1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wairaq Waitaka Marekani kuondoka Iraq miaka minne Baada ya kuvamia

9 Aprili 2007

Maelfu ya wananchi wa Iraq wameandamana kwa amani katika barabara za mji mtakatifu wa madhehebu ya washia wa Najaf kuadhimisha miaka minne tangu kung’olewa madarakani kwa utawala wa Marehemu Saddam Hussein.

https://p.dw.com/p/CB4p
Marehemu kiongozi wa zamani wa Iraq Saddam Hussein
Marehemu kiongozi wa zamani wa Iraq Saddam HusseinPicha: AP

Miaka minne iliyopita macho ya ulimwengu mzima yalikuwa yakikodolewa Iraq ambako wanajeshi wa Marekani waliisaidia kuliangusha sanamu kubwa la Saddam Hussein lililokuwa katikati ya mji wa Baghdad kuashiria mwisho wa enzi ya utawala dhalimu wa Saddam Hussein.

Maelfu ya wairaqi walicheza kwa furaha na shangwe.

Lakini sasa kila kitu kimebadilika na hali imewatumbukia nyongo kwani mauaji yamegeuka kuwa kitu cha kawaida nchini humo.

Kile kilichoanza kuonekana kama ni mashambulio ya waasi wa kisuni dhidi ya wanajeshi wa Marekani na Iraq baada ya uvamizi wa mwaka 2003 kimegeuka sasa na kupanuka zaidi nakuwa mauaji ya kimadhehebu kati ya washia waliowengi na wasunni waliowachache ambao walikuwa wakitamba wakati wa Saddam.

Isitoshe hali inatia wasiwasi zaidi kwani mwanzilishi wa vita vya Iraq Gorge W Bush anaongeza kikosi zaidi cha wanajeshi 30,000 elfu nchini Iraq hasa katika mji wa Baghdad hatua ambayo inaonekana kama ndio nafasi ya mwisho ya kuumaliza mzozo wa Iraq.

Hii leo kukiwa na marufuku ya kutoendesha magari kwa saa 24 katika mji wa Baghdad maelfu ya watu walijitokeza kuadhimisha miaka minne tangu kuondolewa madarakani utawala wa Saddam Hussein.

Polisi wameimarisha usalama katika maeneo mbali mbali ya Iraq.

Maelfu kwa maelfu ya wairaqi wameitikia mwito wa kiongozi wa kidini Muqtada Al Sadr wa kuhudhuria maandamano makubwa ya kupinga uvamizi wa Marekani.

Maelfu ya washia wengi wakiwa wanaume na vijana wakiume walisafiri kwa mabasi na magari ya binafsi hadi mji wa Najaf kumuunga mkono Muqtada al Sadri.

Katika mji huo mtakatifu wa washia wa Najaf kusini mwa Baghdad waandamanaji waliomiminika kwa wingi walibeba bendera za Iraq wakipiga kelele za kuilaani Marekani na wanajeshi wake na kumsifu kiongozi wa huyo wa kidini.

Maandamano ya leo yameitishwa na kiongozi huyo wa kidini mwenye usemi mkubwa nchini Iraq Muqtada Al Sadri ambaye anaongoza idadi kubwa ya wabunge katika serikali ya Iraq inayoshikiliwa na washia wengi.

Kutoka mahali pasipojulikana hapo jana kiongozi huyo anayeikosoa Marekani alitoa taarifa ya kuwataka wanamgambo wake kuongeza nguvu katika vita vyao vya kuwashinda waamarekani.

Sadri alilitaka jeshi la Mehdi na vikosi vya usalama vya Iraq kuacha kupigana katika eneo hatari la Diwaniyah ili kuepuka mtego wa wanajeshi wa Marekani ambao anasema wamechochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iraq.

Wairaqi na wanajeshi wa Marekani wamekuwa wakipambana na wanamgambo katika mji huo wa Diwaniyah tangu siku ya ijumaa pale wanajeshi hao wa Marekani walipoanzisha opresheni ya kuukomboa mji huo kutoka kwa jeshi la Mehdi.

Tayari hii leo mwanajeshi mmoja wa Marekani ameuwawa katika mji huo.

Jeshi la Marekani limesema Sadr pamoja na jeshi lake la Mehdi wanapasa kulaumiwa kwa kuchochea machafuko ya kimadhehebu nchini Iraq.