1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Afghanistan yafanya mazungumzo na Taliban

8 Julai 2015

Maafisa wa Afghanistan na wawakilishi wa Taliban wamekutana usiku wa kuamkia leo mjini Islamabad, kwa mazungumzo ya kwanza rasmi kuwahi kuandaliwa katika kipindi cha miaka miwili

https://p.dw.com/p/1FutQ
Pakistans Premier Sharif mit afghanischem Präsidenten Ghani in Kabul
Picha: AFP/Getty Images/S. Marai

Baada ya mazungumzo hayo, washiriki walikubaliana kukutana tena baada ya kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Pakistan iliandaa mkutano huo katika hatua ya mwanzo kuelekea kumaliza zaidi ya miaka 13 ya vita katika nchi jirani Afghanistan, ambapo kundi la Taliban limekuwa likipigana na serikali likiwa na matumaini ya kuuweka tena utawala wake wa kiislamu wenye itikadi kali ambao uliangushwa na operesheni ya jeshi iliyoongozwa na Marekani mwaka wa 2001.

Duru ijayo ya mikutano imepangwa kuandaliwa Agosti 15 na 16 mjini Doha, mji mkuu wa Qatar, kwa mujibu wa duru za karibu na washiriki wa mazungumzo hayo. Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif aliyasifu mazungumzo hayo kuwa ya “mafanikio makubwa”. Lakini bado haiwezi kujulikana ikiwa mchakato huo unaweza kumaliza mapigano yanayoendelea Afghanistan, kutokana na hali kwamba uongozi wa Taliban umegawika kuhusu suala la mazungumzo na makamanda kadhaa tayari wameasi na kujiunga na kundi hasimu la jihadi, linalojiita Dola la Kiislamu - IS.

Afghanistan Explosionen und Schüsse am Parlament in Kabul
Taliban ililishambulia kwa bomu bunge la Afghanistan mjini Kabul, mnamo Juni 22Picha: Reuters/M. Ismail

Maafisa kutoka Marekani na China walikuwa waangalizi katika mazungumzo hayo yaliyoandaliwa jana katika eneo la mapumziko la milima, Murree, viungani mwa mji mkuu wa Pakistan, Islamabad. Msemaji wa Ikulu ya Rais nchini Marekani Josh Earnest amesema Marekani imeyakaribisha mazungumzo hayo aliyosema ni hatua muhimu kuelekea kuongezeka uwezekano wa kupatikana amani ya kudumu "Tunatambua na kushukuru juhudi muhimu za Pakistan kuandaa mazungumzo haya. Marekani imekuwa ikiwahimiza waafghanistan kushiriki katika mchakato unaoongozwa na nchi hiyo utakaoleta maridhiano ya kisiasa na kusitishwa machafuko ambayo yameikumba nchi hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa. Ni mchakato ambao tutaendelea kuunga mkono na sharti uongozwe na watu wa Afghanistan na serikali ya Afghanistan".

Taarifa ya wizara ya mambo ya kigeni ya Pakistan imesema washirika walikubaliana kuendelea na mazungumzo ili kuweka mazingira bora ya mchakato wa amani na maridhiano.

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani, ambaye ameshinikiza kuanzishwa mchakato wa amani na kuhimiza mahusiano ya karibu na nchi jirani Pakistan katika juhudi za kutimiza lengo hili, alitangaza jana kwa mara ya kwanza kuhusu mkutano huo.

Katika miezi kadhaa iliyopita, kumekuwa na mazungumzo ya mwanzo yasiyo rasmi kati ya wawakilishi wa Taliban na viongozi wa Afghanistan, lakini mazungumzo ya jana yalikuwa ya kwanza rasmi.

Msemaji rasmi wa Taliban katika siku za nyuma alikanusha kuwepo mchakato wowote wa amani, akisema wale wanaokutana na serikali ya Afghanistan hawaruhusiwi kufanya hivyo.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Caro Robi