1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahamiaji wanapogeuka mpira nchini Ufaransa

Admin.WagnerD19 Aprili 2012

Wakati kampeni za duru ya kwanza ya uchaguzi nchini Ufaransa jumapili ijayo zikifikia hatua ya lala salama, wachambuzi wanasema wagombea wa kiti cha urais wanaendelea kutumia neno mhamiaji kama mpira.

https://p.dw.com/p/14h2x
wagombea wa kiti cha urasi nchini Ufaransa
Wagombea wa kiti cha urais nchini UfaransaPicha: dapd/AP

Wote wanatumia ujumbe wa kuwashawishi wapiga kura na baadhi wanaashiria kwamba kuwafukuza wahamiaji ndiyo suluhisho la matatizo ya Ufaransa. Lakini wahamiaji hao hasa ni kina nani?

"Kwa matazamo wa baadhi ya watu, mhamiaji ni yule anayefanana tofauti na wao", anasema Profesa Nonna Mayer, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi cha Po, na mataalamu wa masomo ya ubaguzi wa rangi. Profesa Mayer aliliambia shirika la habari la IPS kuwa miongoni mwa wale wanaoitwa wahamiaji wapo wanaochukiwa zaidi ambao ni Wafaransa wenye asili ya maghrebi, wakati wanaochukiwa kidogo ni Mayahudi.

Francois Hollande akifanya kampeni
Francois Hollande akifanya kampeniPicha: picture-alliance/dpa

Sheria za Ufaransa zinakataza upambanuzi wa wananchi lakini utafiti uliyofanywa na shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) unaonyesha idadi ya wahamiaji nchini humo ni asilimia 10 ya raia wote milioni 63. Karibu theluthi moja ya watu hao ni kutoka nchi za umoja wa Ulaya. Lakini hao siyo walengwa wakuu wa wanasiasa.

Walengwa wakuu ni Waislam
Katika mdahalo moja juu ya uchaguzi wa Ufaransa, wiki iliyopita, Mayer na wanasayansi ya jamii wengine walibaini kuwa kwa ujumla neno uhamiaji linatumiwa sana kumaanisha Waislamu. Kampeni dhidi ya uhamiaji zinazoendeshwa na vyama kama kile cha Mrengo wa kulia cha National Front, ni ukataaji wa Uislamu ndani ya Ufaransa, walisema wachambuzi hao.

Mkuu wa chama cha National Front, Marine Le Pen amegeuza masuala yahusuyo uchinjaji wa wanyama kama vile uuzaji wa nyama halali kama mojawapo ya mambo muhimu katika kampeni yake. Amejaribu kuwavutia wapiga kura kwa kuwaelezea kuwa mamilioni ya wafaransa wanakula nyama ya halali bila wao kujua.

Marine Le Pen
Marine Le PenPicha: AP

Le Pen amekosoa pia hatua ya Waislam kuswalia mitaani, na kuielezea hatua hiyo kama uvamizi. Septemba mwaka jana, Ufaransa ilipiga marufuku swala za mitaani licha ya ukweli kuwa baadhi ya waislamu wapatao milioni tano nchini Ufaransa hawana nafasi ya kuswalia. Hili lilikuja muda mfupi baada ya kupigwa marufuku kwa vazi la niqaab kwa wanawake.

Sarkozy adandia hoja ya Le Pen
Ingawa Le Pen anajaribu kutofautisha kati ya Waislam wafaransa wanaoipenda Ufaransa na wale wenye itikadi kali, wafuasi wake hawaoni tofauti. Kwa sasa mwanamama huyo anashika nafasi ya tatu katika kura za maoni na anaonekana kuwa na nafasi ndogo ya kushinda uchaguzi katika duru ya pili lakini mkakati wake umedandiwa na rais wa sasa Nicolas Sarkozy anayekabana koo na msoshalist Francois Hollande. Kuna wagombea kumi wa kiti cha urais nchini humo.

Mayer aliiambia IPS kuwa Sarkozy alikuwa akitumia suala la uhamiaji kupata kura za watu wa itikadi ya mrengo wa kulia na kwamba matamshi yake kuhusu uhamiaji na Uislamu yamebadilika sana tofauti na zamani. Hii ilidhihirika Julai mwaka 2010 aliposema kuwa serikali ya ufaransa ingefuta uraia wa watu wanaooneka kutishia maisha ya maafisa wa polisi na watu wengine wenye mamlaka katika jamii.

