1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahouthi wauwa 60 Aden

Mohammed Khelef
1 Agosti 2019

Makombora yaliyorushwa na waasi wa Kihouthi katika mji wa Aden ulio kusini mwa Yemen pamoja na mashambulizi kadhaa ya kujitoa muhanga yameuwa zaidi ya watu 60 hivi leo na kuwajeruhi wengine kadhaa.

https://p.dw.com/p/3N9da
Jemen Anschlag auf Polizeikräfte in Aden
Picha: Reuters/F. Salman

Shahidi mmoja aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba aliona miili tisa baada ya mripuko kutokea kwenye kambi ya kijeshi inayomilikiwa na kikosi maalum cha Yemen kinachoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo imo kwenye muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kupambana na Wahouthi.

Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha hospitali, miongoni mwa watu 51 waliouawa, yumo kamanda wa kijeshi. Chanzo chengine kilicho karibu na jeshi la serikali kimemtambua kamanda huyo kuwa Brigedia Jenerali Muneer al-Yafee, mmoja wa viongozi wakubwa wa kijeshi kusini mwa Yemen.

Yafee alikuwa ndio kwanza ameshuka jukwaani kumuamkia mgeni rasmi wakati bomu liliporipuka. Kwenye gwaride hilo, bendera za zamani za iliyokuwa Yemen Kusini na zile za makundi yanayounga mkono ushirika wa kijeshi dhidi ya Wahouthi zilikuwa zimetanda, huku bendi ya kijeshi ikitumbuiza.

Mashahidi wanasema wanajeshi walisikika wakipiga makelele na kuwakimbilia waliojeruhiwa kuwawahisha hospitalini. Sare, viatu, na vifaa vyengine vya kijeshi vilikuwa vimechawanyika aridhini na huku vikiwa vimetapakaa damu.

Jemen Anschlag auf Polizeikräfte in Aden
Mashambulizi kwenye gwaride la kijeshi katika kambi ya Al Jalaa siku ya tarehe 1 Agosti 2019 yaliuwa zaidi ya watu 60.Picha: Reuters/F. Salman

Kituo cha polisi chashambuliwa

Shirika la Madaktari Wasiokuwa na Mipaka (MSF) lilituma taarifa kupitia mtandao wa Twitter kwamba makumi ya watu waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu mjini Aden baada ya mripuko huo, lakini baadaye shirika hilo lilisema kwamba mashambulizi mengine tafauti yalifanyika kwenye kituo kimoja cha polisi kusini mwa mji huo wa bandari. Taarifa hiyo ilisema watu kumi waliuawa na wengine 16 kujeruhiwa.

Kituo rasmi cha televisheni kinachoendeshwa na Wahouthi, Al Masirah, kilisema kundi hilo lilifanya mashambulizi kwa kutumia makombora ya masafa ya kati na ndege isiyo rubani dhidi ya gwaride hilo la kijeshi, ambalo kimesema lilikuwa ni matayarisho ya uvamizi dhidi ya majimbo yanayoshikiliwa na kundi hilo.

Chanzo chengine kimeliambia shirika la habari la AP kuwa bomu liliripuka nyuma ya jukwaa ambalo sherehe zilikuwa zikifanyika kwenye kambi ya kijeshi ya Al Jalaa wilaya ya Buraiqa.

Muungano unaoungwa mkono na mataifa ya Magharibi ukiongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu uliingia kijeshi nchini Yemen mwaka 2015 kwa madai ya kuirejesha madarakani serikali inayotambuliwa kimataifa iliyokuwa imepinduliwa mwaka 2014 mjini Sanaa na Wahouthi. 

Hata hivyo, wengi wanasema lengo la uvamizi huo wa kijeshi lilikuwa ni kuizuwia Iran kujipenyeza kwenye taifa hilo masikini la Kiarabu kupitia utawala wa Kihouthi, ambao nao ni sehemu ya madhehebu ya Shia.