1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea waahidi serikali ya umoja wa kitaifa Afghanistan

Abdu Said Mtullya5 Septemba 2014

Nato imeridhika na ahadi iliyotolewa na wagombea urais nchini Afghanistan ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kuyatia saini makubaliano ya kuyaruhusu majeshi ya kimataifa yaendelee kuwapo nchini humo.

https://p.dw.com/p/1D7bH
Mgombea uchaguzi wa rais nchini Afghanistan Abdullah Abdullah
Mgombea uchaguzi wa rais nchini Afghanistan Abdullah AbdullahPicha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Mahasimu katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais nchini Afghanistan wamewasilisha ujumbe kwa madola ya Nato kuhaidi kwamba wataunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kuuondoa mkwamo wa kisiasa uliofuatia matokeo ya uchaguzi. Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa Nato Rasmussen,amesema anauliunga mkono pendekezo hilo.V

Ujumbe huo uliowaslishwa kwa vongozi wa nchi za Nato wanaokutana Wales una lengo la kuuondoa wasi wasi miongoni mwa viongozi hao ambao ungeweza kusababisha kuondolewa kwa majeshi ya kimataifa nchini Afghanistan.

Wagombea uchaguzi hao Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah pia wameahidi kuyatia saini makubaliano ya kisheria ya kuyaruhusu majeshi ya kimataifa kuendelea kuwapo nchini Afghanistan hadi mwaka ujao.

Makubaliano kuruhusu majeshi ya kimataifa nchini Afghanistan.

Mahasimu hao wamesema wapo tayari kuyatia saini makubaliano hayo kwa moyo wote yatakayowaruhusu wakufunzi wa Nato kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Afghanistan baada ya Nato kuzimaliza operesheni za mapambano nchini humo mnamo mwezi wa Desemba.

Wanasisa hao, Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah wamesema wana imani na mchakato wa kisiasa wa kuwajumuisha watu wote wa Afghanistan .Ujumbe wa wanasiasa hao ulisomwa mjini Kabul na mpambe wa bwana Abdullah Abdullah.

Mazungumzo juu ya kugawana mamlaka baina ya wanasiasa hao yalivunjika mnamo wiki hii na hivyo kusbabisha wasiwasi juu ya kutokea ghasia za kikabila nchini Afghanistan.

Hesabu za awali zilionyesha kuwa bwana Ashraf Ghani alikuwa mbele ya bwana Abdullah Abdullah.Lakini Bwana Abdullah anadai kwamba udanganyifu wa kura ulifanyika. Hapo awali ujumbe wa bwana Abdullah uliamua kujitoa katika hesabu za kura zilizofanywa na wasimamizi wa Umoja wa Mataifa baada ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi. Ujumbe wa bwana Abdullah Abdullah ulisema kuwa haukuridhika na jinsi kura za mashaka zilivyoshughulikiwa.

Wasi wasi juu ya hali ya kisiasa

Mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Nato unafanyika Wales katika muktadha wa wasi wasi wa kutokea vurumai za kisiasa nchini Afghanistan hali ambayo ingeweza kusababisha Nato izimalize harakati za kupambana na Taliban zilizochukua muda wa miaka zaidi ya 10.

Mambo yamezidi kuwa ya mkanganyiko baada ya kupatikana habari kwamba Kanali wa jeshi la Afghanistan ameomba hifadhi ya ukimbizi baada ya kuwasili chini Uingereza. Hata hivyo Waziri wa ulinzi wa Afghanistan Khan Mohammad amezikanusha habari hizo. Amesema Kanali huyo kwanza hakuwamo katika ujumbe wa Afghanistan unaohudhuria mkutano wa Wales.

Mwandishi:Mtullya Abdu.rtre

Mhariri: Josephat Charo