "Muammar, Muammar" kabla ya kutimuliwa na wapinzani wa utawala wake.

https://p.dw.com/p/1GAC3
Hali ya maisha katika mji wa Benghazi.Wakaazi wanamkaribisha msemaji wa jenerali Khalifa HiftarPicha: DW/M. Olivesi

Yadhihirika kama kwamba hakuna aliyejeruhiwa miongoni mwa dazeni kadhaa za wafuasi wa muimla huyo wa zamani aliyepinduliwa na kuuliwa mwaka 2011, ambaye mauaji yake yalizusha vurugu mpaka leo, huku serikali mbili hasimu zikiundwa zinazopigania madaraka huku wanamgambo wa itikadi kali wakiendelea kupanua ushawishi wao.

Wafuasi wa Gaddafi walikuwa wamebeba picha za kiongozi huyo aliyeiongoza Libya kwa muda wa miaka 42 na kutaka aachiliwe huru mtoto wake maarufu wa kiume, Saif al-Islam, aliyehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama moja ya mjini Tripoli wiki iliyopita bila ya mwenyewe kuwepo mahakamani.

Seif al-Islam, aliyekutikana na hatia ya uhalifu, anashikiliwa na kundi la waasi wa zamani la Zintan, eneo lisilotii amri ya Tripoli. Makundi yanayopigania haki za binaadamu yanazungumzia dosari katika hukmu dhidi ya Seif al-Islam.

Wafuasi wa Gaddafi watimuliwa kwa risasi na mawe Benghazi

"Mungu pekee, Muammar na Libya" ndio kauli mbiu ya waandamanaji hao waliokuwa wakipeperusha bendera ya kijani ya utawala wa zamani na ambao walitawanyika baada ya wakaazi wengine, baadhi yao wakibeba bendera mpya ya taifa ya Libya, kufyetua risasi.

Saif al-Islam Gaddafi
Seif al Islam akisikiliza kesi dhidi yake huko ZintanPicha: Reuters/Stringer

Wakaazi wa Benghazi wanasema hii ni mara ya kwanza kwa wafuasi watiifu kwa Gaddafi kuandamana katika mji huo wa pili kwa ukubwa wa Libya - kitovu cha mapinduzi ya mwaka 2011.

Hali ya kukata tamaa imeenea miongoni mwa Walibya kufuatia vurugu na kuwepo serikali mbili zinazopigania madaraka kwa msaada wa waasi wa zamani waliogawika kisiasa, kikabila na kimkoa.

Mji wa Benghazi umeathirika vibaya sana kutokana na mapigano kati ya vikosi vinavyoshirikiana na serikali rasmi yenye makao yake makuu mashariki na makundi ya itikali kali yaliyoifunga bandari na kuzuwia ngano, chakula na mafuta kuingia katika eneo hilo.

Mji mkuu, Tripol,i unadhibitiwa na serikali hasimu na kusababisha serikali inayotambuliwa kimataifa kukimbilia mashariki ya Libya.

Human Rights Watch yataka uchunguzi ufanywe

Wakati huo huo, shirika linalopigania haki za binaadamu la Human Rights Watch limetoa wito wa kufanyika uchunguzi baada ya kusambazwa picha za vidio katika mitandao ya kijamii inayoonyesha jinsi Saadi, mtoto mwengine wa kiume wa Muammar Gaddafi, alivyokuwa akiteswa katika jela moja ya mjini Tripoli. Shirika hilo linaitaka pia serikali ya Libya iwasitishe kazi "walinzi na watumishi wengine wa jela wanaohusika na kisa hicho."

Combobild Amnesty International und Human Rights Watch Logos
Nembo ya mashirika yanayopigania haki za binaadam ;Amnesty International na Human Rights WatchPicha: picture-alliance/dpa, Getty Images

Picha hizo za vidio zimesambazwa siku chache tu baada ya Seif al-Islam kuhukumiwa adhabu ya kifo pamoja na viongozi wengine wanane wa utawala wa zamani wa baba yake, ikiwa ni pamoja na waziri mkuu wa zamani, Baghdadi al-Mahmoud,i na kiongozi wa zamani wa idara ya upelelezi, Abdallah Senoussi.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP'
Mhariri: Josephat Charo