1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Magharibi zaonyesha mshikamano dhidi ya Urusi

Josephat Charo
27 Machi 2018

Wahariri wamejishughulisha na mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki nchini Bulgaria na kuendelea kuzuiwa kiongozi wa zamani wa Catalonia, Carles Puigdemont.

https://p.dw.com/p/2v3Ik
USA Ausweisung sechzig russischer Diplomaten auf Grund der Vergiftung des ehemaligen russischen Spions
Picha: Getty Images/C. Somodevilla

Mada iliyohanikiza katika magazeti ya Ujerumani leo ni kufukuzwa kwa wanadiplomasia wa Urusi kutoka Marekani, Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya. Gazeti la Frankfurter Rundschau linaandika: Sasa muungano kati ya Marekani, Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya unakaza skrubu, kujibu shambulizi la sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi, Sergei Sripal nchini Uingereza, taifa ambalo pia liliwafurusha wanadiplomasia wa Urusi.

Mhariri anasema ni hatua sahihi kuonyesha mshikamano na Uingereza na hivyo kuongeza shinikizo la kidiplomasia kwa Urusi. Pia inaonesha licha ya tofauti ya maoni, mataifa ya Magharibi bado yanaweza kuungana wakati wa matatizo. Hata hivyo mhariri anatilia maanani ingekuwa bora kwenda mbali zaidi kutafuta ufumbuzi badala ya kila mara kuzozana na jirani mkaidi, Urusi.

Nalo gazeti la Badische Neueste Nachrichten la mjini Karlsruhe kuhusu mada hii linasema hii ni hatua halisi ya kipekee ambayo inaweza kumtia tumbo joto rais wa Urusi, Vladimir Putin. Kwa sababu Putin hamuheshimu mpinzani aliye dhaifu. Hata hivyo, mhariri anasema, hatua hii isionekane kama tangazo la vita na Urusi kwani nchi hiyo inabaki kuwa mshirika muhimu wa Ujerumani na mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten nalo linasema hatua hii haitaubadili msimamo wa Urusi kuendelea kukanusha madai ya kuhusika na shambulizi dhidi ya Skripal. Mhariri wa gazeti la Freie Presse la mjini Chemnitz anasema mshikamano ni dhahiri kabisa. Waziri mkuu wa Ungereza Theresa May anakabiliwa na shinikizo kutokana na suala la Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya, Brexit. Mzozo huu na Urusi unampunguzia shinikizo hilo, japo kidogo na kwa muda tu. Kwa hivyo mtu anaweza kusema Urusi ni adui mzuri.

Mkutano kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya

Mada nyingine iliyozingatiwa na wahariri ni mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki. Gazeti la Nürnberger Zeitung limeandika: Hoja au nyenzo zinazotumiwa na mataifa ya magharibi na hususan Umoja wa Ulaya katika mkutano wa kilele mjini Varna nchini Bulgaria ni dhaifu.

Bulgarien EU- Türkei Gipfel: Präsident Donald Tusk, Tayyip Erdogan und Jean-Claude Juncker
Rais wa Umoja wa Ulaya, Donald Tusk (kushoto) rais Recep Tayyip Erdogan (katikati) na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude JunckerPicha: Reuters/S. Nenov

Wito wa kiongozi wa chama cha Kijani Ujerumani, Claudia Roth, kutaka mikataba kuhusu wakimbizi kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ifutwe, imeibua hasira, pamoja pia na kauli ya kansela wa Austria, Sebastian Kurz, kutaka mazungumzo juu ya Uturuki kutaka uanachama wa Umoja wa Ulaya yavunjiliwe mbali. Katika matukio haya mawili, rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, hatasita hata kwa sekunde moja kuzitumia hatua hizi kama silaha dhidi ya Umoja wa Ulaya.

Puigdemont aendelea kuzuiwa Ujerumani

Kuendelea kuzuiwa kiongozi wa zamani wa Catalonia, Carles Puigdemont, nchini Ujerumani pia kumewashughulisha wahariri leo. Mhariri wa gazeti la Sächsische la mjini Dresden anasema haijalishi ikiwa Puigdemont atawasilishwa kwa Uhispania ama la. Serikali ya shirikisho la Ujerumani imekuwa mshirika muhimu katika mzozo huu kana kwamba imeombwa kufanya hivyo. Mhariri anasema serikali inapaswa kubadili msimamo wake. Ingefaa kupatanisha upande wa waasi na rais wa Uhispania Mariano Rajoy.

Belgien Carles Puigdemont
Carles Puigdemont, kiongozi wa zamani wa CataloniaPicha: picture-alliance/dpa/AP/O. Matthys

Gazeti la Allgemeine la mjini Mainz kuhusu mada hii linauliza: Je, itakuwaje iwapo serikali ya Uhispania itaendesha kesi kama maigizo dhidi ya waasi wanaotaka kujitenga? Je, kufanya hivyo kutadhihirisha nguvu za serikali ya mjini Madrid? Ingawa Puigdemont hatakuwa salama Uhispania, angeweza kuwa salama katika mahakama za Ulaya. Mhariri anamalizia kwa kusema mahakama za Ujerumani hazitakiwi kuliruhusu hilo kutokea.

Jeshi la Ujerumani limepungukiwa na fedha

Kuhusu kauli aliyoitoa waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen, nchini Afghanistan kwamba fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya jeshi kwa mujibu wa mkataba ulioiunda serikali ya mseto hazitoshi, gazeti la Mannheimer Morgen linasema: Ni hatua inayokaribia ushupavu kwa waziri huyo kutoa kauli yake, sio mahala pengine bali Afghanistan!

Mhariri anasema von der Leyen anafahamu fika fedha zinazohitajika ni euro bilioni 15 katika mpango wa fedha hadi mwaka 2021 kukidhi mapungufu yaliyopo maana aliandikiwa takwimu zote na kukabidhiwa kabla mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto mjini Berlin. Mhariri anaibua hoja akisema waziri huyo lakini hakuwasilisha madai haya katika mazungumzo hayo.

Mwandishi: Josephat Charo/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef