1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Congo, waendelea kuombolezwa kutekwa kwa watoto wao.

Nyanza, Halima20 Oktoba 2008

Wakati amani bado haijapatikana kaskazini mwa Uganda, wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, bado wanaendelea kuomboleza kutekwa kwa watoto wao na Waasi wa Uganda wa kundi la Lord Resistance Army LRA.

https://p.dw.com/p/FdM2
Mmoja wa askari watoto wa kundi la waasi wa Uganda wa Lord's Resistence Army, ambapo wakimbizi wa Kikongo wamelaumu waasi hao, kuwanyakua watoto wao na kuwafanya wapiganaji.Picha: AP

Kwanza, waasi hao wamekuwa wakiwafungia watoto wanapokuwa shuleni katika maeneo ya vijiji, Halafu kuwaua watu wazima wote wanaowapinga, kuwanyima uhuru wengine, kuchoma nyumba za makuti pamoja na kuharibu maghala ya vyakula.

Waasi hao wa LRA, wanadaiwa kuwakamata watoto wa kikongo kutoka madarasani na kutoroka nao msituni kuwafanya wapiganaji.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya wanavijiji kukimbia makazi yao, mfano ni Mary, mama wa mtoto wa mwaka mmoja kutoka katika jamii ya Dungu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yeye alikimbilia kusini mwa Sudan wiki mbili zilizopita.

Mkurugenzi wa taasisi moja inayoshughulika na wakimbizi katika eneo la Equatoria magharibi, Sudan ya kusini, Lexson Wali Amozai ambaye pia ni mratibu wa juhudi zinazofanywa na Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada kusaidia watu wasio na makazi kutokana na kukimbia mashambulio, anasema mateso wanayotoa waasi hao kwa watu,sio ubinadamu.

Anaeleza kuwa waasi hao wa LRA, wamekuwa wakiteketeza maisha ya watu wanaoishi kwa amani.

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, mapema mwezi huu imewashutumu wapiganaji hao wa kaskazini mwa Uganda kwa vitendo vya ukiukaji haki za binadamu dhidi ya jamii zinazozunguuka eneo hilo.

Karibu wakimbizi elfu tano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamekimbilia kusini mwa Sudan, lakini mashambulio yanayofanywa na waasi hao, yamewaacha pia wengine kadhaa kutokuwa na makazi ndani ya nchi yao.

Aidha Maafisa nchini humo wanakadiria kuwa zaidi ya watoto mia moja wametekwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na wengine mia kusini mwa Sudan.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mkazi wa maeneo hayo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yaliyovamiwa na waasi wa LRA, John Karyami mtoto yoyote atakayekamatwa na waasi hao katika ardhi hiyo wanasema kuwa ni wao na wanamchukua na kwamba mtu mzima yoyote watamkamata ama kumuua.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, waasi hao wa Uganda waliingia katika misitu ya mbali kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemopkrasi ya Kongo na pia kuingia katika mpaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan kusini.

Waasi hao wa LRA, ambao pia wamekuwa wakifanya mashambulizi kuelekea Sudan, wamesababisha pia mamia ya watu kukimbia makazi yao katika eneo la Sudan ya kusini.

Mkurugenzi wa taasisi moja inayoshughulika na wakimbizi katika eneo la Equatoria magharibi, Sudan ya kusini, Lexson Wali Amozai anasema waasi wa LRA, wamekuwa wakiwafanyia mzaha kutokana na kudai kuwa huwezi kuamua kuingia katika mazungumzo ya amani, wakati jeshi lako linashambulia watu wasio na hatia.

Naye Gavana wa jimbo la Sudan la Equatoria magharibi, ambalo liko mpakani mwa Kongo Jemma Nunu Kumba anasema watu wa huko wamekuwa wakijiuliza swali, kwanini waasi wa LRA, wamekuwa wakiwaua, kutokana na kwamba wao sio waGanda na kwamba hawahusiki na mzozo huo... Lakini hayo ni maswali ambayo hakuna mtu wa kujibu.