1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waislamu milioni 3 waanza ibada ya hijja mjini Mecca

Mohamed Dahman6 Desemba 2008

Mamia kwa maelfu wa mahujaji wa Kiislam leo wameanza ibada ya hija kwa kuelekea kwenye kambi ya hema nje ya mji mtakatifu wa Mecca katika utaratibu wa kupita kwenye njia alizopita Mtume Muhammad SAW karne 14 zilizopita.

https://p.dw.com/p/GAiL
Maelfu kwa maelfu ya Waislamu wakifanya ibada ya hijja katika msikiti mkuu wa Mecca.Picha: AP

Takriban Waislamu milioni 3 wamewasili katika mji huo mtakatifu wa Mecca wiki hii kwa ibada hiyo ya Hijja huku kukiwa na operesheni kubwa ya usalama kuepusha mashambulizi yoyote yale ya wanamgambo wa itikadi kali za Kiislam, mkanyangano wa watu au harakati za kisiasa ambazo zinaweza kuifedhehesha Saudi Arabia.

Baadhi ya mahujaji walikuwa wakitembea kwa miguu wakiwa na mikoba yao wengine wakiwa kwenye mabasi yanayokwenda kwa mwendo wa pole miongoni mwa umati mkubwa kuelekea Mina mashariki mwa mji wa Mecca.Mahujaji hao watanategemewa kuwasili hapo kesho asubuhi katika Mlima Arafa kama kilomita 15 mashariki ya Mecca.Wanaume walikuwa wamevalia mavazi meupe yenye kuashiria kutakasika na kuwa sawa chini ya Mwenyeenzimungu na wanawake wakiwa wamejifunika kuanzia kichwani hadi miguuni isipokuwa kwa nyuso na mikono yao walikuwa wamekusanyika mjini Mecca hapo jana.

Sikukuu ya Eid el Adha au sherehe ya kuchinja mnyama itaanza siku ya Jumatatu wakati mahujaji hao watakapoanza siku tatu za kupiga mawe nguzo kama ishara ya kumlaani shetani.

Hija ambayo ni mojawapo ya nguzo kuu za Kiislamu inatakiwa kutimizwa na kila Muislamu mwenye uwezo wa na afya angalau mara moja katika uhai wake.

Saudi Arabia imeweka takriban wana usalama 100,000 kuweka utulivu wakati wa kipindi cha siku tano cha hija.