1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waisrael washiriki katika uchaguzi mkuu

17 Machi 2015

Vituo vya kupigia vimefunguliwa kote nchini Israel hii leo asubuhi katika uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kuamua hatma ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu ambaye amekuwa madarakani kwa miaka sita.

https://p.dw.com/p/1ErsU
Picha: Reuters/Baz Ratner

Zaidi ya wapiga kura milioni tano na laki nane wanatarajiwa kupiga kura kuwachagua wabunge wapya 120 katika uchaguzi ambao unaonekana kama kura ya maoni kuhusu utawala wa Waziri mkuu Benjamin Netanyahu na chama chake cha Likud.

Akizungumza baada ya kupiga kura yake asubuhi katika shule moja mjini Jerusalem, Netanyahu amesema hataunda serikali ya muungano na chama cha leba iwapo atashinda, bali ataunda serikali ya kizalendo na vyama vya mrengo wa kulia.

Netanyahu anatafuta muhula wa nne madarakani lakini itachukua wiki kadhaa ya mazungumzo kuhusu kuundwa kwa serikali ijayo baada ya uchaguzi kujua iwapo atasalia madarakani au atabanduliwa na mpinzani wake wa karibu Isaac Herzog wa chama cha sera za wastani cha umoja wa Uzayuni.

Netanyahu hatakubali kuwepo taifa la Palestina

Katika siku ya mwisho ya kampeni hapo jana, Netanyahu aliapa kuwa hataruhusu kuundwa kwa taifa la Palestina iwapo atachaguliwa tena na kuwarai wapiga kura kumchagua ili wapinzani wake wasiingie madarakani na kuhujumu usalama wa Israel na udhibiti wa mji wa Jerusalem.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akipiga kura
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akipiga kuraPicha: picture-alliance/AP Photo/Sebastian Scheiner

Hii itakuwa mara ya tatu Israel inafanya uchaguzi mkuu tangu mwaka 2009 badaa ya Netanyahu kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema kufuatia tofauti ndani ya serikali yake ya muungano iliyotishia kuusambaratisha utawala wake.

Kura za maoni kabla ya uchaguzi huu wa leo zimeonyesha chama cha Likud cha Netanyahu kiko nyuma ya chama cha umoja wa Uzayuni kwa kama viti vinne.

Herzog ambaye amedokeza kuwa huenda akagawana madaraka na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Israel Tzipi Livni ameahidi kurekebisha uhusiano na wapalestina na jumuiya ya kimataifa na kuangazia kuboresha viwango vya maisha kwa kuboresha uchumi.

Iwapo watafanikiwa kuunda serikali ijayo, Herzog na Livni watahudumu miaka miwili kila mmoja kama waziri mkuu. Waziri mkuu mpya wa Israel atakabiliwa na kibarua kigumu cha kushughulikia changamoto kadha wa kadha za ndani ya Israel na zinazohusiana na sera za kigeni ikiwemo suala tete la mpango wa kinyuklia wa Iran, kuboresha uhusiano na Marekani na kuimarisha uchumi wa taifa hilo.

Kiongozi mpya atakuwa na kibarua kigumu

Masuala mengine yanayomsubiri kiongozi mpya wa Israel ni uhusiano tete na Palestina baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya kutafuta amani mwaka jana, msukosuko uliosababishwa na vita vya Gaza vya mwaka jana na mzozo wa kisheria katika mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita.

Rais wa Israel Reuven Rivlin mjini Jerusalem
Rais wa Israel Reuven Rivlin mjini JerusalemPicha: picture-alliance/Zumapress/Xinhua/Li Rui

Kuambatana na sheria za Israel matokeo kamili ya uchaguzi sharti yatangazwe katika kipindi cha siku nane baada ya kura lakini matokeo ya awali yanatarajiwa kunaza kutolewa hapo kesho.

Baada ya matokeo kujulikana, Rais Reuven Rivlin ana siku saba za kushauriana na viongozi wa kila chama cha kisiasa kinachowakilishwa bungeni kuhusu ni nani wangependa awe waziri mkuu kisha atamchagua mmoja wa kiongozi wa chama anayeamini ana nafasi nzuri za kuunda serikali.

Rivlin amewaomba raia wa nchi hiyo kujitokeza kwa wingi kupiga kura akisema leo ni siku ya kusherehekea demokrasia na kuamua mustakabali wa baadaye wa taifa hilo.

Wagombea wengine wa wadhifa wa waziri mkuu mbali na Netanyahu na Herzog ni Naftali Bennett ambaye Netanyahu amedokeza huenda akawa mshirika wake katika serikali ijayo, Tzipi Livni, Avigdor Lieberman, Yair Lapid na Moshe Kahlon.

Mwandishi:Caro Robi/Afp/dpa/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo