1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa Rousseff waitisha maandanamo Brazil

18 Machi 2016

Wafuasi wa Rais Dilma Roussef wa Brazil wametowa wito wa kufanyika kwa maadamano ya umma Ijumaa (17.03.2016) kumuunga mkono na kujibu mapigo kwa mzozo wa kisiasa unaotishia kumuangusha madarakani.

https://p.dw.com/p/1IFgf
Rais Dima Rousseff wa Brazil na rais wa zamani Luiz Inacio Lula Da Silva wakati wa kuteuliwa wake kwa wadhifa wa mnadhimu mkuu wa serikaii Brasilia. (17.03.2016)
Rais Dima Rousseff wa Brazil na rais wa zamani Luiz Inacio Lula Da Silva wakati wa kuteuliwa wake kwa wadhifa wa mnadhimu mkuu wa serikaii Brasilia. (17.03.2016)Picha: Reuters/R. S. Filho/Brazilian Presidency

Polisi ilibidi kutumia mabomu ya mshutuo na gesi ya kutowa machozi jana usiku kuwatawanya waandamanaji wenye hasira waliokuwa wanadai kujiuzulu kwa Rais Roussef wakati kambi yake ya sera za mrengo wa kushoto nayo ikijiandaa kukabiliana na upinzani dhidi yake.

Kambi yake imeitisha maandaamano leo hii katika miji zaidi ya 30 ikiwa ni nafasi ya kuonyesha nguvu zao baada ya watu zaidi milioni tatu kujiunga na maandamano dhidi ya serikali mwishoni mwa juma lililopita.

Maandamano hayo yanafuatia sakata la kisiasa baada ya hapo jana wabunge kuanzisha upya mchakato wa kumshtaki Rais Rouseff mweyne umri wa miaka 68.

Mahakama yakwamisha uteuzi wa Lula

Wakati hayo yakijiri mahakama imekwamisha juhudi za kumrudisha katika baraza la mawaziri mtangulizi wake mwenye ushawishi mkubwa Luiz Inacio Da Silva katika baraza la mawaziri.Rouseff na washirika wake wanapambana kuzima madai ya rushwa dhidi yao na kukabiliana na hali ya kutoridhika kwa wananchi kutokana na kuporomoka vibaya kwa uchumi.

Maandamano ya kumpinga Rais Dilma Rousseff na uteuzi wake wa Luiz Inacio Lula da Silva.Brasilia. (17.03.2016)
Maandamano ya kumpinga Rais Dilma Rousseff na uteuzi wake wa Luiz Inacio Lula da Silva.Brasilia. (17.03.2016)Picha: Reuters/R.Moraes

Pigo hilo kwa Roussef linakuja siku moja baada ya ushahidi mpya wa kashfa ya rushwa ambapo mawasiliano ya simu yaliumbuwa njama kati ya Roussef na mtangulizi wake Lula.Roussef alimwapisha Lula mwenye umri wa miaka 70 kama mnadhimu wake mkuu hapo jana.

Jaji mjini Brasilia ametowa hukumu ya kusitisha uteuzi huo kutokana na madai kwamba rais huyo alikuwa akijaribu kumlinda Lula kutokana na madai ya rushwa kwa kumpa kinga ya kutoshtakiwa kwa mawaziri wanapokuwepo madarakani.

Hukumu hiyo ilibatilishwa jana usiku wa manane kwa rufaa lakini mahakama nyengine tafauti ya Rio de Janeiro imefunguwa shauri jengine lenye kuzuwiya uteuzi huo wa Lula.

Kusudio la mapinduzi

Wakati wa kumuapisha Lula hapo jana Rais Roussef aliwashutumu maadui zake kwa kutaka kumpinduwa.

Maandamano ya kumpinga Rais Dilma Rousseff na uteuzi wake wa Luiz Inacio Lula da Silva.Brasilia. (17.03.2016)
Maandamano ya kumpinga Rais Dilma Rousseff na uteuzi wake wa Luiz Inacio Lula da Silva.Brasilia. (17.03.2016)Picha: Reuters/P.Whitaker

Roussef amesema "Kuitigisha jamii ya Brazil chini ya misingi isio na ukweli ,mbinu za hila na vitendo vinavyoshutumiwa mno vyenye kukiuka hakikisho la katiba na kuanzisha mifano mibaya sana.Hivyo ndivyo yanavyoanzia mapinduzi:“

Matukio ya hapo jana yamezidi kuitumbukiza serikali ya Roussef katika dimbwi la mashaka wakati ikikabiliana na hasira ya umma,matatizo ya kiuchumi na kugawika kwa muungano wake katika bunge.

Lula na Roussef kati yao wameiongoza Brazil kwa miaka 13 iliopita. Lula aliiongoza Brazil wakati uchumi ulipokuwa ukinawiri lakini matatizo ya kiuchumi na kisiasa hivi sasa yanaliandama taifa hilo kubwa kabisa la Amerika Kusini.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri :Yusuf Saumu