1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajerumani washerehekea taji la nne la dunia

14 Julai 2014

Ujerumani yasherehekea ubingwa wa kombe la dunia baada ya miaka 24, dhidi ya Argentina, wakati huko Argentina ulikuwa mchanganyiko kati ya machozi, sherehe na ghasia.

https://p.dw.com/p/1Ccmp
Fußball WM 2014 Brasilien Deutsche Fußballnationalmannschaft Jubel Pokal
Mabingwa wa dunia UjerumaniPicha: Reuters

Bao la Mario Goetze limeiweka Ujerumani katika historia ya kuwa timu ya kwanza kutoka bara la Ulaya kulinyakua kombe la dunia katika ardhi ya Amerika ya kusini, baada ya fainali za kombe hilo kuchezwa mara sita katika Latin America , lakini timu za bara la Ulaya zikatoka patupu. Mara hii jina la Mario Goetze litakuwa katika vitabu vya kumbukumbu , kwamba ni mchezaji aliyeiletea ushindi Ujerumani na kuandika historia mpya katika kombe la dunia.

Ujerumani inaelea katika fahari ya ushindi wa taji la nne katika kombe la dunia baada ya fainali iliyokuwa ya vuta nikuvute iliyotoa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Argentina.

Fußball WM 2014 Fans Jubel
Mashabiki wakicheza kusherehekea ushindiPicha: picture-alliance/dpa

Mashabiki wenye furaha kupindukia wa Ujerumani waliamka leo wakiwa wamevimba macho kutokana na sherehe za usiku kucha mitaani , wakifyatua fashifashi , kupiga honi za magari nchi nzima, huku mashabiki waliojawa na furaha wakiimba , " super Deutchland" huku wakiendelea kunywa na kuburudika kwa mambo mbali mbali.

Ni kweli , limeandika gazeti la kila siku la Die Welt , huku maandishi hayo yakiwa na rangi za bendera ya taifa ya Ujerumani. Kikosi hicho cha kocha Joachim Loew kitalakiwa na mamia kwa maelfu ya mashabiki kesho Jumanne mjini Berlin. Huu ni ushindi wa kwanza wa Ujerumani tangu ilipoungana tena kati ya Ujerumani mashariki na magharibi.

Gauck na Merkel wahudhuria

Pambano hilo la fainali mbele ya mashabiki 74,738 , ambao walikuwa pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel , lilionekana kuelekea kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti baada ya pande zote kushindwa kuvunja kuta ngumu za kila timu zilizokuwa makini kulinda lango wakati matokeo yakiwa sare ya bila kufungana.

Lakini zikiwa zimesalia dakika saba mpira kumalizika , Andre Schuerrle alichomoka na mpira upande wa wingi ya kushoto na kuteremsha krosi ambayo Mario Goetze aliituliza kifuani kabla ya kuachia kombora la mguu wa kushoto hadi wavuni , na kuamsha shangwe kubwa kwa mashabiki wa Ujerumani.

Fußball WM 2014 Deutschland gegen Argentinien Fans Jubel Deutschland
Mashabiki wakifurahia ushindiPicha: Matthias Kern/Bongarts/Getty Images

Ushindi wa Ujerumani ulizusha furaha kubwa kwa mashabiki wa Brazil , ambao walikuwa wakihofu uwezekano wa mahasimu wao wa Amerika kusini Argentina kushinda taji hilo katika ardhi yao.

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew amesema kuwa mafanikio haya yameanza miaka kumi iliyopita.

"Nadhani ni kazi ambayo imeanza miaka kumi iliyopita pamoja na Jurgen Klinsmann na sasa tumeikamilisha. Tumefanya kila kitu, kuweza kufikia hapa na nadhani kikosi hiki kimestahili ushindi. Hakuna mtu aliyeweza kufanikiwa kama tulivyofanya. Tunastahili kusema hivyo.Kikosi hiki kimejenga umoja zaidi katika wiki za hivi karibuni. Kimekuwa na umoja uliosababisha kupambana kuwania taji hili. Kila mmoja alikuwa na wajibu , kwa kikosi hiki na kujitolea kwa kila hali, nguvu zake zote na huu ndio msingi wa ushindi huu."

