1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wajieleza mbele ya Baraza Kuu la UN

Isaac Gamba13 Aprili 2016

Kwa mara ya kwanza Umoja wa Mataifa umeweka wazi mchakato wa kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa baada ya kutoa nafasi kwa mataifa yote kuwauliza maswali wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

https://p.dw.com/p/1IUTU
Picha: Getty Images/AFP/K. Betancur

Hatua hii inaonekana kuvunja sasa mazingira ya siri yaliyokuwepo hapo kabla katika mchakato wa kujaza nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni miaka 70 tangu kuanzishwa kwa umoja huo.

Wagombea watatu miongoni mwa tisa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo walipata nafasi ya kuulizwa maswali na kuelezea mipango yao ya baadaye katika utendaji wao iwapo watafanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya kumalizika muda wa uongozi wa Katibu Mkuu wa sasa Ban Ki-moon hapo January 1, mwakani.

Kwa miongo kadhaa sasa mchakato wa uchaguzi wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umekuwa ukifanyika katika mazingira ya siri chini ya usimamizi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaloundwa na wajumbe kutoka nchi wanachama wa baraza hilo ambazo ni pamoja na Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Marekani.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilibadilisha utaratibu wa awali

Hata hivyo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka jana lilipiga kura kubadilisha utaratibu huo na kuwataka wagombea wa nafasi hiyo kuwasilisha barua za maombi, kutoa muhtasari wa malengo yao pamoja na kuwa tayari kujieleza na kuulizwa maswali.

Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: Reuters/D. Balibouse

Uamuzi wa mwisho wa uteuzi wa nafasi hiyo bado unabakia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini hatua hiyo ya kuweka uwazi katika mchakato huo utaweka msukumo kwa mataifa hayo yenye nguvu kuteua jina la mtu ambaye atakuwa anakubalika kwa kiwango kikubwa.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mogens Lykketoft alisikika akisema kuwa haya ni mabadiliko muhimu.

" Iwapo kutakuwa na idadi kubwa ya nchi zinazomuunga mkono mgombea mmoja sidhani kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakuja na jina tofauti na hilo " alisema.

Waziri wa Mambo ya nje wa Montenegro Igor Luksic mwenye umri wa miaka 39 ambaye ni mgombea kijana kuliko wote waliojitokeza kuwania nafasi hiyo alikuwa wa kwanza kujieleza mbele ya wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akielezea jinsi atakavyotumia uzoefu wake wa nafasi alizowahi kushika katika nchi yake ikiwemo uwaziri mkuu katika kuwania nafasi hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la sayansi, Elimu na Utamaduni-UNESCO Irina Bokova pamoja na mtendaji mkuu wazamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia masuala ya wakimbizi ambaye pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Ureno Antonio Guterres ni miongoni mwa waliopata nafasi ya kujieleza mbele ya baraza hilo.

Mkurugenzi Mkuu wazamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi(UNHCR) Antonio Guterres
Mkurugenzi Mkuu wazamani wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi (UNHCR) Antonio GuterresPicha: picture-alliance/dpa/O. Panagiotou

Kwa mujibu wa Katiba ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huchaguliwa na wajumbe kutoka nchi wanachama 193 wa umoja huo kutokana na mapendekezo yaliyowasilishwa na wajumbe kutoka nchi wanachama 15 zinazounda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Isaac Gamba/ APE/AFPE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo