1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagabon wasubiri matokeo ya uchaguzi.

31 Agosti 2009

Wagabon wanasubiri matokeo ya uchaguzi uliofanyika jana kujua nani atakayemrithi marehemu Omar Bongo aliyekuwa madarakani kwa miaka 40.

https://p.dw.com/p/JM0Z
Marehemu Omar Bongo, aliyekuwa rais wa Gabon.Picha: picture-alliance/dpa

Wagombea watatu wakuu tayari kila mmoja ameshajitangazia ushindi, hata kabla ya matokeo rasmi ya awali kuanza kutangazwa. Munira Muhammad ana taarifa kamili.

Jana jioni pale zoezi la kupiga kura lilipomalizika, wagombea wa urais walikuwa na matumaini makubwa, baada ya Wagabon kujitokeza kwa wingi kupiga kura. Hii ni licha ya matatizo ya awali- pale vituo vingi vya kupiga kura katika mji mkuu wa Libreville kufunguliwa kwa kuchelewa kutokana na kwamba maafisa wa uchaguzi hawakuwepo.

Äthiopien Gipfeltreffen der Afrikanischen Union AU Präsident Omar Bongo Gabon
Omar Bongo aliitawala Gabon kwa miaka 41.Picha: AP

Leo Wagabon wameamkia kusubiri- nani kati ya wagombea watatu wakuu atakayechukua mahali pa marehemu Omar Bongo ambaye wengi wao tangu kuzaliwa kwao hawajaona rais mwingine kwa miaka 41, ambayo Bongo amekuwa madarakani.

Pengine ni ile dhamira ya kumrithi Bongo, baada ya muda mrefu ndiyo iliozusha msisimko mkubwa katika uchaguzi huo wa Gabon. Wagombea wote watatu akiwemo mwanawe Bongo- Ali Ben Bongo wameshajitangaza kwamba wameshinda. Ben Bongo ambaye anapigiwa upatu kuibuka na ushindi anajivunia uungwaji mkono wa chama tawala cha Gabonese Demokratic na pia kampeini yenye fedha na ushawishi mkuu.

Akizungumza wakati kila mmmoja anasubiri matokeo ya uchaguzi- Ben Bongo alisema ana imani Wagabon watamvika kofia ya uongozi, kwa kuwa walikuwa na imani naye. Bongo ambaye alihudumu kama waziri wa usalama katika serikali ya babaake alitoa wito wa kuwepo na utulivu wakati huu wa kihistoria nchini Gabon.

Wagombea wengine wawili wanaomhemea Bongo mgongoni ni pamoja na kiongozi wa upinzani Pierre Mamboundou na waziri wa zamani wa mambo ya ndani Andre Mba Obame.Wawili hawa pia wameshatangaza kwamba wanaamini pia wameshinda uchaguzi huo.

Mpinzani mwingine wa Bongo, Casimir Oye Mba alijiondoa jana. Mba ambaye alikuwa waziri mkuu wa zamani alisema alijiondoa kwa sababu tayari ameona shughuli nzima ya uchaguzi ina walakini na inatishia kuingiza Gabon katika wimbi la machafuko.

BdT Junge in Libreville, Gabon
Wagabon wanasubiri matokeo ya uchaguzi wa jana.Picha: AP

Wagombea kadhaa pia wamekosoa orodha ya wapigaji kura nchini Gabon wakisema laki nane wenye haki ya kupiga kura ni ya juu sana katika nchi yenye idadi ya watu milioni moja na lakini tano.

Gabon ni nchi ya nne katika jangwa la Sahara yenye utajiri wa mafuta, ndiye nchi ya tatu duniani inayotoa madini ya Manganese - yanayotengeneza vyuma. Gabon pia ni nchi ya pili barani Afrika inayotoa mbao.

Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman