1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafungwa wateswa Afghanistan

MjahidA22 Januari 2013

Umoja wa Mataifa umesema kuwa polisi na maafisa wa ujasusi nchini Afghanistan wanaendelea kuwatesa wafungwa waliokamatwa katika vita vinavyoungwa mkono na mataifa ya Magharibi dhidi ya waasi nchini humo.

https://p.dw.com/p/17PJT
Moja ya jela, Afghanistan
Moja ya jela, AfghanistanPicha: AP

Mateso haya yanatokea wakati kukiwa na juhudi mbali mbali za kukomesha mateso wanayopata wafungwa wa Afghanistan.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, baadhi ya mateso wanayopata wafungwa hao ni kupigwa, mateso ya kutumia umeme, kufungwa kwa minyororo mikononi kuning'inizwa kwa masaa mengi na hata vitisho vya kunyanyaswa kimapenzi.

Ripoti hiyo ya kurasa 139 ni muendelezo wa ripoti nyengine inayoelezea mateso kama hayo nchini humo takribani mwaka mmoja uliopita. Ripoti hii imekuja wakati serikali ya Afghanistan ikitaka udhibiti kamili wa jela na wafungwa wote kutoka kwa Kikosi cha Majeshi ya Ushirika yanayohudumu chini Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini humo, ISAF.

Bendera ya Umoja wa Mataifa
Bendera ya Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, kutokana na matukio mapya ya mateso katika maeneo tofauti ya wafungwa, ikiwemo mahali ambako majeshi ya kimataifa ISAF ilipokuwa imewahamisha wafungwa wake, ilipelekea jeshi hilo kuwacha kusafirisha wafungwa kutokana na taarifa za mateso zilizofichuliwa katika maeneo walikokuwa wafungwa hao.

Karzai ataka wafungwa kuwa chini ya udhibiti wake

Huku hayo yakiarifiwa, bado Rais wa Afghanistan Hamid Karzai anasisitiza kuwepo kwa uhamishaji wa wafungwa ili wawe chini ya udhibiti wa serikali yake, akisema kuwa ni swala la mamlaka ya nchi wakati ambako majeshi ya kimataifa yanajitayarisha kuondoka ifikapo mwaka wa 2014.

Msemaji wa Rais Karzai, Aimal Faizi, alisema nchi hiyo bado haijatuhumiwa kwa maswala ya uhalifu dhidi ya binaadamu, wala mateso na kusema kuwa jambo la kuwatesa wafungwa ni kinyume cha sera yake ni jambo ambalo Afghanistan haiwezi kufanya.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai
Rais wa Afghanistan Hamid KarzaiPicha: Reuters

Faizi amesema huenda kukawa na aina fulani ya mateso kwa wafungwa inayoendelea ndani ya jela za nchi hiyo, kama inayosema ripoti ya Umoja wa Mataifa, lakini tayari wameshaanzisha uchunguzi na watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kando na hayo, msemaji huyo amesema wanachukulia kwa umakini na umuhimu mkubwa mambo yaliyosemwa katika ripoti hiyo lakini pia wanajiuliza ni kwa mantiki gani ripoti hiyo ilikusanywa na ni vipi walivyopata ushahidi wao.

Habari hizi za kutatanisha kuhusu mateso ya wafungwa nchini Afghanistan zinakuja wakati Marekani ikijadili kuhusu mpango wa usalama kati yake na Kabul ili kuwepo kwa mahusiano baada ya kuondoka majeshi ya Marekani mwaka wa 2014. Majadiliyano hayo pia yataangazia iwapo kuna umuhimu wa kuwepo kwa vikosi vya Marekani kusaidia Afghanistan kupambana na waasi wa Taliban.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef