1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wageni na uchaguzi wa Ujerumani

Saumu Mwasimba
6 Septemba 2017

Wajerumani wenye asili ya kigeni wahimizwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kuamua hatma ya nchi hiyo inayonyemelewa na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia

https://p.dw.com/p/2jQOL
Deutschland Aydan Özoguz
Picha: picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kila mwenye uraia wa Ujerumani na aliyefikisha umri wa miaka 18 anahaki ya kupiga kura nchini Ujerumani tarehe 24 mwezi huu wa Septemba.Watakaopiga kura kuamua mwelekeo wa kisiasa Ujerumani haijalishi wanakotokea,iwe ni familia kutoka Kolon au  kutoka Kazakhstan au hata Uturuki na Poland. Mmoja kati ya wapiga kura 10 ambao bila shaka pia wanahaki ya hata kugombea binafsi ana mizizi ya uhamiaji. Wengi ya watu hao ama wameishi na kuwa na haki ya kuwa na uraia wa kijerumani au hata kuzaliwa ndani ya Ujerumani. Kundi hili la wapiga kura ndilo linaloangaaliwa kwa makini na vyama mbali mbali pamoja na vyombo vya habari na hasa baada ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AFD kuonekana kuzirandia kura za wahamiaji milioni 3.1  kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa mwaka 2016 wengi kutokea nchi za uliyokuwa muungano wa Sovieti.

Wahamiaji walio na uraia wa kijerumani wanahaki ya kupiga kura kama raia mwingine yoyote wa Ujerumani.Kuna wahamiaji kutoka nchi mbali mbali wanaoishi nchini Ujerumani na kuchukua uaraia wa taifa hili,Kundi kubwa la wahamiaji hao ni kutoka nchi za uliokuwa muungano wa Kisovieti.Kundi la pili ni la watu wenye asili ya Uturuki .Takwimu zinakadiria kwamba kuna kiasi wahamiaji 730,000 wenye asili ya kituruki wenye haki ya kupiga kura.Kundi hili tayari limeshaonywa na rais wa Uturuki kutothubu kupigia kura wagombea wa CDU SPD au chama cha kijani.

Mwito kwa wageni

Lakini Aydan Özoguz mwanasiasa wa chama cha SPD ambaye anajukumu la kiserikali la kushughulikia suala la wakimbizi,wahamiaji na ujumuishaji wa wahamiaji katika jamii ya Kijerumani anawatolea mwito kwamba wasikubali kushawishiwa na Erdogan dhidi ya misingi ya jamii ya Ujerumani.

Deutschland Aydan Özoguz
Picha: picture alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Wanasiasa wa Ujerumani wamekuwa wakiwahimiza sana jamii ya Waturuki nchini Ujerumani wenye uraia wa kijerumani kutojiweka nyuma na badala yake wajitokeze kupiga kura. Aliyepewa jukumu la kuwajumuisha wageni katika jamii ya kijerumani na vyama vya muungano serikalini Cemile Gioussouf akizungumza kupitia kituo cha redio cha Ujerumani amewaambia wahamiaji wa jamii ya kituruki kwamba suala la uchaguzi linahusu maisha yao nchini Ujerumani na katu rais Erdogan hawezi kuwasaidia na kuyatafutia ufumbuzi matatizo ya Waturuki wanaoishi Ujerumani. Raia wengi wa Ujerumani wenye asili ya uhamiaji wamekuwa na maswali mengi kuhusu jinsi ya kupiga kura nchini Ujerumani amesema Aydan Özoguz na ndio sababu ameanzisha mpango maalum wa kutoa maelezo kwa kundi hili la wapiga kura,mpango huo unajulikana kama ''Vote D''.

Binafsi Özoguz wazazi wake wanatokea Uturuki na yeye akazaliwa mjini Hamburg.Leo hii ni mmoja wa manaibu  viongozi wa chama cha SPD na  na anashiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi kama ambavyo pia anafanya Cemile Gioussouf wa chama cha CDU.Wote ni miongoni mwa wabunge 37 wa bunge la Ujerumani wenye  asili ya kigeni nchini Ujerumani katika bunge la wabunge 631.Hata hivyo bado kuna tatizo kwamba kiasi nusu ya wageni wanaoishi Ujerumani kwa muda mrefu  bado hawana uraia wa kijerumani. Hii inamaanisha kundi hili limetengwa kwa mfumo fulani kushiriki mchakato wa kisiasa nchini humu.

Wageni walengwa

Lakini pia mwanasiasa wa SPD Özoguz anasema hatua kubwa imepigwa nchini Ujerumani lakini bado yapo mengi yakufanywa linapokuja suala la wageni.Mwanasiasa huyo anasema mtu yoyote mwenye asili ya kigeni ndiye mlengwa mkubwa wa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia.

Deutschland SPD zur Bilanz der großen Koalition
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

''Kwa pande zote nahisi  kuna mengi bado yakufanywa.Upande mmoja unawahusu wahamiaji wenyewe ambao wanabidi wajitahidi kuwa na nguvu katika vyama na kwa upande mwingine ni wa vyama venyewe vinabidi kuwa wazi na kundi hili kuwaambia kwamba wanataka kuwasaidia kwasababu tunawajali na  mna umuhimu katika jamii na ni kiunganisho muhimu katika nchi hii kwa wageni wanaokuja nchi hii''

Mwaka 1994  Kansela wakati huo Helmut Kohl akihutubia bungeni  aliwahi kujitokeza mtu akahoji tangu lini kukaweko kiongozi katika chama cha kisiasa nchini Ujerumani mwenye asili ya kigeni?Mtu huyo alikuwa akimlenga kiongozi wa chama cha Kijani Cem Özdemir.Özdemir alikuwa ni Mjerumani wa kwanza mwenye asili ya kituruki kuingia bungeni.Leo hii kuna wabunge 11 wenye asili ya kituruki na kuifanya kuwa jamii kubwa ya wageni kuwasilishwa kikamilifu katika siasa za Ujerumani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/Grunau Andrea

Mhariri:Iddi Ssessanga