1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa kisomali wadhalilishwa Nairobi

29 Mei 2013

Ripoti ya Human Rights Watch iliyochapishwa Nairobi imeorodhesha visa 1000 vinavyoonyesha jinsi wakimbizi wa kisomali walivyokuwa wakitendewa maovu, wakipigwa, wakipokonywa mali zao na kubakwa na polisi ya Kenya.

https://p.dw.com/p/18gR6
Wakimbizi wa kisomali katika kambi ya DedaabPicha: Getty Images

Polisi wamevunja na kupora nyumba,wamewakamata na kuwabaka wakimbizi. Kwa mujibu wa wakimbizi polisi walikuwa wakiwaambia "Nyie wasomali ,nyote ni magaidi", hamna haki yoyote nchini Kenya". Matamshi hayo ndiyo yaliyomo ndani ya ripoti ya Human Rights Watch iliyochapishwa mjini Nairobi.Shirika hilo la haki za binaadam limezungumza na wakimbizi mia moja.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch kuanzia November 2012 hadi january mwaka huu wa 2013, wakimbizi wasiopungua elfu moja na wenye kuomba kinga ya ukimbizi kutoka Somalia na Ethiopia, na hata wakenya wenye asili ya kisomali waliangukia mhanga wa visa vya udhalilishaji kutoka vikosi tofauti vya polisi mjini Nairobi. Ripoti ya Human Rights Watch inataja aina tofauti za udhalilishaji tangu wa kimwili mpaka wa kiakili-kuanzia watu kuibiwa mali zao,kutiwa ndani kinyume na sheria hadi kufikia mateso na ubakaji."Visa hivi ni sehemu ya historia ndefu ya matumizi ya nguvu yanayofanywa na polisi na wanejshi dhidi ya wakimbizi wa kisomali na wakenya wenye asili ya kisomali.Hadi wakati huu matumizi ya nguvu yalikuwa yakitokea kaskazini mashariki ya Kenya,karibu na mpaka wa Somalia na katika kambi za wakimbizi.Hivi sasa  yameshafika Nairobi."..anasema Gerry Simpson, mwandishi mkuu wa ripoti ya Human Rights Watch.

Kama watu hawatolalamika mambo yatazidi

Human Rights Watch Logo
Nembo ya shirika la haki za binaadam la Human Rights Watch

Chanzo cha wimbi hilo jipya la matumizi ya nguvu ya polisi huenda lilikuwa shambulio dhidi ya basi dogo la usafiri katika mtaa wa Eastleigh mjini Nairobi, lililotokea Novemba 18 mwaka jana. Wasomali wengi wanaishi katika mtaa huo. Shambulio hilo lilisababisha watu sabaa kuwawa na 30 kujeruhiwa. Waliokuwa nyuma ya shambulio hilo bado hawakupatikana.

Shirika linalopigania haki za binaadam Human Rights Watch linalikosoa pia shirika la Umoja wa mataifa linalowahudumia wakimbizi UNHCR. Licha ya kwamba visa vya udhalilishaji vya polisi vimetokea karibu na ofisi yao-shirika hilo liliamua kwanza kutosema chochote. Msemaji wa shirika hilo la Umoja wa mataifa Emmanuel Nyabera anaelezea kwanini baadhi ya wakati wanaamua wasiseme kitu. Emmanuel Nyabera anasema kuna wakati wanapendelea zaidi kushirikiana na serikali ili wenyewe wapitishe uamuzi bila ya kunyooshewa kidole cha lawama.

Hata hivyo Human Rights Watch wanahisi hayo hayatoshi. Mwandishi mkuu wa ripoti ya shirika hilo la haki za binaadam Gerry Simpson anahisi polisi wanaweza kuanza tena kuwatendeya maovu  raia ikiwa watu watakaa kimya.

Mwandishi: Philipp Sandner/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed