1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafugaji Kenya kunufaika na Bima ya mifugo

Flora Nzema8 Novemba 2013

Bima ya Mifugo Nchini Kenya imeimarisha maisha ya wafugaji, ambapo idadi kubwa ya wafugaji sasa wanalipwa mifugo yao inayopotea kwa kuibiwa au kuathirika na majanga kama vile ukame.

https://p.dw.com/p/1AE8l
Maisha ya kuhama kutoka eneo moja hadi jingine kwa wafugaji
Maisha ya kuhama kutoka eneo moja hadi jingine kwa wafugajiPicha: Getty Images

Mfugaji kutoka eneo la Marsabit, Hussein Ahmed, ni mmoja wa watu wanaonufaika na Bima hiyo, ambaye alipoteza mifugo yake yote kufuatia ukame ulioikumba nchi hiyo mwaka juzi.

Hussein Ahmed anasema wakati wote anakumbuka sauti za kengele iliyofungwa kwenye miguu ya ng'ombe ambayo humburudisha wakati akirudisha mifugo kutoka malishoni, sauti azipendazo kuzisikia katika dunia hii.

Lakini, Amhed ambaye ni mfugaji kutoka eneo la Marsabit nchini Kenya ana masikitiko kufuatia kupoteza mifugo yake yote mwaka juzi, wakati wa janga kubwa la ukame liliyoikumba Kenya katika kipindi cha zaidi ya miaka 60 iliyopita, na kulazimika kusafiri kwenda katika nchi jirani ya Ethiopia kutafuta maji kwa ajili ya mifugo yake.

Husafiri kilomita 250 kutafauta malisho ya wanyama

Anasema alilazimika kusafiri umbali wa kilomita 250 kutoka Marsabit kuelekea Ethiopia alipokuwa akikimbiza mifugo yake kutokana na janga hilo na wimbi kubwa la wizi wa mifugo, lakini matokeo yake alipoteza mifugo yote baada ya kukosa eneo la malisho ya wanyama hao na maji.

Ahmed ameliambia shirika la habari la IPS kuwa, kabla ya janga la ukame alikuwa ameshapoteza idadi kubwa ya mifugo yake kutokana na kuibiwa.

Ukame ni tatizo kwa wafugaji kutokana na mifugo kufa kwa kukosa chakula
Ukame ni tatizo kwa wafugaji kutokana na mifugo kufa kwa kukosa chakulaPicha: Fatoumata Diabate/Oxfam

Mwezi mmoja baadaye alirejea tena Marsabit akiwa mikono mitupu lakini jamaa yake katika ukoo ambaye alikuwa amekata Bima ya mifugo alimpatia ng'ombe mmoja na mbuzi watano na kuanza upya kufuga.

Kwa sasa maisha ya Ahmed yamebadilika ambapo amefanikiwa kurejesha mifugo yake yote na kuikatia Bima ya mifugo na hata kama kutatokea tatizo la ukame na wizi wa mifugo, atakuwa salama.

Mfugaji huyo amejiunga na Bima ya mifugo tangu mwaka jana, Bima pekee kwa wafugaji nchini Kenya, inayofadhiliwa na Taasisi ya Kimataifa ya utafiti wa mifugo na amekwishanufaika na Bima hiyo mara mbili baada ya kulipwa mifugo iliyopotea.

Bima hiyo ilianzia utaratibu wake katika eneo la Marsabiti lakini sasa huduma hiyo imeenea katika maeneo ya Isiolo na Wajir yaliyopo Kaskazini mwa Kenya na kuna mpango wa kuisogeza huduma hiyo katika maeneo ya wafugaji, Afrika Mashariki.

Wafugaji 4,000 wanufaika na Bima ya mifugo

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, jumla ya wafugaji 4,000 au nusu ya wafugaji nchini Kenya wamejiunga na Bima hiyo, ingawa ni vigumu kutaja idadi kamili ya wafugaji kutoka na tabia ya wafugaji ya kuhama eneo moja hadi jingine, anasema afisa mmoja anayeshughulikia mazingira Kaskazini mwa Kenya, Teresia Njeri.

Ingawa kwa mujibu wa takwimu za wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini humo, wafugaji huchangia makadirio ya Dola milioni 800 za Marekani kwenye pato la taifa, wakati takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa jumla ya pato la taifa Kenya ni dola bilioni 37.

Hata hivyo maisha ya wafugaji Kenya bado ni magumu hasa kuanzia kipindi cha mwezi Juni hadi Desemba wakati ambapo kunakuwa na ukame na hali hiyo huendelea kuwa mbaya kati ya Januari na Aprili ambapo mifugo inakuwa katika hatari ya kufa kwa njaa au kuibiwa, anasema Issa Salesa mfugaji kutoka eneo la Isiolo.

Eneo la malisho ya mifugo
Eneo la malisho ya mifugoPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa mfugaji mwingine kutoka Marsabit anayenufaika na Bima hiyo ya mifugo, Yusuf Aden wanaonufaika wanalipa Bima ya Dola 20 za Marekani kwa mwaka.

Mwandishi: Flora Nzema/IPS

Mhariri: Josephat Nyiro Charo