Ujerumani ilitarajia mpambano mkali na Argentina

Kuhusu timu ya Argentina kutoa changamoto kubwa kwa Ujerumani kocha Joachim Loew, amesema kuwa hilo walikuwa wakilitarajia kwasababu Argentina ni timu yenye wachezaji wazuri na wenye uzoefu mkubwa.

Fußball WM Finale Argentinien Deutschland
Joachim Loew kocha wa UjerumaniPicha: picture-alliance/AP

"Ilikuwa wazi kwetu, kwamba Argentina itatoa kila kitu na nguvu zote walizonazo katika fainali hii . Ilikuwa ni kazi ngumu. Wachezaji walifikishwa ukingoni kabisa mwa uwezo wao. Wamejitolea kila wanachokiweza leo, ili kuweza kufikia lengo, ambalo hawajawahi kulifikia , ambalo ni taji hili na kulipeleka nyumbani."

Nahodha wa Die Mannschaft , timu ya Ujerumani Philipp Lahm amewamwagia sifa wenzake katika kikosi hicho na kusema haamini kile walichoweza kukifanikisha. Iwapo wana wachezaji mmoja mmoja wenye vipaji hii haina maana tena. Unahitaji tu kuwa na kikosi kizuri, amesema nahodha huyo wa Ujerumani Philipp Lahm akionekana mwenye furaha.

"Inashangaza , kile tulichokifanya katika muda wa dakika 120.Jinsi tulivyopambana kama timu. Kama vile tulivyoona wachezaji wa akiba wakiingia , inashangaza. Hii inaonesha uwezo wa timu hii. Iwapo ni kwamba tunawachezaji binafsi wazuri hilo halina maana kwa sasa . Ni lazima uwe na timu nzuri na hilo limeonekana katika mashindano haya. Tumepandisha kiwango chetu, hatukutetereka katika wakati wa matatizo, tuliendelea tu na utaratibu wetu na tumeweza hatimaye kuwa mabingwa wa dunia."

Mchezaji wa kati wa Ujerumani Bastian Schweinsteiger amezungumzia kujitolea kwa moyo wote na uwezo wote kufanikisha lengo kama hili muhimu maishani.

"Si rahisi kushiriki kila mara katika mchezo kama huu maishani mwako na hata iwapo una pata maumivu ya misuli ama umefanyiwa madhabi. Na hilo halikunitokea mimi pekee, lakini kila mmoja wetu. Ni uwezo wa hali ya juu tuliouonesha , lakini kama ilivyokuwa kwa wachezaji waliokuwa wa akiba walivyofanya. Hili sijawahi kuliona kabisa. Hii inatia moyo sana na ndio sababu tumeweza kunyakua taji hili."

Fußball WM 2014 Finale Argentinien Deutschland
Huraaah Ujerumani imekuwa bingwaPicha: Reuters

Mlinzi wa kati wa Ujerumani Mats Hummels amesema kuanguka ama kushinda ni kazi ya timu iliyo pamoja.

"Unaweza kushinda kombe la dunia, iwapo timu inacheza kwa umoja. Hilo ndio tulilolisema kabla , na kuweka wazi kwa kila mmoja, na na hilo ndio tulitaka kuliweka wazi na ndio tulivyoweza kutimiza. Na leo katika mchezo huu ambao ulikuwa nguvu sawa , huenda bahati ilikuwa upande wetu , ndio sababu hatukuwa na matatizo."

Rais wa Ujerumani Joachim Gauck ameipongeza timu ya taifa kwa kunyakua taji hilo la nne, akiwa pamoja na kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambapo walikwenda mjini Rio de Janeiro kushuhudia fainali hiyo katika uwanja wa Maracana.