Wafuasi wa Hollande katika mkutano wa kampeni
Wafuasi wa Hollande katika mkutano wa kampeniPicha: Reuters

Hii ilifuatia hatua yake ya kuamrisha kufukuzwa kwa wagypsy wa Roma wanaoishi nchini humo kinyume na sheria, jambo lililosababisha Ufaransa kukaripiwa na Umoja wa Ulaya. Tangu wakati huo, matamshi ya Sarkozy yanalenga kumzidi kete Le Pen. Mwezi uliyopita alisema Ufaransa imekuwa nchi ya wahamiaji wengi na aliahidi kupunguza uhamiaji endapo atachaguliwa kwa mara ya pili.

Wogombea wamkana Le Pen
Lakini vyama vingine vimepinga kuwalenga wahamiaji na vimemshtumu Le Pen na chama chake kuwa wabaguzi. Jean Luc Mlenchon, kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto cha Front de Gauche amemuita Le Pen mtu aliepungukiwa na akili na mnafiki na kwamba chama chake ni cha kibaguzi.

Hollande kwa upande wake ameendelea kuwa na msimamo wa wastani na kusisitiza kuwa ni jukumu la Ufaransa kuunganisha wahamiaji wake katika jamii, na amekuwa akikutana na viongozi mbalimbali wa dini na kuwaelezea mawazo yake na kuwaomba kumuunga mkono. Yeye ameelekeza nguvu zake kwa matajiri ambao amesema atawaongezea kiwango cha kodi.

Francois Hollande na Nicolas Sarkozy
Francois Hollande na Nicolas SarkozyPicha: AP

Mchambuzi wa masuala ya siasa na mwandishi wa vitabu Alan Riding anasema Hollande hazungumzii hofu za watu na wala hawapi matumaini. Lakini asilimia kubwa wa Wafaransa wenye asili ya uhamiaji waliyofanyiwa utafiti walisema watachagua chama cha kisoshalisti.

Nadia, mhasibu mwenye umri wa miaka 30 aliehamia jijini paris na wazazi wake akiwa na umri wa miaka 13, aliiambia IPS kuwa yeye na marafiki zake watamchagua Hollande au hawatachagua kabisaa. "Huwezi kuwachagua watu wanaokufanya ujiskie kama mtu asiyetakiwa," alisema.

Viongozi wa dini nao wapaza sauti
Claude Baty, rais wa waprotestant wapato 800,000 nchini Ufaransa na ambao wamekuwa wakilalamikia kubaguliwa mara kwa mara, alisema inatokea hofu juu ya mtu mtu mwingine ikasababisha tabia fulani, linakuwa jambo la dharura kuchukua hatua zinazolenga kuwatofautisha watu na mazoea.

Baty alisema anasononeshwa sana na kampeni hizi kwa vile wanasiasa wanakuwa kama watoto walioko katika uwanja wa mpira. Baty na viongozi wengine wa dini wanasema wanasiasa wanatumia karata ya uhamiaji ili kuwatoa wapiga kura kwenye masuala muhimu kama vile uchumi na kushindwa kwa sekta ya elimu.

Mgombea wa chama cha Parti de Gauche, Jean-Luc Melenchon
Mgombea wa chama cha Parti de Gauche, Jean-Luc MelenchonPicha: Reuters

Lakini Mayer aliiambia IPS kwamba anategemea uvumilivu kurejea baada ya uchaguzi maana Ufaransa imekuwa nchi inayokaribísha watu wanaotafuta hifadhi. Ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) inaonyesha kuwa Ufaransa ilipokea maombi 51,910 ya hifadhi mwaka 2011, hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 8 kutoka mwaka wa 2010, ikiwa ni ya pili baada ya Marekani.

Wengi wa wakimbizi hawa ni kutoka Afghanistan, ambako majeshi ya Ufaransa yanashiriki katika juhudi la kulinda amani na Mayer anasema hii inaongeza dhana kuwa wahamiaji wengi zaidi wanakwenda nchi Ufaransa. Lakini aliongeza kuwa vyama vikubwa kama kile cha rais Nicolas Sarkozy vilikuwa vinacheza mchezo wa hatari kwa kuunga mkono mawazo ya itikadi kali kutoka watu wa mrengo wa kulia kuhusu wahamiaji.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\IPS

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman