1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wajumbe wa FIFA kumchagua rais mpya

Oummilkheir Hamidou26 Februari 2016

Shirikisho la Kandanda Ulimwenguni (FIFA) linakabiliwa na siku muhimu katika historia yake ya miaka 112, litakapomchagua rais wake mpya katika ukumbi wa mikutano mjini Zurich, Uswisi.

https://p.dw.com/p/1I2kj
Hallenstadion utakakofanyika mkutano mkuu wa FIFA mjini Zurich.Picha: picture-alliance/dpa/P.Seeger

Wajumbe kutoka zaidi ya nchi 200 wanamchagua rais mpya atakayeshika nafasi ya Sepp Blatter, siku mbili baada ya raia huyo wa Uswisi na mgombea mwengine, mkuu wa Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA), Mfaransa Michel Platini, kukataliwa rufaa zao na korti ya maadili ya FIFA.

Masuala kadhaa yanajitokeza:watamchagua nani kurithi nafasi inayoachwa na Joseph Blatter baada ya miaka 17 kama rais wa FIFA? Vipi shirika la FIFA linaloandamwa kisheria na hadhi yake kuchujuka kutokana na madai ya rushwa, litaweza kukabiliana na changamoto hizo kubwa kuwahi kushuhudiwa tangu shirikisho hilo lilipoanzishwa?

Kwa vyovyote vile, atakayemrithi Blatter atakuwa na kazi ngumu kuliongoza shirikisho hilo baada ya maafisa wake kadhaa kushitakiwa Marekani kwa madai ya udanganyifu, kubadilisha fedha kinyume cha sheria na rushwa.

Mkutano mkuu wa FIFA wafunguliwa

Katibu Mkuu wa muda wa FIFA, Markus Kattner, ameufungua hivi punde mkutano mkuu utakaopelekea kuchaguliwa rais mpya. Kati ya wagombea watano, wawili wanapigiwa upatu wa kuwa na nafasi nzuri ya kushinda; Sheikh Salman mwenye umri wa miaka 50, ambaye ni rais wa shirikisho la kabumbu la Asia na mwanasheria wa Uswisi mwenye asili ya Italia, Gianni Infatino, mwenye umri wa miaka 45 na ambaye ni Katibu Mkuu wa UEFA.

Wagombea wengine watatu ni pamoja na mwanamfalme Ali wa Jordan, mfaransa Jérome Champange, naibu katibu mkuu wa zamani wa FIFA na mfanyabiashara wa Afrika Kusini, Tokyo Sexwale, aliyesema jana yuko tayari kushirikiana na Infantino.

Schweiz Zürich FIFA Außerordentlicher Kongress Thomas Bach
Thomas Bach akifungua mkutano mkuu wa dharura wa FIFA mjini ZurichPicha: Reuters/R. Sprich

Marekani, Australia kumuunga mkono Mwanamfalme Ali wa Jordan

Uamuzi wa Australia unakwenda kinyume na msimamo wa Shirikisho la Kabumbu la Asia (AFC) lililotangaza kuwa nyuma ya mgombea wake Sheikh Salman. "Kwa vyovyote vile, Shirikisho la Kabumbu la Australia (FFA) linahisi wana kila sababu ya kuendelea kumuunga mkono Mwanamfalme Ali," alisema mwenyekiti wa shirikisho hilo, Steven Lowy katika taarifa yake.

Rais wa Shirikisho la Kabumbu la Marekani, Sunil Gulati, naye pia alisema shirikisho lake litamuunga mkono Mwanamfalme Ali wa Jordan.

Rais mpya wa FIFA atachaguliwa leo jioni, ambapo kila mjumbe ana kura moja tu, ama awe anatokea katika nchi kubwa ama ndogo.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Josephat Charo