1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakenya kuruhusiwa kufanya kazi nchi za Ghuba

Fathiya Omar10 Januari 2018

Kenya inakusudia kuondoa marufuku kwa wananchi wake kufanya kazi katika nchi za Ghuba iliyotolewa mwaka 2014 kwa sababu ya unyanyasaji. Lakini bado kuna hofu mpya za unyanyasaji kwa wahamiaji huko Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/2qcwA
Wanawake wanaofanya kazi za ndani mara nyingi huteswa
Picha: Imago/UIG

Akifanya kazi kama mwalimu wa watoto watatu kutoka  familia tajiri huko nchini Qatar, Wairimu, mhamiaji kutoka Kenya, hakutarajia kwamba hatua ya mwajiri wake ya kumpeleka kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu ilikuwa mbinu ya kumpokonya pasipoti yake. Miezi mitatu baadaye, mwanamke huyo amekwama, wala hajui cha kufanya, kwa sababu bado hajakuwa na ujasiri wa kumwomba mwajiri wake amrudishie hati hiyo ili apate kuacha kazi yake.

Wairimu aliliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kutoka mji mkuu wa Doha kuwa, amekwenda Qatar kwa ajili ya kazi ya ualimu lakini mwajiri wake anamtaka afanye kazi za nyumbani na bado asaidie watoto na kazi zao. Kulingana na Wairimu, hizo ni kazi nyingi sana kwake.

Hakuna njia ya kutoroka

Anaendelea kusema, "Bila pasipoti, siwezi kupata kazi wala  kusafiri kwenda nyumbani. Mwajiri wangu pia amegeuka kuwa mkali na mjeuri kwangu kwahiyo imekuwa vigumu kwangu hata kumkaribia."

Haya yanajiri wakati Kenya inakusudia kuondoa marufuku iliyoiweka mwaka wa 2014 kwa wananchi wake kufanya kazi katika nchi za Ghuba –kukiwa na  hatua mpya za kinga, kama vile mawakala wa kusafirisha watu kwenda nchi za ghuba  watahitajika kulipa dhamana ya usalama ili waweze kuwarejesha nyumbani mhamiaji yeyote wenye shida.

Lakini wataalam wanahofia kwamba sheria hiyo mpya haitawakinga wahamiaji huku kukiwa na rushwa, tamaa na haja kubwa ya maisha bora zaidi. Wakishawishiwa na ahadi za kazi zenye malipo bora ughaibuni na nafasi ya kutoroka ukosefu wa kazi nyumbani, mamia kwa maelfu ya Wakenya wanakisiwa kuajiriwa katika Mashariki ya Kati, wakituma misaada inayohitajika kwa familia zao kila mwaka.

Wanawake waandamana kutetea haki za wafanyakazi wa ndani
Wanawake waandamana kutetea haki za wafanyakazi wa ndani Picha: picture-alliance/dpa/J. Favre

Kulingana na wanaharakti, Wafanyakazi wa nyumbani mara nyingi wanafungiwa na mwajiri, wakilazimishwa kufanya kazi zaidi ya saa 18 kwa siku, wakinyimwa chakula na mshahara na kunyanyaswa kimwili na kijinsia.

Sheria za udhamini wa Visa huko Qatar, inayojulikana kama mfumo wa kafala- inayotumika katika nchi nyingi za Kiarabu za Ghuba – ina maana ya wafanyakazi kutoka nje kama Wairimu hawawezi kubadili kazi bila idhini ya mwajiri wao na wanaweza kushtakiwa kwa kukwepa majukumu yao ikiwa watakimbia.

Kenya ilisaini mikataba ya kazi na nchi mbili  Qatar na Saudi Arabia mnamo Novemba, ikiahidi usalama wa wafanyakazi wakenya katika nchi hizo mbili, na kutoa leseni kwa  mawakala 29 nchini Kenya  wa kusafirisha watu kufanya kazi katika nchi za ghuba Mashirika yote yalipoteza leseni zao katika msako wa mwaka wa 2014.

Makundi ya kutetetea haki yaliipongeza hatua hii.

Mashirika hayo lazima yawe na ofisi maalum na kuwasilisha Ripoti kila baada ya miezi mitatu kwa serikali kuhusu wahamiaji wao walioko nje ya nchi. Aliyekuwa waziri wa leba Phyllis Kandie alisema wakati akitaja majina ya mashirika mapya yaliosajiliwa.

Alisema mashirika pia yanapaswa kulipa dhamana ya usalama ya kiasi cha shillingi  500,000 hadi milioni 1.5 shilingi za Kenya kwa serikali kuwarudisha wafanyakazi wakati wa dharura.

"Wizara yakazi inatusaidia kuelewa kanuni mpya na umuhimu wake," amesema Suzan Ngosho, ambaye anafanya kazi kwa Shirika la kusafirisha watu kufanya kazi nje la Derimel, mojawapo ya makampuni yaliopewa leseni.

Lakini hatua zaidi zinahitajika kuwalinda wahamiaji, alisema Rothna Begum, mtafiti wa haki za wanawake katika Shirika la Human Rights Watch.

Alisema, "Mamlaka lazima ziweke usalama zaidi, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha haki kwa upande wa mafunzo ya kabla ya kusafiri ambapo watu wanafundishwa haki zao na wapi watafute  msaada na ujuzi wa lugha ili kuwasaidia kuwa na  mawasiliano. Hatua  nyingine nzuri itakuwa kuanzisha mikataba mizuri na nchi za Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na viwango  mishahara, na hakikisho  kuwa nchi wanazokwenda zitaujulisha ubalozi wa Kenya wakati wafanyakazi wahamiaji wanapotafuta msaada au kama wamekamatwa."

Lakini kwa Wairimu, suluhisho liko nyumbani, anasema: "Matumaini yangu ni kwamba serikali itaunda fursa zaidi za kazi ili tuweze kurudi nyumbani - kwa sababu hatuwezi kuhakikishiwa usalama wetu tunapoendelea kuwa katika nchi za watu."

Mhariri: Fathiya Omar/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman