1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakazi warejea polepole Bonde la Swat

14 Julai 2009

Mapigano mapya dhidi ya Wataliban yameua zaidi ya wanamgambo 30 nchini Pakistan. Wakati huo huo serikali inajaribu kuwarejesha makwao wakazi waliyokimbia mapigano katika la Bonde la Swat .

https://p.dw.com/p/IpF7
Map of Pakistan's Swat Valley, once known for tourism, and now affected by Taliban militancy
Ramani ya Bonde la Swat lililokumbwa na machafuko ya wanamgambo wa Taliban.Picha: Faridullah Khan

Mapigano hayo yalitokea Jumatatu usiku katika kijiji cha Anbar kaskazini-magharibi ya Pakistan,baada ya wanamgambo wa Kitaliban kukataa kuondoka licha ya kufukuzwa na wanavijiji wa eneo hilo. Mapambano makali yaliyozuka yameua wanamgambo 23 na wenyeji 3 walijeruhiwa kwa risasi. Isipokuwa kwa wanamgambo 5 waliotokea wilaya ya mashariki-Punjab- wote wengine ni kutoka eneo hilo la mvutano kaskazini-magharibi ya nchi. Waasi wengine 5 waliuawa katika eneo la Kuza Banda huko huko Swat baada ya kupambana na vikosi vya usalama. Wanne wengine waliuliwa katika vijiji vya Tahirabad na Billogram.Serikali ya Pakistan inawahimiza wenyeji kuchukua hatua dhidi ya waasi katika maeneo hayo ya machafuko ambako wakuu wa kikabila wana ushawishi mkubwa. Na sasa wanavijiji ndio wameanza kuwashambulia wanamgambo wa Taliban.

Wakati huo huo majeshi ya serikali yanaimarisha operesheni zake kuzima uasi katika Bonde la Swat na maeneo ya jirani na imefanikiwa kudhibiti sehemu kubwa katika eneo hilo. Zaidi ya waasi 1,700 na takriban wanajeshi 160 wameuawa katika operesheni iliyoanza zaidi ya miezi miwili iliyopita.Sasa upinzani wa waasi ukiendelea kupunguka,serikali imeanzisha mpango wa kuwarejesha nyumbani takriban wakazi milioni 2 waliokimbia mapigano. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, katika siku mbili za mwanzo, kiasi ya familia 3,000 - kila moja ikiwa na kama watu saba- zimerejea nyumbani. Lakini mpango huo unakwenda pole pole kinyume na vile ilivyotarajiwa. Sababu kuu ni wasiwasi kuhusu hali ya usalama watakaporejea nyumbani.

Kwa upande mwingine serikali ikikaribia kukamilisha operesheni yake katika Bonde la Swat, majeshi yake sasa yanajiandaa kumsaka kiongozi mkuu wa kundi la Wataliban nchini Pakistan Baitullah Mehsud katika Wilaya ya Waziristan ya Kusini. Eneo hilo linajulikana kama ni kitovu cha wanamgambo wa Al-Qaeda.Operesheni za Pakistan kupambana na ugaidi katika maeneo hayo ya machafuko zimesifiwa na Marekani na nchi za magharibi. Kwani maeneo hayo ya mpakani yanatumiwa na wanamgambo wa Taliban kushambulia vikosi vya kimataifa nchini Afghanistan. Kwa mfano leo tanki lililokuwa likisafirisha petroli kwa majeshi ya NATO yaliyo Afghanistan, lilivamiwa na kuteketezwa na wanamgambo katika barabara kuu inayoziunganisha Pakistan na Afghanistan. Mapigano yaliyozuka yameua raia wawili na wengine watatu wamejeruhiwa.Barabara hiyo hutumiwa kusafirisha chakula na zana za kijeshi kwa vikosi vya kimataifa huko Afghanistan. Mara kwa mara, magari yanayopeleka misaada Afghanistan na hata viwanja vya kuegeza magari hayo hushambuliwa na wanamgambo.

Mwandishi: P.Martin (DPAE/AFPE)

Mhariri: Miraji Othman