1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni nani atakayeiongoza FIFA?

29 Oktoba 2015

Orodha ya majina ya viongozi saba watakaowania urais wa Shirikisho la Kandanda Duniani - FIFA imetolewa. Uchaguzi mkuu wa Fifa unatarajiwa kuandaliwa Februari 26 mwakani mjini Zurich

https://p.dw.com/p/1GwKF
Kandidaten des Fifa-Präsidentenamtes

Wagombea hao ni Mwanamfalme Ali bin al-Hussein, mwenye umri wa miaka 39 ambaye ni rais wa Shirikisho la Kandanda la Jordan.

Katika kinyang'anyiro hicho cha kumrithi Sepp Blatter, yupo katibu mkuu wa Shirikisho la Kandanda Ulaya - UEFA Gianni Infantino, raia wa Italia mwenye umri wa miaka 45.

Musa Bility raia wa Liberia mwenye umri wa miaka 48 ni rais wa wa Shirikisho la Kandanda la Liberia.

Mgombea mwingine ni mtendaji mkuu wa zamani wa FIFA, Jerome Champagne, Mfaransa mwenye umri wa miaka 57.

Rais wa Shirikisho la Kandanda la Asia Sheikh Salman bin Ebrahim al-Khalifa, akiwa na umri wa miaka 49 pia anatafuta nafasi ya kumrithi Blatter

Mwingine anayewania kiti hicho ni waziri wa zamani wa Afrika Kusini Tokyo Sexwale, mwenye umri wa miaka 62.

Na wa mwisho ni Michel Platini rais wa shirikisho la Kandanda Ulaya UEFA aliyesimamishwa uongozi kwa siku 90 na tume ya maadili ya FIFA kwa tuhuma za rushwa. Atapewa nafasi ya kugombea kiti hicho ikiwa adhabu yake ya kufungiwa itaisha kabla ya muda wa uchaguzi.

Jina la mchezaji wa zamani wa Trinidad na Tobago, David Nakhid, halikujumlishwa katika orodha hiyo licha ya nyota huyo kusema aliwasilisha jina lake katika kuwania nafasi hiyo.

Uchaguzi mkuu wa Fifa unatarajiwa kuandaliwa Februari 26 mwakani katika mkutano wa baraza kuu la FIFA mjini Zurich, Uswisi.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Caro Robi