"Kikosi hiki kimefanya kazi nzuri sana.Kina nyota wengi na pamoja na hayo kimekuwa timu moja, sio kila mmoja anaweza kufanya hivyo. Nawapongeza sana. Na shirikisho la soka la Ujerumani pia nalipongeza. Kikosi hiki hakina tu nyota lakini pia wachezaji kandanda wengi , ambao wanacheza katika vilabu nchini Ujerumani na kuonesha mchezo mzuri kama walivyofanya hapa. Nimefarijika sana kwa hilo. Nawashukuru Wabrazil, na wanashukuru mashabiki wa Ujerumani , ambao wamekuja hapa Brazil , natoa shukurani zangu kwa kikosi hiki."

Fußball WM 2014 Finale Argentinien Deutschland
Rais wa Brazil Russef (kushoto na kansela wa Ujerumani Merkel (kulia)Picha: Reuters

Mashabiki wakesha mitaani

Mashabiki walikesha mitaani , mikahawani na mabaa wakisherehekea usiku kucha , na mjini Berlin hakukuwa na kitu cha kuwanyamazisha mashabiki ama kuwazuwia. Eneo la mashabiki kukusanyika lilikuwa limejaa kabla ya mchezo huo mjini Berlin , na haya yalikuwa matarajio yao wakati wa mchezo .

"Tulikuwa tuna matumaini, na tumeweza kufanikiwa. Sikuwa na shaka kwamba Ujerumani ingeshinda . Tangu mwanzo tumesema , Ujerumani itakuwa mabingwa wa dunia."

Timu ya Ujerumani inarejea nyumbani kesho asubuhi na kuanzia saa tatu asubuhi majira ya Ulaya ya kati mjini Berlin kutakuwa na sherehe kubwa ya kuwapokea na kuwatambulisha mabingwa hao wa dunia.

Watayarishaji wa kombe la dunia nchini Brazil wanaweza sasa kusema , kila kitu kimekwenda vizuri, licha ya kuwa watu wengi walikuwa wakihofia kuwa fainali hizi hazitakuwa za mafanikio.

Mchezaji maarufu wa zamani wa Argentina amelishutumu shirikisho la kandanda duniani FIFA kwa uamuzi wa kumzawadia Lionel Messi tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo. Maradona amesema "naweza kumpa Messi pepo," lakini kama sio halali na watu wa biashara wanataka ashinde kitu ambacho hajawahi kupata , hili si jambo zuri. Manuel Neuer mlinda mlango wa Ujerumani amekuwa mlinda mlango bora wa mashindano hayo, na James Rodriguez wa Colombia amekuwa mfungaji bora kwa kupachika mabao 6 katika fainali hizi.

Na mashabiki nchini Argentina walionekana kutitirikwa na machozi, wengine wakishangiria na hata ghasia baada ya ndoto yao kuwa mabingwa wa dunia kuzimwa na Ujerumani. Mamia kwa maelfu ya wapenzi wa kandanda walimiminika katika uwanja wa Obelisk mjini Buenos Aires, wakipepea bendera ya taifa na kufyatua fashifashi na kuimba nyimbo za kumsifu shujaa wao wa taifa Lionel Messi na timu yao.

Licha ya kufungwa bao 1-0 na Ujerumani , vijana walipanda katika nguzo za taa wakiimba na kupiga ngoma. Lakini furaha hiyo ilibadilika kuwa ghasia baada ya kundi linalofahamika kama "Barra Brava" kuanza kurusha mawe dhidi ya polisi wa kuzuwia ghasia , ambao nao walijibu kwa kufyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi na mabomba ya maji. Ghasia hizo zilisababisha familia zilizokuwa na watoto kukimbilia kujihifadhi katika mikahawa na hoteli za karibu.

WM 2014 Spiel um Platz drei Brasilien Niederlande
Kocha wa Brazil Felipe ScolariPicha: Reuters

Nalo shirikisho la kandanda nchini Brazil limesema leo kuwa halitarefusha mkataba na kocha wa taifa Luiz Filipe Scolari , baada ya mabingwa hao mara tano kugaragazwa na Ujerumani kwa mabao 7-1 katika ardhi yake.

Taarifa hizo za hali ya baadaye ya Scolari zilipatikana usiku wa manane jana Jumapili , saa chache baada ya Ujerumani kutawazwa mabingwa wa dunia mwaka 2014 baada ya kuishinda Argentina mjini Rio de Janeiro.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman