1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafuasi wa siasa kali watiwa mbaroni kwa ugaidi Ujerumani

Iddi Ssessanga
1 Oktoba 2018

Mwendesha mashtaka nchini Ujerumani ameamuru kukamatwa kwa watu sita wanaotuhumiwa kuunda kundi la kigaidi la mrengo mkali wa kulia na kupanga kuwashambulia wahamiaji katika mji wa Chemnitz mashariki mwa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/35nXq
Chemnitz Deutschland Rechtsextremismus Neo-Nazis
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Meyer

Karibu maafisa 100 wa polisi walivamia majengo kadhaa katika majimbo ya Saxony na Bavaria mapema Jumatatu asubuhi kama sehemu ya uchugnuzi dhidi ya kundi la kigaidi la itikadi kali za mrengo wa kulia la "Revolution Chemnitz," lililopewa jina la mji wa Chemnitz ambao ulishuhudia maandamano makubwa ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia hivi karibuni, kufuatia mauaji ya mwanaume wa Kijerumani yaliodaiwa kuwahusisha wahamiaji.

Wanaume sita waliokamatwa, wakiwa na umri wa kati ya miaka 20 na 30, wanashukiwa kuunda kundi la kigaidi chini ya uongozi wa Christian K. mwenye umri wa miaka 30, aliekamatwa septemba 14. Kwa mujibu wa waendesha mashitaka wa serikali ya jimbo, wanaume hao walikuwa wamepanga kuwashambulia "wageni" na watu wenye mitazamano ya kisiasa inayotofautiana na ya kwao.

Wachunguzi wamesema kundi hilo lilijaribu kupata silaha za kisasa, na Septemba 14, walishiriki katika mashambulizi ya kupanga dhidi ya wageni mjini Chemnitz kwa kutumia chupa za bilauri, glavu za mapambano ya mkono kwa mkono, na vifa vya kurusha kwa umeme. Mwanaume mmoja alijeruhiwa katika shambulizi hilo. Wachunguzi wamelielezea tukio hilo kama "zoezi lililofanywa" kujiandaa na shambulizi kubwa zaidi lililopangwa kufanyika Oktoba 3.

Deutschland Demonstration Pro Chemnitz
Wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wakiandamana mjini Chemnitz, katika jimbo la Saxony, Septemba 21, 2018.Picha: picture-alliance/dpa

Taarifa ya waendesha mashtaka ilisema wanaume hao sita wote walikuwa wanachama wa makundi ya wahuni na wanazi mamboleo katika eneo la Chemnitz, na wote walijichukulia kama wanachama wa juu wa kundi la siasa kali za mrengo wa kulia jimboni Saxony. Waendesha mashtaka wanaamini lengo la kundi hilo lilikuwa "kupindua utawala wa kidemokrasia wa sheria" kwa misingi ya itikadi yao kali ya mrengo wa kulia.

Wanaume hao wote saba watafikishwa katika mahakama ya shirikisho siku za Jumatatu na Jumanne.

Maandamano ya Chenmitz

Mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Chemnitz ulishuhudia makabiliano kadhaa mwishoni mwa mwezi Agosti na mwanzoni mwa Septemba, baada ya mwanaume Mjerumani mwenye asili ya Cuba, kufariki kutokana na majeraha aliyoyapata kwa kuchomwa kisu, wakati wa makabiliano na waomba hifadhi kutoka Syria na Iraq. Mtuhumiwa wa Kiiraqi aliachiwa baadae.

Kifo hicho kilisababisha maandamano ya wiki nzima ambayo baadhi ya wakati yalikumbwa na vurugu yakihusisha wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wapinzani wao, na kusababisha kufanyika kwa tamasha la kupinga ubaguzi lililohudhuriwa na watu zaidi ya 60,000.

Matukio hayo yaliamsha tena hali ya wasiwasi nchini Ujerumani kuhusiana na wimbi la wakimbizi walioingia humo miaka mitatu iliyopita, ambapo vurugu zinazohusisha wahamiaji zilivutia nadhari kubwa ya vyombo vya habari na hatimaye kusababisha ugonvi wa kisiasa: mkuu wa shirika la upelelezi wa ndani la Ujerumani Hans-Georg Maassen, alipoteza kazi yake baada ya kuhoji hadharani ukweli wa picha za video zilizoonyesha wahamiaji wakishambuliwa mjini Chemnitz.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW https://bit.ly/2QkBI2g

Mhariri: Mohammed Khelef